Machozi ya Rais Samia kwa Asimwe hayatawaacha salama wauaji albino

Na Daniel Mbega, Kisarawe

TAIFA limegubikwa na msiba, majonzi na masikitiko! Kila mtu anamlilia mtoto Asimwe Novart (2), ambaye uhai wake umekatishwa ghafla na majahili waliomuua na kunyofoa baadhi ya viungo vyake.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, naye analia, tena kilio cha mtu mzima. Unaweza usiyaone machozi yake hadharani, lakini kwa kauli yake utajua tu kwamba, Mama analia.

Na alionyesha majonzi yake Jumanne, Juni 18, 2024 wakati wa Kongamano la Pili la Maendeleo ya Sekta ya Habari jijini Dar es Salaam, wakati alipoeleza kusikitishwa kwake na kifo cha Asimwe, mtoto mwenye ualbino, mkazi wa Kitongoji cha Mbale, Kijiji cha Bulamula, Kata ya Kamachumu, Wilaya ya Muleba mkoani Kagera.

Hii ilikuwa ni baada ya mwili wa mtoto huyo kupatikana ukiwa umefungwa kwenye sandarusi na kutelekezwa kwenye moja ya karavati iliyopo Barabara ya Ruhanga-Makongora, Kata ya Ruhanga, Tarafa ya Kamachumu, Wilaya ya Muleba huku baadhi ya viungo vyake vikiwa vimekosekana.

“Kuna kifo kimetokea na kimenigusa sana, kifo cha albino, alikuwa akicheza nyumbani akatekwa, wamekwenda wamemnyofoa nyofoa, siku tatu hajaonekana, kimeonekana kimeshaharibika,” akasema.

Mtoto Asimwe alitekwa nyara Alhamisi, Mei 30, 2024 majira ya saa moja usiku, lakini maiti yake iliokotwa Juni 17, 2024 saa sita mchana ikiwa imekatwa baadhi ya viungo. Ni unyama ulioje.

Rais Samia, kama mzazi na mlezi wa Watanzania wote, kamwe hawezi kuacha kulia. Lazima atamwaga machozi. Binadamu asiye na hatia anauawa kikatili na watu wanaotekeleza imani zao potofu.

Inasikitisha zaidi unaposikia kwamba, ati Paroko, kiongozi wa kiroho, ndiye aliyekuwa nyuma ya tukio hilo la kikatili.

Taarifa ya Jeshi la Polisi ilisema jeshi hilo limewakamata watu tisa akiwemo Elipidius Rwegoshora, ambaye ni Paroko Msaidizi wa Parokia ya Bugandika, wanaodaiwa kuhusika katika utekaji na mauaji ya mtoto Asimwe Novart, baada ya kumshawishi baba mzazi wa mtoto huyo, kufanya baishara ya viungo vya binadamu.

Na taarifa hiyo ikawataja watuhumiwa akiwemo baba mzazi wa mtoto huyo aitwaye Novart Venart, Desidei Evarist ambaye ni mganga wa jadi mkazi wa Nyakahama, Elipidius Rwegoshora Paroko Msaidizi wa Parokia ya Bugandika ambaye anadaiwa kumfuata na kumshawishi baba mzazi wa mtoto ili wafanye biashara ya viungo vya binadamu, pia anatuhumiwa kuwa ndiye aliyemtafuta mganga wa jadi na kulipia gharama zote za uganga.

Wengine ni Dastan Kaiza mkazi wa Bushagara, Faswiru Athumani mkazi wa Nyakahama, Gozbert Alkadi mkazi wa Nyakahama Kamachumu, Rwenyagira Burkadi mkazi wa Nyakahama Kamachumu, Ramadhani Selestine mkazi wa Kamachumu na Nurduni Hamada mkazi wa Kamachumu. Wote walieleza namna walivyoshiriki katika tukio hilo.

Hakuna wa kuweza kumfuta machozi Bi. Kebyera Richard, mama wa marehemu, na hasa anapogundua kwamba mumewe kipenzi, kumbe ndiye mhusika mkuu wa mauaji ya binti yao, ambaye huenda angekuja kuwa Rais wa Tanzania baadaye, ama rubani, ama daktari. Naye ajuaye kesho yake?

Kilio cha Mheshimiwa Khadija Taya, maarufu kwa jina la usanii kama Keysha, Mbunge wa Viti Maalum (CCM), nacho kimewaliza wengi.

Keysha, ambaye ana ualbino pia, akakumbusha kwamba, kila unapofika wakati wa uchaguzi watu wenye ualbino hukosa amani kutokana na kukithiri kwa matukio ya kuwadhuru.

