- Biteko asema ni kiu ya Rais Dkt. Samia
Na Salha Mohamed, Dar es Salaam
NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko amesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuona Mradi wa Bwawa la Kufua Umeme la Julius Nyerere (JNHPP) unakamilika mapema ili Watanzania wapate umeme wa uhakika.
Mradi huo umefikia asilimia 92.74, unatarajia kufanyiwa majaribio ya utekelezaji Januari, 2024.
Dkt. Biteko aliyasema hayo jana alipokutana, kufanya kikao na ujumbe wa Waziri wa Nyumba, Nishati na Maendeleo ya Makazi kutoka nchini Misri, Dkt. Assem Elgazzar kuhusu maendeleo ya utekelezaji wa mradi wa JNHPP jijini Dar es Salaam.
“Rais Dkt. Samia ana mategemeo makubwa ya kuanza utekelezaji wa mradi huo, anatamani mwanzoni mwa mwaka 2024 utekelezaji wake uanze.
“Mradi wa JNHPP ndio mwarobaini wa kutatua changamoto ya hali ya upatikanaji umeme nchini,” alisema.
Aliimshukuru Serikali ya Misri kwa kuonesha ushirikiano katika utekelezaji wa mradi huo kwa wakati na kusisitiza kuwa, Serikali ya Tanzania itaendelea kutoa ushirikiano ili mradi huo ukamilike kwa wakati.
Kwa upande wake, Waziri wa Nyumba, Nishati na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Elgazzar, aliishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuiamini nchi hiyo katika kutekeleza mradi huo ambao utakua mfano katika ufuaji umeme.
Balozi wa Misri nchini, Sherif Ismail aliahidi kuwa, nchi yao itaendelea kushirikiana na Tanzania katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo wa JNHPP.
Hata hivyo, mradi wa JNHPP unatekelezwa na Kampuni ya Arab Contractor kutoka nchini Misri.
Kikao hicho kilihudhuriwa na ujumbe wa TANESCO, Kampuni inayotekeleza mradi huo (Elsewedy Electric) ya nchini Misri na Wawakilishi kutoka Wizara ya Nishati.