Na DW
MAHAKAMA ya Juu ya Pakistan jana imekubali ombi la dhamana la Waziri Mkuu wa zamani Imran Khan, kwa mujibu wa wakili wake.
Uamuzi huo wa mahakama hiyo unakuja siku moja baada ya mahakama nyengine kutangaza kuwa kinyume cha sheria kesi nyingine inayomkabili ya kuvujisha siri za serikali.
Khan ambaye ni nyota wa zamani wa mchezo wa kriketi, anakabiliwa na mashtaka kadhaa mahakamani akiwa na matumaini ya kuachiwa na kukiongoza chama chake katika kampeni ya uchaguzi mkuu utakaofanyika Februari 8, ambapo hasimu wake, Waziri Mkuu mwengine wa zamani anatumai kushinda.
Khan (71) alifungwa kwa miaka mitatu jela mnamo Agosti 5 kwa kuuza zawadi za serikali wakati wa utawala wake kati ya mwaka 2018 na 2022.
Aliondolewa madarakani mwaka 2022 baada ya kupoteza kura ya kutokuwa na imani naye bungeni.