Na akasema, mnamo Mei 4, 2024 mtoto anayeitwa Julius Kazungu (10) alijeruhiwa na kitu chenye ncha kali kichwani na mikononi huko Katoro, Wilaya ya Geita, mkoani Geita kabla ya tukio la kutekwa nyara na hatimaye kuuawa kwa Asimwe Mei 30, 2024.

“Mtoto huyu amepatikana Juni 17, 2024 akiwa amekatwa viungo, Mheshimiwa Naibu Spika, hapa ninapozungumza watu wenye ualbino hawana amani, hawana raha, wanaamini kwamba karibia na uchaguzi maisha yao yanakuwa hatarini.

“Na sisi wabunge tunaenda katika uchaguzi, hivyo mheshimiwa Spika kwa maumivu waliyonayo watu wenye ualbino, kwa maumivu ya wazazi hawa ambao watoto wao wamejeruhiwa. Ninaomba Bunge liahirishe shughuli zake na kujadili namna nzuri ya kuwalinda watu wenye ualbino pamoja na watoto,” akasema huku akibubujikwa na machozi.

Akaongeza: “Tuitake Serikali kuleta sheria kali ambazo zitaweza kuonyesha mfano kwa watu wengine kutokufanya vitendo hivi. Naomba sana kiti chako kikubali na kuridhia lakini kuwaomba wabunge wenzangu waniunge mkono hoja hii.”

Kilio hiki si cha albino peke yao wala si cha Mama Samia tu, bali ni cha Watanzania wote.

Ikumbukwe kwamba, hakuna kabila la Albino wala hakuna dini au dhehebu la Albino. Kama yangekuwepo hayo, pengine mwingine asiye na utu angeweza kusema “watajua wenyewe na mila na tamaduni zao”.

Hawa ni Watanzania wenzetu, wanatoka katika dini na makabila mamoja kama sisi, na wanatoka katika familia zetu.

Kama siyo watoto katika familia na koo zetu, basi ni majirani na rafiki zetu. Pengine hata ni wenza wetu.

Kilio hiki cha mauaji ya albino ni cha muda mrefu, takriban miaka 20 iliyopita.

Ingawa jitihada kadhaa zimefanyika, nyingine kwa mafanikio makubwa, lakini albino wanayo haki ya kupaza sauti zao kwa sababu kuna kesi nyingi ambazo ziko katika mahakama za sheria, lakini uchunguzi unaonyesha kwamba, baadhi ya kesi hizo hazina washtakiwa hata mmoja, matukio ambayo yalitokea tangu mwaka 2006.

Wenye ualbino, na hata kupitia Chama cha Albino Tanzania (TAS) wanatambua kwamba orodha ya kesi hizo ni ndefu na kadiri matukio hayo yanavyoibuka tena, wanapata hofu kama zile za nyuma zinaweza kupata washtakiwa.

Kwa kumbukumbu nilizo nazo, orodha ya kesi zinazoendelea katika Mahakama za Sheria na ambazo hadi mwaka 2015 hazikuwa na washtakiwa hata mmoja, ni kama zifuatazo:

  • Shauri lenye kumbukumbu namba KAH/IR/92/2006, la mauaji ya Ariph Amon wa Kahama mkoani Shinyanga ambalo lilitokea mwaka 2006, halina mshtakiwa hata mmoja.
  • Shauri namba BND/IR/2811/2007 la mauaji ya Minza Lugema (10), Mwanafunzi wa darasa la tano Shule ya Msingi Rubana, Msukuma, Mkazi wa Kijiji cha Balili wilayani Bunda. Tukio lilitendeka Oktoba 4, 2007 majira ya saa 4:00 usiku katika Kijiji cha Balili ambapo watuhumiwa walimkata mguu wa kulia na kutoweka nao. Hakuna hata mtuhumiwa mmoja aliyekamatwa.
  • Shauri lenye kumbukumbu namba MIS/IR/2010/2007 la mauaji ya Sitakelewa Shitobelwa, mkazi wa Misungwi lililotokea mwaka 2007. Hakuna mtuhumiwa aliyekamatwa.
  • Shauri lenye jalada namba KDO/IR/1334/2008, kuhusu mauaji ya Safina Meshaki (miezi mitano), Mhutu, Mkazi wa Magalama – Kibondo mkoani Kigoma. Hakuna mshtakiwa aliyepatikana.
  • Shauri lenye kumbukumbu namba GER/IR/2056/2009 la mauaji ya Gasper Elikana (10), Msukuma, Mwanafunzi wa Shule ya Msingi Nyawilimirwa, Geita. Hakuna mtuhumiwa aliyekamatwa.
  • Shauri namba BAR/IR/708/2014 MC 18/2014 la mauaji ya Mungu Lugata wa Bariadi liko mahakamani. Bado liko chini ya upelelezi.
  • Shauri lenye jalada namba BUI/IR/117/2007 na kesi namba MCC No. 42/2007 kuhusu mauaji ya Rwegamoyo Tilanga (58), Mzinza, Mkulima na mkazi wa Chigunga mkoani Geita. Tukio hilo lilitokea Oktoba 3, 2007 huko Chigunga ambapo marehemu alikatwa panga sehemu mbalimbali za mwili na kuchukua mikono yote na nywele. Kwa kumbukumbu zangu, Shauri hilo lilikuwa linaendelea mahakamani likiwakabili washtakiwa Nelson Yinza na Ndimanya Tobo.
  • Shauri lenye majalada BI/IR/1502/2008 na PI 58/2008 la mauaji ya Arodio Augustino (16), Msubi, Mwanafunzi wa Shule ya Msingi Rugondo, Mkazi wa Kitongoji cha Kibirizi, Kijiji cha Rugondo wilayani Biharamulo. Tukio hilo lilitokea Desemba 3, 2008 majira ya saa 1:30 usiku maeneo ya Rugondo. Marehemu alikatwa sehemu za mikono yote miwili, lakini hawakuondoka nayo. Washtakiwa walikuwa Sodoki Samson, Richard Christian, Tibenderana Kalimanzila, na Damas Simon.
  • Shauri lenye kumbukumbu namba ULY/IR/45/2013 na MC 12/2013 la mauaji ya Lugolola Bunzari (7), Msukuma, Mkazi wa Kitongoji cha Kinondoni, Kata ya Kanoge, Tarafa ya Ulyankulu, Wilaya ya Kaliua, Mkoa wa Tabora. Kesi hiyo iko Mahakama Kuu.
  • Shauri lenye kumbukumbu namba KAU/IR/835/2014 na CC. 63/2014. Kosa la kujaribu kuua ambapo majeruhi ni Pendo Sengerema (15), Msukuma, Mkazi wa Ugasa, Kata ya Usinge, Wilaya ya Kaliua mkoani Tabora. Kesi hiyo ilikuwa inasubiriwa Ripoti ya Mkemia Mkuu wa Serikali ili jalada litumwe kwa Mwanasheria Mkuu kwa hatua zaidi.
  • Shauri lenye jalada namba NGU/IR/1202/2014 la kumteka nyara mtoto Pendo Emmanuel Nundi (6), Msukuma, Mkazi wa Kijiji cha Ndamhi wilayani Kwimba ambalo lilitokea Desemba 27, 2014. Hadi Julai 2015 upelelezi ulikuwa unaendelea na baadhi ya watuhumiwa walikuwa mahabusu.
  • Shauri namba IGN/IR/1070/2014 na CC. 18/2014. Kosa ni kujaribu kuua. Majeruhi ni Muungu Masaga Gedi, Mkazi wa Kitongoji cha Mkuyuni, Kijiji cha Buhekela, Kata ya Igoweko, Tarafa ya Simbo, Wilaya ya Igunga. Washtakiwa kadhaa walikamatwa na kesi hiyo ilikuwa inasubiri majibu kutoka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali.
  • Shauri namba MTO/IR/76/2015 na CC. 198/2015. Kosa la kujeruhi ambapo majeruhi ni Limi Luchoma. Tukio hilo lilitokea Mei 14, 2015 huko Mpanda mkoani Katavi. Kesi hiyo iko mahakamani.

Jamii ya wenye ualbino pia ina haki ya kumwaga machozi, kwa sababu kesi 22 za mauaji zilifutwa mahakamani na DPP na washtakiwa kuachiliwa kwa Nolle Prosequi.

Kwamba ni kutokana na makosa ya kiupelelezi au udhaifu wa kuandaa mashtaka ambayo yangeweza kuwaweka hatiani washtakiwa ndivyo vilivyomlazimu DPP kuwaachia huru washtakiwa, hakuna anayejua.

