Na Daniel Mbega, Dar es Salaam
KATI ya vitu vilivyowakera wanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM), akiwemo Mwenyekiti wa chama hicho Taifa, Dkt. Samia Suluhu Hassan, sina shaka yoyote kwamba ni kauli iliyotolewa na aliyekuwa Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Moses Nnauye.
Nape, aliyewahi kuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Halmashauri Kuu ya CCM, akiwa katika Soko la Kashai mjini Bukoba Julai 15, 2024 usiku, aliwahakikishia wananchi wa Bukoba kwamba mbunge wao, Stephen Byabato, atashinda uchaguzi wa mwaka 2025 na hakuna mwingine, kwani, alisema, siyo lazima kutegemea sanduku la kura.
Nanukuu kauli yake iliyozua taharuki: “Matokeo ya kura siyo lazima yawe yale ya kwenye box, inategemea nani anahesabu na nani anatangaza. Unajua kuna mbinu nyingi za uchaguzi. Kuna halali, nusu halali na haramu na zote zinaweza kutumika ilimradi ukimaliza unasema Mungu nisamehe.”
Mara tu baada ya kauli hiyo, wananchi, wakiwemo wanaCCM na viongozi wakuu wa chama hicho, ‘wakaikana’ kauli ya Nape na kusema ‘ni yake mwenyewe na Chama hakihusiki nayo’.
Na hata Jumapili, Julai 21, 2024 wakati Rais Samia ‘alipowaweka kando’ Nape na Byabato, ambaye alikuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, hakuna aliyeshangaa.
Kimsingi, kauli ya Nape imeonyesha kwenda kinyume na dhamira safi ya Rais Samia, ambaye amekuwa akipambania demokrasia huku akisisitiza falsafa yake ya 4R – Maridhiano, Ustahimilivu, Mabadiliko na Kujenga Upya.
Na kwa falsafa hiyo ndiyo maana akarejesha uhuru wa maoni huku akiyafungulia magazeti manne yaliyokuwa yamefutiwa usajili tangu awamu ya tano.
Lakini akafanya kile ambacho wengi hawakukitarajia baada ya kuondoa zuio la mikutano ya vyama vya siasa lililodumu kwa miaka saba.
Katika kuhakikisha demokrasia inatamalaki, Rais Samia akatimiza ahadi yake baada ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuridhia kupitishwa kwa Sheria tatu ikiwemo ya uchaguzi na vyama vya siasa, ambapo hata Tume ya Taifa ya Uchaguzi imebadilishwa.
Itakumbukwa pia kuwa, mnamo Februari mwaka huu, wakati akiwa katika sherehe za kuukaribisha mwaka mpya wa 2024 kwa Mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao nchini Tanzania pamoja na wawakilishi wa mashirika ya kimataifa zilizofanyika Ikulu, Rais Samia aliahidi kwamba uchaguzi ujao utakuwa huru na wa haki.
Na akasema, ili kuhakikisha uchaguzi huru na wa haki, Kikosi Kazi huru cha kupitia na kushauri mageuzi muhimu katika mfumo wa siasa kiliundwa na kuwasilisha ripoti yake mwaka 2023.
“Haki, demokrasia, sheria na utawala bora utadumishwa kwa watu wote wakati wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu,” alisema Rais Samia.
Rais Samia pia akasema mapendekezo mengi ya Kikosi Kazi hicho yaliyopokelewa na serikali na wadau wote yalihusu kuongeza uwazi katika michakato ya uchaguzi ikiwa ni pamoja na uteuzi wa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi.
Kwa maana hiyo, kilichofanywa na kada kama Nape kwa kauli iliyozua taharuki ni Dhahiri kilikuwa kinapingana na dhamira ya dhati aliyonayo Rais Samia.
Kimsingi, kauli hizi za makada zinamfanya Rais Samia, na kwa kofia nyingine kama Mwenyekiti wa CCM Taifa, kuwa na mzigo mzito katika kujenga demokrasia nchini ambayo inazingatia uwazi na kujenga umoja, amani na mshikamano.
