Na Daniel Mbega
MWAKA 2022 Rais Samia Suluhu Hassan aliielekeza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kujenga utamaduni wa kukusanya mapato bila kutumia mabavu, lengo likiwa kuhamasisha uzalendo na kuwafanya walipa kodi wajisikie huru.
Maagizo hayo ya Rais Samia ni sehemu tu ya maboresho ya ukusanyaji mapato ambayo Serikali imekuwa ikiyafanya na kwa kiasi kikubwa ndiyo yamechangia TRA kukusanya kiasi cha Shs. trilioni 2.3 kwa mwezi Septemba 2023 ikiwa ni zaidi ya lengo la makusanyo ya Shs. trilioni 2.2, ukiwa ni ufanisi wa asilimia 100.5 ya lengo.
Siyo siri kwamba, ulipaji wa kodi bila shuruti ni nyenzo muhimu ya kuwezesha makusanyo ambayo yana tija kubwa katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kwa nchi yoyote.
Kitendo cha kulipa kodi bila shuruti ni uzalendo wa hali ya juu na kinaiwezesha Serikali kuonyesha ufanisi mkubwa katika makusanyo ya mapato yake.
Utekelezaji wa miradi ya maendeleo unahitaji fedha, na Bajeti ya Serikali inategemea mapato ya ndani kwa asilimia kubwa ambayo yanatokana na makusanyo ya kodi.
Ikumbukwe pia kwamba, hata fedha za wahisani ambao ama wanatoa misaada au mikopo kwa nchi zinazoendelea kama Tanzania, ni sehemu ya makusanyo ya kodi kutoka kwa wananchi wao.
Kimsingi, kulipa kodi ni jambo la fahari na uzalendo, hivyo ni wajibu wa kila mfanyabishara kuhakikisha analipa kodi kwa wakati ili kusaidia maendeleo ya nchi na sekta mbalimbali ambazo zinategemea kodi katika kujiendesha.
Kila mwananchi kwa nafasi yake ana mchango katika maendeleo yanayopatikana ndani ya Taifa hili, hivyo ni muhimu watu wawe na utamaduni wa kulipa kodi ili Serikali iweze kutekeleza majukumu yake na wao wawe na haki ya kudai na kuona fahari juu ya maendeleo yanayofanyika nchini.
Mipango ambayo Serikali imejiwekea haiwezi kufanikiwa endapo nchi itazembea katika ukusanyaji kodi na mapato ya serikali, na ili kutimiza malengo hayo ya makusanyo, Serikali inaendelea kulinda vyanzo vya mapato, kuimarisha ukusanyaji wa mapato wenyewe kudhibiti biashara za magendo, kuhimiza matumizi ya mashine za kielekroniki (EFD) katika kukusanya mapato na kudhibiti katika ukadiriaji wa ushuru wa forodha.
Mafanikio ya sasa ya TRA katika ukusanyaji wa mapato yanaelezwa pia na Kamishna Mkuu wa mamlaka hiyo, Alphayo Kidata, kuwa yanatokana na uadilifu na uzalendo unaooneshwa na wananchi kwa nchi yao.
Kidata anasema, mapato ndani ya nchi yana kazi nyingi kwenye shughuli za maendeleo hivyo wananchi wanapaswa kulipa kodi kwa uaminifu ili miradi ya kijamii iweze kutekelezwa.
Anaongeza kusema kwamba, makusanyo yanapokuwa makubwa miradi ya maendeleo nayo inakuwa mingi ikiwa ni pamoja na elimu, afya, miundombinu, maji na huduma muhimu za kibinadamu.
“Tunawaomba wananchi na wafanyabiashara walipe kodi na watu wakinunua bidhaa wahakikishe wanapewa risiti na matumizi ya mashine za EFD ili kuboresha ukusanyaji mapato,” anasema Kidata.
Maboresho ya Sera
Ilikuyafikia malengo tarajiwa ya Serikali katika ukusanyaji wa mapato, ni vyema Sera za Kodi zifanyiwe maboresho mbalimbali ambayo yataleta tija.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dkt. Hashil Abdallah, hivi karibuni akiwa katika Kongamano la Jukwaa la Wafanyabiashara lililoandaliwa na mkoa huo, aliwataka wafanyabiashara kutoa maoni ya uboreshaji wa Sera za Kodi kupitia Timu ya Wataalamu wa Uchambuzi wa Sera za Kodi kutoka Wizara ya Fedha ili waweze kulipa kodi kwa mujibu wa Sheria kwa ajili ya Maendeleo ya Taifa.