Lakini kumbukumbu zilizopo zinaonyesha kesi hizo kama ifuatavyo:

  • Machi 30, 2009 mahakama iliwaachilia huru John Masanja, Lucas Sebesebu, John Elias na Madoki Kasubi walioshtakiwa kwa mauaji ya Waziya Bun’hele, tukio ambalo lilitokea Februari Mosi, 2008 huko Sengerema mkoani Mwanza na kufunguliwa jalada namba SEN/IR/178/2008.
  • Agosti 10, 2008 mahakama iliwaachilia huru Japhet Lugegeta na Elias Lutambi katika Shauri namba MCC 13/2008 la mauaji ya Vumilia Makoye, mkazi wa Kijiji cha Bugonda wilayani Magu mkoani Mwanza aliyeuawa Mei Mosi, 2007.
  • Oktoba 30, 2008 Kapugi Bukwimba, John Lugaila Na Nkhanga Charles waliachiliwa huru na mahakama katika Shauri namba MCC No. 08/2008 la mauaji ya Nyerere Lugaila wa Kijiji cha Usagala wilayani Misungwi aliyeuawa Juni 28, 2008.
  • Septemba 8, 2010 washtakiwa Lucas Kulwa, Samwel Budeba na Sega Tishimo waliachiliwa huru na mahakama katika Shauri namba MCC No. 05/2009 la mauaji ya Jonas Maduka wa Kijiji cha Songoro wilayani Sengerema aliyeuawa Januari 21, 2009.
  • Desemba 6, 2010 mahakama iliwaachilia huru Bahati Lugwisha na Emmanuel Shigongo katika Shauri la mauaji ya Yunis Bahati wa Kijiji cha Butongwa, Sengerema mkoani Mwanza aliyeuawa mwaka 2008 ambalo lilipewa jalada namba SEN/IR/1224/2008.
  • Julai 8, 2009 Regina Lusorubangija, Dalali Makoye na William Manyara waliokuwa wanakabiliwa na mashtaka ya mauaji ya Rahel NyamabululA wa Magu katika Shauri namba MCC No. 42/2007 waliachiliwa huru na mahakama.
  • Desemba 9, 2011 washtakiwa Kajumulo Emmanuel, Godfrey Matabanya, Juvenile Damas na Shida Juvenile katika Shauri namba MCC No. 13/2008 la mauaji ya Sifa Juvenile (4) wa Kasulu mkoani Kigoma, waliachiliwa huru.
  • Desemba 2, 2011 mahakama iliwaachilia huru washtakiwa nane Juma Buyagaji, Deus Mtana, Yahaya Bulasanzaye, Jadili Jontham, Yohana Lukwakwa, Masulu Sima, Dangwili Mwelu, Kwihize Kababara na Anthony Dickson katika Shauri namba MCC No. 09/2010 la mauaji ya Nahimana Daudi (4) wa Kijiji cha Kitahana, wilayani Kibondo aliyeuawa Aprili 18, 2010.
  • Februari 17, 2009 washtakiwa Philemon Mgoyezi, Ngendamenya Nelson Muntu, Safari Mnobero na Boniface Juma waliachiliwa huru na mahakama katika Shauri la mauaji ya Jovin Majaliwa (46) wa Rusahunga, Nyantakara wilayani Biharamulo lililokuwa na kumbukumbu za majalada yenye namba BI/IR/904/2008 na PI No. 36/2008. Mauaji hayo yalifanyika Julai 25, 2008.
  • Julai 14, 2014 Mahakama ilimwachilia huru Edward Kuberth katika Shauri la mauaji ya Sauda Ibrahim (20) mkazi wa Songambele, Kagondo wilayani Biharamulo aliyeuawa Septemba 3, 2008. Shauri hili lilikuwa na majalada yenye kumbukumbu namba BI/IR/1102/2008 na PI No.58/2008.
  • Januari 6, 2012 mahakama iliwaachilia huru washtakiwa sita ambao ni Joas Martine Kaizelege, Hassan Said, Jones Binamugizi, Gwemelo Pius, Elipidius Kekanika Wasara na Daudi Karuma katika Shauri la mauaji ya Solomon Laurian (28) wa kitongoji cha Misana wilayani Muleba aliyeuawa Januari 17, 2009. Shauri hilo lilikuwa na majalada yenye kumbukumbu namba MUL/IR/117/2009 na PI 04/2009.
  • Januari 9, 2012 washtakiwa Shija Raphael, Jonathan Anatory, Venant Ancibert, Germany Norbert, Makoye Magazi na Daudi Karuma waliachiliwa huru katika Shauri la mauaji ya Michael Petro (6), wa Kijiji cha Nyamiranda wilayani Muleba aliyeuawa Januari 14, 2009 lililokuwa na majalada yenye kumbukumbu namba MUL/IR/100/2009 na PI 03/2009.