Wakati Rais Samia anarejesha umoja wa kitaifa, sote tunapaswa kumuunga mkono, lakini wanapotokea viongozi wengine wa chini yake wanatoa kauli zinazoonyesha kukinzana na maono yake, hali inakuwa ngumu kuanza tena kuwaaminisha wananchi kwamba, kauli hiyo siyo ya taasisi bali ya mtu mmoja.
Jumuiya za kimataifa zinaamini kwamba, chini ya utawala wa Rais Samia, mambo mengi yamebadilika, na tunashuhudia hata uungwaji mkono anaoupata katika mataifa ya nje kila anakokwenda.
Mnamo Alhamisi, Januari 18, 2024, Rais Samia Suluhu Hassan alikemea mwenendo wa wanachama wa CCM wanaofanyiana hujuma kwenye nafasi za uchaguzi wakati akizindua tawi la Tasani Makunduchi lililopo Wilaya ya Kusini, Mkoa wa Kusini Unguja.
Rais Samia aliwaonya wanaCCM waache tabia ya kuhujumiana wakati wanapoelekea kwenye chaguzi mbalimbali, ukiwemo wa Serikali za Mitaa utakaofanyika baadaye mwaka huu na Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025.
“Mwakani Taifa linaingia kwenye uchaguzi, hivyo rai yangu kwa wanaCCM ni kutohujumiana, na kuwapa nafasi wenye sifa na wachapakazi huku wakihakikisha wanakivusha chama ili kiendelee kuwatumikia Watanzania na kuwaletea maendeleo,” alisema.
Rai hiyo ilikuwa ya pili kutolewa na Rais Samia ndani ya siku mbili, kwani Jumatano, Januari 17, 2024 wakati akifungua Tawi la CCM Chaani Masingini, Wilaya ya Kaskazini A katika Mkoa wa Kaskazini Unguja, alionya wanaowania ubunge na uwakilishi pamoja na udiwani kutotumia rushwa kupata uongozi.
Akawaonya pia wananchi kutokubali kuhadaiwa kwa kupewa khanga, vitenge na Shs. 10,000 ili kuwapa kura wanaogombea nafasi mbalimbali huku akisisitiza kwamba, wagombea wote watapimwa kulingana na kazi zao na kwamba mchujo utaanza kulingana na kazi walizofanya.
Amekomesha ‘zabuni’ ya uongozi
“Nataka kuona tathmini ya kila mbunge, mwakilishi kwa alichofanya, na ninyi mnaokwenda kuchagua wapimeni hawa kwa kazi walizozifanya. Muache ule mtindo wa kutembezewa kkanga, vitenge na Shs. 10,000 ndani, anayefanya hivyo maana yake hakufanya kazi yake, anawapa hongo mumchague,” Rais Samia alisema akiwa Chaani Masingini.
Akaonya wanaotumia fedha za zawadi kusaka kura waache mara moja, kwani vitendo hivyo haviwezi kutoa viongozi bora wenye kujali maslahi ya wananchi.
Oktoba 2023 Serikali iliwasilisha Bungeni miswada kadhaa ya Sheria zinazohusiana na uchaguzi kwa lengo la kuhakikisha kwamba chaguzi zinaendelea kuwa huru na haki na kukomesha vitendo vya rushwa kwenye uchaguzi ambavyo vinadhulumu haki za msingi za Watanzania wenye sifa za uongozi.
Pia vitendo hivyo vinadhulumu haki za Kikatiba za wananchi kuwachagua viongozi wanaowataka kwa sababu tu ya shinikizo la rushwa.
Miswada iliyowasilishwa Bungeni ambayo imeshapitishwa kuwa Sheria ni pamoja na wa Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya Mwaka 2023, Sheria ya Tume ya Uchaguzi ya mwaka 2023 na Sheria ya Marekebisho ya Sheria za Vyama vya Siasa ya Mwaka 2023.
Lakini pia ikumbukwe kwamba kuna Sheria ya Gharama za Uchaguzi ya Mwaka 2010 na marekebisho yake ya Mwaka 2015, ambayo kimsingi inaelekeza wagombea na vyama vya siasa kuainisha vyanzo vyao vya fedha za kampeni na namna ya kuzitumia. Hii haitoi fursa ya kutumia fedha ‘kununua’ kura.
Ipo pia Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, ambayo inaainisha sifa za wanaohitaji kuwania uongozi wa Serikali za Mitaa kuanzia kwenye Vitongoji, Vijiji na Mita.