Dkt. Abdallah, anasema eneo muhimu katika ufanyaji biashara ni Kodi, na kwamba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, anawataka watu walipe kodi lakini Mamlaka za kukusanya kodi zikusanye kodi kwa weledi bila kuleta mgongano.
“Kodi haikusanywi kwa mtutu wa bunduki kwa kuwa anayekwenda kukusanya kodi haendi kukamata mhalifu na anayelipa kodi anapaswa kujua analipa kwa mujibu wa sheria na analipa kodi kwa sababu ndiyo maendeleo ya nchi,” anasema Dkt. Abdallah.
Anatoa rai kwa Wizara ya Fedha kuendelea kutoa elimu kwa walipa kodi wajue wanapaswa kulipa kodi namna gani ili kutengeneza uhusiano baina ya wafanyabiashara na Serikali.
Na Kamishna wa Idara ya Uchambuzi wa Sera, Wizara ya Fedha, William Mhoja, anasema kunatakiwa kuwekwa mikakati ya pamoja ya kuendelea kurasimisha biashara, kuhamasisha kutumia mashine za kielektroniki katika utoaji wa stakabadhi na kuibua vyanzo vipya vya mapato ili kupunguza utegemezi wa mikopo kutoka nje ya nchi.
Anasema, zipo kodi ambazo zililalamikiwa na wananchi hususani kodi ya miamala, Serikali ilisikia na kuondoa kodi hiyo unapotuma pesa, jambo linalodhihirisha kuwa Serikali ni sikivu hasa inapopata maoni ya walipakodi kuhusu utozaji kodi.
“Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Dkt. Samia inatambua mchango wa Sekta Binafsi katika uwekezaji, hivyo imeendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara ili iweze kukuza uchumi wa nchi,” anasema Mhoja.
Anasema, Serikali inaendelea kuimarisha miundombinu wezeshi ya usafirishaji na nishati, kuhakikisha uhimilivu wa viashiria vya uchumi jumla na kuwa na sera za kodi zinazotabirika na kuwianisha tozo na ada mbalimbali zinazotozwa na Wizara na Mamlaka za Udhibiti.
Kwa upande mwingine, Mhoja anasema kwamba, Makongamano ya Kodi yanayofanywa na Wizara ya Fedha kwa kuwashirikisha wadau mbalimbali wakiwemo wananchi wa kawaida yamewezesha kufanyiwa maboresho kwa zaidi ya maeneo 57 ya kikodi katika mwaka wa Fedha 2023/2024 huku hatua hiyo ikilenga kusisimua ufanyaji biashara, kulinda viwanda vya ndani na kuchochea uwekezaji nchini.
Katika kongamano lililofanyika jijini Mwanza Novemba 23, 2023, Mhoja aliwaeleza washiriki kwamba, kuanzishwa kwa Kongamano hilo kumeleta tija katika maboresho ya mfumo wa kodi ambapo katika maandalizi ya Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2023/24 ushirikishwaji wa wadau uliongezeka.
“Maoni yaliyotolewa yalisaidia kufanya maboresho kwenye maeneo 57 ambapo malengo yake ni pamoja na kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara na uwekezaji, kulinda viwanda vya ndani, kuvutia uwekezaji nchini na kuongeza ushindani wa viwanda vya ndani,” akasema Mhoja.
Baadhi ya maeneo yaliyofanyiwa kazi ni pamoja na kuongeza kima cha usajili wa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kutoka shilingi milioni 100 hadi milioni 200.
Maeneo mengini ni kuanzisha utaratibu wa kufanya marekebisho kwenye viwango vya ushuru wa bidhaa kila baada ya miaka mitatu kwa ajili ya utulivu wa kisera, kusamehe VAT ya uuzaji, uingizaji na ukodishwaji wa ndege ikiwa ni pamoja na matengenezo ya ndege.
Pia Serikali imeondoa VAT kwenye malighafi zinazotumika kutengeneza vifungashio vya madawa na kuondoa ada ya ukaguzi kwenye madini yanayouzwa kwenye vituo vya kusafishia madini nchini.
Na Mhoja anasema, lengo la makongamano hayo yatakayofanyika maeneo mbalimbali nchini ni kuboresha uratibu wa ukusanyaji maoni na kuongeza ushirikishwaji wa makundi mbalimbali ili kuboresha Sera za utozaji Kodi, hatua itakayochochea ukusanyaji wa mapato ya Serikali kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya kijamii na ya kimkakati, halikadhalika kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara nchini.
