
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
UMOJA wa Wanawake Machinga Dodoma(UWAMADO) wamempongeza, Rais Dkt. Samia Hassan kwa ujenzi wa Soko la Kisasa la Machinga Complex na miundombinu ya kisasa ya soko hilo ambalo ni la kipekee nchini.
Hayo yamesemwa jana wakati wa uzinduzi wa chama cha UWAMADO uliofanyika kwenye eneo la soko la Machinga Complex kwa kuzinduliwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule.

Akisoma Risala Katibu wa UWAMADO, Mariam Kajembe, amesema umoja huo umelenga kuwaleta wanawake Machinga pamoja ili kujijenga na kujiimarisha uchumi.
Aidha, UWAMADO umempongeza Rais Dkt. Samia kwa Ujenzi wa Soko la Machinga Complex, ambalo limesaidia kuwaleta pamoja wafanyabiashara wengi wadogo pamoja ambao awali hawakuwa katika maeneo rasmi na hivyo kuwafanya kutokuwa rasmi.

Akitoa hotuba yake, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, amewapongeza UWAMADO kwa kuamua kuanzisha umoja wao ambao utawasaidia kujiendeleza zaidi na kujiimarisha kiuchumi.
“Jambo hili la kuanzisha umoja ni jambo jema, hakikisheni umoja unafikia malengo mliyokusudia.Rais kawajengea soko kubwa na zuri, soko hili liwe kichocheo cha ukuaji wenu kimtaji na kibiashara.
Niwatake Uongozi wa Jiji la Dodoma kuendelea kubuni na kuanzisha maeneo mapya ya kuwapanga vizuri wafanyabiashara wadogo wa Dodoma,”amesema Senyamule.

Akitoa salamu zake Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini, Anthony Mavunde, amewapongeza UWAMADO kwa kuona umuhimu wa kukaa pamoja kujiinua kiuchumi na kuwataka kuchangamkia fursa ya mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya ndani ya jiji ambayo kiasi cha Sh. bilioni 7 kimetengwa kwaajili ya kuwawezesha wakina mama,vijana na watu wenye ulemavu.