Kauli ya Rais Samia haikuja kwa bahati mbaya, kwa sababu kwa miaka mingi kumekuwepo na malalamiko mengi kuanzia ndani ya CCM kwamba rushwa – ambayo ilibatizwa majina mengi kuihalalisha – ilikuwa imetamalaki nchini na kuwa sumu mbaya katika uchaguzi ulio wazi na wa haki.
Siyo siri, kwamba rushwa na ufisadi ni vitu ambavyo vilikuwa vinatishia uhai wa CCM kiasi kwamba kulikuwa na jitihada ambazo zingeweza kukizamisha chama hicho, ingawa ziligonga mwamba, japokuwa zinaendelea chini kwa chini.
Uwepo wa makundi au kambi ndani ya Chama ndio huzalisha rushwa na ufisadi kwa sababu makundi hayo siyo tu kwamba hutumia ushawishi wa kisiasa, bali mabilioni ya fedha hutumika kuhakikisha yanaungwa mkono ili kutimiza malengo yao.
Mara tu baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 kulikuwa na tetesi nyingi kwamba ‘mradi mkubwa’ wa wanachama na viongozi kuhama chama hicho ulikuwa umeiva. Mradi huo uliwahusisha wanachama wote waliokuwa kwenye kambi za vigogo wa chama hicho waliokuwa wakituhumiwa kwa ufisadi.
Jitihada za kuwashinikiza waasi hao waondoke haraka ndani ya chama hata kupitia uamuzi wa ‘Kujivua Gamba’ hazikuweza kusaidia, ingawa tetesi ziliendelea kuwataja baadhi ya vigogo hao ‘wakifunga mikataba’ na baadhi ya vyama ama viongozi wa vyama vya upinzani na kwamba tayari walikuwa wamewatanguliza ‘watu wao’ kwenye vyama hivyo.
Zoezi la kujivua gamba liliposhindikana, ikabidi baadhi ya vigogo ndani ya chama, wale ‘watuhumiwa’ waliotajwa ndani ya chama na hata nje, waamue kujizatiti kwamba hawataondoka kamwe.
Mkakati wao mkubwa ulikuwa wa mwaka 2012 wakati wa Uchaguzi wa Chama ambapo vigogo hao walihakikisha wanaimarisha mtandao wao kwa kusimika watu wao kuanzia ngazi ya chini kabisa hadi taifa.
Rushwa ya mabilioni ya fedha ilitumika na ilikuwa nje nje kiasi kwamba Dodoma ilibadilika ghafla hata wakati wa uchaguzi wa ngazi ya taifa, ambapo watu walikuwa wakiwatumia mafundi viatu, wauza magenge na mama lishe kupitisha rushwa hiyo kwa watu wao (wapiga kura) kuhakikisha mkakati wao unafanikiwa.
Mbinu hiyo ilifanikiwa, lakini ilionekana kama Chama hakikuwa na uthubutu wa kuwaadhibu wahusika, hali ambayo iliendelea kukidhoofisha kwa kuwa rushwa na ufisadi ni kinyume na misingi ya CCM na ilishangaza ni kwa vipi viongozi walishindwa kuwawajibisha.
Yalisemwa mengi ndani na nje ya CCM, baadhi wakayabeza na kuyadharau, lakini yalidhihirika mwaka 2015 wakati kundi kubwa la wanaCCM, wakiwemo wenyeviti wa Chama wa Mikoa, walipoamua kumfuata Edward Lowassa kujiunga na upinzani, hususan Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Ndilo kundi hilo hilo ambalo lilitaka kuleta fujo wakati wa uteuzi wa mgombe urais kupitia CCM Julai 11, 2015 pale Dodoma kiasi cha kuanzisha mapambio ndani ya ukumbi huku uongozi wa juu ukiwaangalia tu.
Tena ni kundi hilo hilo ambalo ilielezwa lilikuwa limewakusanya vijana takriban 400, wakiwemo wanafunzi wa vyuo vikuu, kwenda Dodoma ili kuanzisha maandamano endapo Lowassa angeshindwa kupitishwa kuwa mgombea urais.
