Na Farida Ramadhani na Joseph Mahumi, WF, Arusha
Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa ameiagiza Wizara ya Fedha kuandaa mpango maalum wa kutoa elimu na hamasa kwa Watanzania ili kila mmoja ajenge tabia ya kutumia huduma rasmi za fedha.
Alitoa agizo hilo jijini Arusha wakati akizindua Maadhimisho ya Tatu ya Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa yanayoendelea katika viwanja vya Sheikh Amri Abeid jijini humo, yenye kaulimbiu ya “Elimu ya Fedha, Msingi wa Maendeleo ya Uchumi”.
Alisema huduma hizo zinatambulika kisheria na zitawawezesha wananchi kuepuka madhara mbalimbali ya kutumia huduma ambazo sio rasmi ikiwemo kupoteza fedha kwa kudhulumiwa.
Mhe. Majaliwa pia aliiagiza Wizara hiyo kushirikiana na watoa huduma za fedha kuhakikisha wanaweka mfumo endelevu wa kutoa elimu ya fedha kwa wananchi katika maeneo ya mijini na vijijini.
Alisema elimu hiyo itolewe kwa lugha rahisi inayoeleweka kwa wananchi huku akisisitiza elimu hiyo iangalie yale mambo muhimu ambayo wananchi wanaweza kuyatekeleza.
“Sio tu kutumia maadhimisho haya ambayo yanadumu kwa wiki moja kutoa elimu, inabidi tuwe na mfumo endelevu wa kutoa elimu kwa wananchi, mijini na vijijini. Mtumie matangazo mbalimbali lakini sasa hivi kuna vyombo vingi vya habari na mitandao ya kijamii”, alisema Mhe. Majaliwa.
Pia aliitaka Wizara hiyo kuongeza juhudi za kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kudai risiti wanapofanya manunuzi ya bidhaa na huduma mbalimbali.
Alisema kila wananchi wanapofanya manunuzi fedha wanayolipia kuna kiasi kinaingia Serikalini hivyo kuchangia katika Pato la Taifa.
“Usipodai risiti maana yake fedha hizo hupeleki Serikalini kutunisha mfuko wetu unamuachia mfanyabiashara na wewe unaefanya biashara kuwa mzalendo toa risiti hata kama mtu kasahau mkumbushe kama wafanyabiashara”, alisisitiza.
Mhe. Majaliwa pia aliiagiza Wizara hiyo kuwasimamia watoa huduma za fedha nchini kwa kuhakikisha wanapunguza gharama za upatikanaji wa huduma hizo ikiwemo riba na ada ili kuwawezesha wananchi kupata huduma hizo rasmi.
Aliitaka Wizara hiyo kuimarisha mifumo ya kuwalinda watumiaji wa huduma za fedha ili baadhi ya watoa huduma wasio waadilifu wasitumie changamoto ya uelewa mdogo wa baadhi ya wananchi kuhusu masuala ya fedha na kuwadhulumu.
Aidha, aliiagiza Ofisi ya Rais TAMISEMI kushirikiana na Wizara ya Fedha kukamilisha kwa haraka taratibu za utoaji wa mikopo ya asilimia10 ya halmashauri iliyokuwa imesitishwa.
Alitoa muda hadi kufikia Januari 24, 2024 taarifa zote ziwe zimewekwa kwenye mfumo ili wananchi waweze kukopeshwa katika halmashauri zote nchini.
“Kwa kuwa tulisitisha mwezi wa nne, naamini kila halmashauri inafedha za kutosha kwa ajili ya kuwakopesha wananchi ikiwemo wajasiriamali“, alibainisha Mhe. Majaliwa.
Kwa upande wake Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba alitoa rai kwa wananchi kufuata taratibu wakati wa kutoa na kupokea huduma mbalimbali za fedha ili kuwawezesha kujikwamua kiuchumi.
Aliziagiza Taasisi za Fedha hususani benki kuwaendeleza wateja wao hususan wafanyabiasha na wananchi kwa ujumla pale wanapoona wanashindwa kujiendeleza na kurejesha mikopo kwa wakati.
“Baadhi ya Taasisi zetu zikiwemo Benki pamoja na kazi nzuri wanazofanya lakini inapofika mteja wao analegalega, lile jukumu la kulea linawatoka kabisa. Yaani unakuta mtu ameshalipa robo tatu, amekwama kulipa robo tu, au ameshalipa asilimia 80 amekwama 20, wanachukua dhamana yake yenye thamani kubwa kuliko kile kilichobakia”, alibainisha Mhe. Nchemba.
Alisema taasisi hizo zinatakiwa kuwawezesha wateja wao kulipa mikopo ili waendelee kupata faida.
Akizungumzia maadhimisho hayo, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-Maamry Mwamba alisema Wizara hiyo inaratibu maadhimisho hayo kwa kushirikiana na wadau wengine wa Sekta ya Fedha wakiwemo Wizara, Idara na Wakala wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Zanzibar, Taasisi za Fedha, Asasi zisizo za Serikali na Sekta Binafsi.
Alisema katika maadhimisho wananchi watapata elimu ya masuala ya fedha hususani katika maeneo ya usimamizi wa fedha binafsi, uwekaji wa akiba, mikopo, uwekezaji, bima, kodi na hatifungani.
Dkt. Mwamba alisema elimu hiyo inalenga kuwafikia wadau wote ikiwemo watumishi wa umma, wanafunzi, wanawake, vijana, watu wenye mahitaji maalumu, wajasiriamali, asasi za kiraia, asasi za kidini, wanahabari na wananchi wote kwa ujumla.