Makongamano haya ya kodi Kitaifa yanayofanyika kikanda yanaendelea na lengo ni kukusanya maoni ya kodi kwa ajili ya kuboresha Sera za Utozaji kodi kwa mwaka 2024/25.
Wafanyabiashara wanavyoitikia
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Taifa (JWT), Hamis Livembe, anasema Rais Samia anataka wafanyabishara walipe kodi halali na siyo haramu kwa ajili ya ustawi mpana wa Taifa.
Livimbe anasema, Rais Samia yupo mstari wa mbele kuhakikisha wafanyabishara wanasikilizwa kero zao ili kupatiwa ufumbuzi wa kudumu na kufanya biashara kwa amani na utulivu.
“Rais Samia anataka kila Mtanzania anafanya biashara kwa amani na utulivu, hataki kodi haramu, kila anayelipa kodi, alipe ile anayostahili kulipa kwa amani.
“Sote ni mashahidi kuwa katika miaka iliyopita wafanyabiashara hawakuwa na fursa ya kukaa pamoja kama hivi na kujadili mambo ya msingi na kero zao kama ilivyosasa. Hivyo tuendelee kuimarisha jumuiya zetu ili tuwe na chombo imara kinachoweza kusikilizwa kwa pamoja,” anasema.
Livembe anasema, baada ya mgomo wa wafanyabiashara Kariakoo, kero za wafanyabiashara kote nchini zilikusanywa na kuanza kufanyiwa kazi na kwa asilimia kubwa nyingi utekelezaji wake umeonekana.
Anasema suala la Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuwakamata wafanyabishara kwa ajili ya kudai Force Tax na kuwasababishia kufunga maduka yao lilifanyiwa kazi na sasa hawakamatwi tena.
“Tangu mwezi wa sita, sijasikia tena mfanyabishara anafungiwa duka au kukamatwa, hivyo kama bado wapo wanaowakamata naombeni mripoti ili hatua zichukuliwe,” anasema akitoa rai kwa wafanyabiashara nchini.
Livembe anasema, suala la wafanyabishara wanaotoa mizigo Dar es Salaam kukamatwa limeshafanyiwa kazi na hakuna anayekamatwa tena na wanaofanyiwa hivyo wawasilishe taarifa zao kwa viongozi wao ili hatua zichukuliwe.
Anasema pia kodi ya VAT, ilipigiwa kelele na wafanyabishara walilijadili na kukawa na hoja mbili, ikiwamo kuondolewa kwa kiwango cha mtaji wa kuanzia milioni 100 na kupunguza kiwango kutoka asilimia 18 hadi asilimia 10.
Anaongeza kwamba, suala la kiwango cha juu cha anayetakiwa kulipa kodi ya ongezeko la thamani VAT ni kuanzia mwenye mtaji wa milioni 500 hivyo wameanza kuongeza kiwango na kwa mwaka huu wameongeza iwe Shs. milioni 200 na kitapanda kila mwaka hadi kufikia Shs. milioni 500.
Anawataka wafanyabishara ambao bado mitaji yao haijafika milioni 200 kuandika barua kupeleka TRA ili kuondolewa kwenye kodi ya VAT.
Livembe alisema pia wamekubaliana kuwa ushuru wa huduma (Service Levvy) ambao ulianzishwa kwa mujibu wa Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa, Sheria ya mwaka 1982 na kufanyiwa marekebisho mwaka 2012, ipunguzwe kutoka asilimia 0.3 hadi 0.1 na itoke kwenye faida badala ya mtaji.
“Tumekubaliana na serikali kuwa, ipungue lakini kuanzia mwakani kwa sababu bajeti kuu ya serikali imeshatoka, kwahiyo wafanyabishara tuendelee kuwa wavumilivu linafanyiwa kazi,” anasema.
Jambo linguine, anasema, ni ushuru wa kutoa vitenge bandarini ambapo wamekubaliana kupunguza ushuru kutoka Shs. milioni 248 hadi milioni 90 kwa kasha moja ili kupunguza wafanyabishara kuingiza bidhaa hiyo nchini kimagendo.
“Suala hili lilikuwa jepesi, kuwa mwaka 2019 ilipitishwa Sera ya Kulinda Viwanda vya Ndani. Lakini nchini kuna kiwanda kimoja na hakitumii pamba ya ndani na kwa mwezi kinazalisha kontena sita wakati wafanyabishara wanaingiza kontena za vitenge kutoka nje 120 hadi 200 kwa mwezi.
“Baada ya zuio TRA walikuwa wanakusanya Shs. bilioni 66.5 ya vitenge kwa mwezi lakini kodi iliporomoka hadi kufikia Shs. bilioni 2.5 kwa mwezi, hivyo tumekuabaliana kushusha kwa bei hiyo,” anasema.
Mfanyabishara Ezekiel Mwalipanu, kutoka wilayani Rungwe, anamshukuru alimshukuru Rais Samia kwa kuboresha huduma, milango ya TRA ipo wazi, wanasikilizwa na kutatuliwa kero zao kwa wakati.
“Tukibisha hodi TRA wanafungua mlango na kutusikiliza tofauti na siku za nyuma walituona kama maadui ambao walituwinda kila mara ili kutufilisi, Rais Samia aendelee kudumu madarakani kwa sababu ametetea wanyonge tuliokosa sauti kwenye Taifa letu,” anasema.
Uzalendo uanzie shuleni
Kwa kuwa suala la ulipaji kodi ni la uzalendo, ni dhahiri umefika wakati ambapo Serikali inapaswa kuboresha mitaala yake ya elimu na kuhakikisha somo la uzalendo linafundishwa kuanzia ngazi ya shule ya msingi hadi vyuo vikuu hata kama si kwa ajili ya kujibia mitihani, bali kwa kuwajengea watoto uelewa.
Enzi zile za Chama Kimoja tukifuata Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea, ambayo bado ingalipo japokuwa si kwa vitendo, uzalendo uliimbwa mpaka mitaani – kila mwananchi alijiona ni sehemu ya Serikali na anawajibika kuitumikia, kuilinda na kuitetea nchi yake kwa vitendo.
Ilikuwa ni nadra kuona mtu anaharibu miundombinu ya umma halafu akaachwa bila kuchukuliwa hatua, kila mwananchi alikuwa mlinzi na angeweza kumkemea mwenzake kwa vitendo visivyofaa na akasikilizwa.
Leo hii imekuwa tofauti kabisa. Watu wanaiba mafuta ya mashineumba (transformer) iliyoko mbele ya nyumba na watu wanamwangalia tu huku baadhi wakisema “Watajua wenyewe Serikali!” Wanasahau kwamba, Serikali ni “Mimi na Wewe”.
Hoja hii ya kufundisha uzalendo shuleni inashadidiwa pia na TRA, ambayo imependekeza kwa Kamati ya Taifa ya Uboreshaji wa Mitaala inayoongozwa na Profesa Makenya Maboko kufundishwa kwa somo la kodi kuanzia shule ya msingi ili kujenga utamaduni wa kupenda kulipa kodi.
Mkurugenzi wa Huduma na Elimu ya Mlipakodi, Richard Kayombo, anasema kwamba, kwa kuwa elimu imekuwa bure wanaamini kwa kutoa elimu hiyo kuanzia ngazi ya chekechea kutawezesha wananchi wote kuguswa na elimu ya mlipakodi na hivyo kujenga utamaduni na uzalendo wa kulipa kodi.
“Wataelewa vyanzo vya mapato vinatokana na kodi wanayolipa ambayo inatumika kujenga miundombinu ya barabara na mingine. Wataelewa pia kulipa kodi si adhabu,”anasema Kayombo.
Anasema, wanafunzi wanaweza kufundishwa kidogo kidogo kuanzia chekechea kwa kadiri kamati hiyo itakavyoona inafaa na kujenga uelewa kwa wananchi walio wengi.
Anasema kwamb, mapendelezo hayo yametokana na maoni ya wadau kwa nyakati tofauti ambao wamesema kama elimu hiyo ingefundishwa hata uchungu wa kulipa kodi ungepungua.
Akaongeza kwamba, hata utafiti uliofanywa na TRA mwaka 2012 umeonyesha kuna haja kuanza kutoa elimu katika ngazi ya chini ili kuongeza ufahamu kuhusu masuala ya kodi.
Pia wabunge wamekuwa wakitoa mapendekezo yao kila mwaka wakati wa bajeti kuwa somo la kodi lifundishwe kuanzia ngazi za chini ili kupunguza ugumu na kujenga uzalendo wa kuilinda miundombinu ya Serikali.
Ni dhahiri kwamba, maboresho ya Sera mbalimbali za Kodi yakifanyiwa kazi, pamoja na mapendekezo yanayotolewa na wadau, uzalendo utatamalaki na wananchi watalipa kodi kwa hiari na kwa wakati.