Baada ya vyombo vya ulinzi na usalama kuwadhibiti vijana hao, bado hawakuacha kuwashawishi wanafunzi kadhaa wa vyuo vya mjini Dodoma kutaka kuanzisha fujo nje ya ukumbi, jambo ambalo pia lilidhibitiwa ipasavyo.
Lakini makandokando yale yaliendelea kubakia ndani ya CCM licha ya kundi kubwa kuondoka, ambapo waasi hao ndio waliokuwa wakivujisha siri za chama na mikakati yote ya kampeni kupeleka upinzani.
Hatimaye CCM ikawafagia. Wakaondoka. Ingawa uchunguzi unaonyesha kwamba, bado tu wapo baadhi yao ambao wamesalia. Na wanazidi kukita mizizi yao tangu kilipotokea kifo cha Rais John Magufuli mwaka 2021, ambapo baadhi walipinga na hawakutaka Katiba ichukue mkondo wake.
Kwamba, Samia Suluhu Hassan, ambaye alikuwa Makamu wa Rais na Kikatiba ndiye aliyekuwa anastahili, asiapishwe kuwa Rais wa Awamu ya Sita.
Yaliyoendelea wengi wameyaona, waliopinga wakajitokeza bila kutarajia. Mfumo ukawazima ingawa bado wanahisi kuwa wana nguvu.
Hata hivyo, juhudi za kudoofisha CCM zimekuwa hafifu kwa maana kwamba hoja hazijawa thabiti na wengi wanaotumika na, au kutumiwa, wana sifa za uanasiasa wa magazetini, redioni na kwenye televisheni tu; siyo wana-mikakati.
Misingi iliyobomoka
Alichokisema Rais Samia Zanzibar ndicho kinachotakiwa, kwa sababu CCM ilikwishapoteza sifa kitambo na ilihitaji kujitafakari.
Kauli ya Rais Samia imekilenga chama chote, haijawalenga wagombea ubunge, uwakilishi na udiwani pekee.
Kuna biashara kubwa inayofanywa na baadhi ya wanasiasa ambao wanashirikiana na wafanyabiashara halisi wanaojificha katika mwamvuli wa ‘kukisaidia’ chama.
Wafanyabiashara walio wengi nia yao si njema bali kuficha madudu yaoni ya msingi kabisa kwa kuwaweka watu ambao watakuwa ‘watetezi’ wa madudu hayo, au wao wenyewe kuamua kuingia madarakani kwa kutumia fedha walizonazo.
Kwa miaka mingi CCM ilikuwa ‘pango la wafanyabiashara, wapiga dili na mafisadi’. Tena tunaambiwa hata wafanyabiashara haramu na wahalifu wengine walijiingiza huko kwa kutumia fedha walizozichuma kiharamu ‘kununulia’ uongozi.
Kwa kifupi, uongozi kuanzia ndani ya CCM na upande wa Serikali, ulikuwa ‘zabuni’, kwamba mtu mwenye fedha ndiye anayechaguliwa na maskini ‘wakafie mbele’.
Chama hiki kikongwe kabisa barani Afrika na kinachoheshimika kutokana na kusaidia Ukombozi wa nchi za Kusini mwa Afrika, kilionekana kuyumba kwa kiasi kikubwa.
Watanzania wanaopenda haki na demokrasia wameshuhudia jinsi Rais Samia alivyotumia staili yake ya R4, na hasa Reconciliation, katika kuhakikisha demokrasia inatamalaki.
Kila mmoja anaamini kwamba Rais Samia anaweza kurejesha misingi imara ya TANU na baadaye CCM, ambayo imeachwa kwenye makaratasi.
Rushwa ni adui wa haki, sitatoa wala kupokea rushwa! Hii ni mojawapo ya Ahadi 10 za Mwana-TANU ambazo zilirithiwa na CCM inayosisitiza kwamba mtu yeyote anayepewa uongozi hapaswi kuutumia kwa maslahi yake binafsi bali kwa maslahi ya wote.
Ahadi hii na nyinginezo zilikuwa zikiimbwa kila mahali kuanzia shule za msingi, sekondari na vyuo vikuu ambako somo la Siasa lilianzishwa na serikali ya TANU na kuendelezwa na CCM kabla ya kufutwa mwanzoni mwa miaka ya 1990 kufuatia kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa.
0629299688