  • Mahakama ilimwachilia huru Masumbi Kipeja katika Shauri la mauaji ya Kija Mbogo maarufu kama Mariam (7) wa Meatu lililokuwa na jalada lenye kumbukumbu namba MEA/IR/454/2008.
  • Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali iliwaachilia huru Mbona Kabila Kakuza, Faustine Thadeo, Timotheo Ngoromere na Sayoni Mtahondi katika Shauri la mauaji ya Zacharia John (47) wa Kijiji cha Kasumo wilayani Kasulu lililokuwa na jalada namba KAS/IR/1423/2008.
  • Aprili 25, 2012 mahakama iliwaachilia huru kwa Nolle Prosequi washtakiwa Songi Luhende, Maige Maduka na Nkende Mwandu katika shauri la mauaji ya Kurwa Jiliba (7) mkazi wa Kijiji cha Mgogwa, Kata ya Roywa, Wilaya ya Uyui mkoani Tabora. Shauri hilo lilikuwa na kumbukumbu namba UW/IR/383/2009 na MC. 15/2009. Hata hivyo, jalada lilipelekwa kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa barua yenye Kumb. TBR/SCR/CID/434/2009/9 ya tarehe 03/12/2014 kwa lengo la kutaka lisomwe na kutolewa uamuzi.
  • Agosti 10, 2009 washtakiwa Muyengi Nyalukendi na Sospeter Nyalukendi waliachiliwa huru na mahakama kwa Nolle Prosequi chini ya Kifungu cha 91 (1) cha CPA 1985 katika Shauri namba MUS/IR/5564/2007 na MC. 30/2007 la mauaji ya Judith Daudi (16), Msukuma, aliyekuwa mwanafunzi wa darasa la sita Shule ya Msingi Kabulabula, Wilaya ya Msoma Vijijini mkoani Mara ambaye aliuawa mwaka 2007.
  • Agosti 20, 2008 washtakiwa Sabato Masini Funyenye, Fabian Maelo Funyenye na Nyamtondo Makwega Nyaberenge waliachiliwa huru na mahakama kwa Nolle Prosequi chini ya Kifungu cha 91 (1) cha Sheria za Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA) 1985 katika Shauri namba MUS/IR/2176/2008 na MC. 17/2008 la mauaji ya Nyamiti Onyamakanya Masatu (37), Kabila Mkwaya, mkazi wa Kijiji cha Bwai-Kitururu, Wilaya ya Musoma Vijijini.
  • Washtakiwa Robert Tangawizi, Agnes Majala na Machibya Alphonce waliokuwa wakikabiliwa na mashtaka ya kumjeruhi Adam Robert (13) aliyekuwa mwanafunzi wa darasa la tatu katika Shule ya Msingi Kaseme ‘B’, mkazi wa Kijiji cha Nyalubuguna, Wilaya ya Nyanghwale mkoani Geita waliachiliwa huru kwa Nolle Prosequi. Tukio hilo lilitokea Oktoba 14, 2011 kijijini Nyalubuguna.
  • Novemba 24, 2009, washtakiwa Kamana Ludogoza, Sebastian Emmanuel, Josephat Kagoma, Angelemunwe Kazili na John Japhet waliachiliwa huru katika Shauri la kumjeruhi Elias Ludogoza (37) wa Kijiji cha Lunanzi, Tarafa ya Nyarubungo wilayani Biharamulo lililokuwa na majalada yenye kumbukumbu namba BI/IR/1370/2008 na PI No.48/2008.
  • Novemba Mosi, 2011 mshtakiwa George Jostone aliachiliwa huru katika Shauri la kujaribu kumuua Mariam Stanford (28) mkazi wa Mkatoketoke – Ntobeye wilayani Ngara lililotokea Oktoba 17, 2008 ambalo lilikuwa na majalada yenye kumbukumbu namba NGR/IR/916/2008 na PI No. 28/2008.
  • Washtakiwa Petro Nkolo na Rosha John waliachiliwa huru katika Shauri la kumjeruhi Kulwa Lusana (18) wa Kijiji cha Mbizi wilayani Kahama lililokuwa na jalada lenye kumbukumbu namba KAH/IR/4744/2011.
  • Washtakiwa Magobo Njige, Senga Mabirika na Bupina Mihayo waliachiliwa huru katika Shauri la kumjeruhi Kabula Nkarango (13) wa Kijiji cha Luhaga wilayani Kahama lililokuwa na jalada lenye kumbukumbu namba KAH/IR/1770/2010.

Kwa kadiri inavyoonekana, Rasi Samia hawezi kukaa kimya kati hili n ani Dhahiri wote wanaojihusisha na vitendo vya kuwadhuru albino nchini watashughulikiwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *