Maboresho Bandari ya Dar yatachochea uchumi wa taifa

Na Daniel Mbega,

Dar es Salaam

RAISA wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amebainisha kwamba, maboresho ya Bandari ya Dar es Salaam yatachochea ukuaji wa uchumi wa Taifa.

Akizungumza wakati wa utiaji saini wa mikataba mitatu baina ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kwa niaba ya Serikali, na kampuni ya Dubai Port World (DP World) ya Dubai, jana, Oktoba 22, 2023, kwenye Ikulu ya Chjamwino jijini Dodoma, Rais Samia alisema, uboreshaji wa bandari hiyo una umuhimu mkubwa.

“Bandari inahudumia sehemu nyingi au shehena kubwa ya mizigo ya nchi jirani na hata mataifa ya mbali. Kwa hiyo maboresho yoyote ya kiutendaji yanakwenda kufanya uwekezaji huu yatakuza biashara zetu na kuongeza mapato ya serikali na kuchangia kwenye uchumi wa Taifa,” alisema.

Rais Samia alisema, zilitumika kumpata mwekezaji: “Busara zilituelekeza kuwa tupate mwekezaji ambaye tutashirikiana naye, siyo tu kujibu changamoto za upatikanaji wa mizigo au mzigo wa kutosha kuingia na kutoka nchini, lakini vilevile kuongeza ufanisi utakaofanya gharama zetu kuwa shindani na bandari zingine katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini mwa Bara la Afrika.”

“Leo tumeshuhudia mikataba mitatu muhimu ya uwekezaji wa Bandari yetu ya Dar es Salaam kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Kampuni ya DP World ya Dubai. Mikataba hii iliyosainiwa imezaliwa kutoka kwenye makubaliano ya awali. Lile dude lile lililoleta maneno mengi limetoa sasa mikataba hii mitatu kama ilivyoridhiwa na Bunge na mikataba hii ilishasemwa, nitumie fursa hii kulishukuru sana Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ushauri wao makini na kuridhia azimio la makubaliano ya awali ya ushirikiano na uendeshaji wa Bandari Juni 10, 2023. Aidha, nalishukuru Baraza la Mawaziri kwa kubariki mikataba hii mitatu iliyosainiwa kwa mazingatio ya kifungu,” alisema.

Rais Samia alisema, Serikali imesikiliza hoja zote zilizotolewa na kwamba hakuna hata moja iliyopuuzwa katika kuweka sawa mazingira hadi walipofikia kuweka saini.

“Kwa uhakika hakuna kundi au sauti ambayo haikusikilizwa ama ilipuuzwa. Serikali tuliunda jopo la wataalam lakini pia wanasiasa na wanasheria waangalie zile hoja zote zilizotolewa na watuambie ipi iingie kwenye mikataba na ipi haina mashiko isiingie kwenye mikataba,” alisema.

Rais Samia alisema, Bandari ya Tanzania ni maliasili, ni jaha, ni hidaya na lango kuu la biashara ambalo pia ni chanzo kikuu cha mapato ya Serikali.

“Tunafarijika kuwa DP World wameridhia mahitaji na matakwa yetu kama tulivyobainisha na matamanio ya wananchi wetu na maslahi mapana ya nchi yetu. Bandari ya Dar es Salaam ni maliasili, ni jaha, ni hidaya adhimu tuliyojaliwa na Mwenyezi Mungu. Bandari hii pia ni lango la biashara la nchi zinazotuzuunguka. Bandari hii kuumbwa na kuwekwa kwetu Tanzania, inatupa wajibu wa kuhudumia nchi jirani wanayoitegemea,” alisema.

Alisema, Serikali ilikubaliana kushirikiana na sekta sekta binafsi ili kuwanyanyua wananchi kiuchumi.

“Kila pale ambapo sekta binafsi inaweza kuweka fedha, serikali tusiweke fedha – [badala yake] tuitumie kwa maendeleo ya jamii. Waje wawekeze, tufanye nao biashara, wapate, tupate. Na yale mapato ya serikali tuyapeleke kwenye matumizi mengine zaidi. Mmesikia hapa tuna asilimia kubwa ya watu wetu ambao ni masikini, tutumie kuwanyanyua katika ngazi tofauti tofauti,” alisema.

Alibainisha kwamba, Watanzania wote walikubaliana kuwa bandarini kuna changamoto ya uendeshaji na ndiyo maana hakukuwa na ufanisi mkubwa na mapato yalikuwa haba.

“Katika mzunguko wote wa majadiliano, nilichobaini ni kwamba sote Watanzania tunakubaliana tunayo changamoto pale bandarini. Tunatofautiana tu juu ya namna ya kuzitatua. Wapo wanaoamini sisi wenyewe bila mbia tungeweza kuzitatua. Ni mawazo mazuri ya kimapinduzi, lakini yapo mbali na uhalisia. Na njia hiyo itatuchukua muda mrefu sana kufika wakati Dunia inakwenda mbio. Sisi tungekuwa bado tunasota. Na isitoshe tulishajaribu lakini hatukufanikiwa. Kwa hiyo mikataba hii imezingatia maoni yote yaliyotolewa kwa mtu mmoja mmoja na kupitia makundi ya kijamii pamoja na sheria na taratibu zote za nchi yetu,” alisema.

Aidha, alisema kwamba, uwekezaji wa DP World katika Bandari ya Dar es Salaam umezingatia maslahi mapana ya nchi.

“Nataka niwahakikishie kuwa au niwape uhakika Watanzania wote kwamba maslahi mapana ya nchi yetu yamezingatiwa. Kwa mfano, amesema hapa Mkurugenzi hakuna atakayepoteza kazi. Awe mwajiriwa wa Bandari au hata wanaofanya kazi zao bandarini. Hakuna atakayepoteza kazi. Kutakuwa tu na kufuata mfumo fulani katika kufanya kazi zetu ili viwango vile vikae sawa tuendane na Dunia. Kinachofanyika, kama nilivyosema, ni kuhakikisha Bandari inaendeshwa katika viwango vinavyokubalika duniani, kukuza ufanisi na biashara na hatimaye kukuza mapato ya nchi yetu,” alisema.

Rais Samia alisema, Tanzania ndiyo lango kuu pekee la Bahari Mashariki na Kusini mwa Afrika.

“Kuna milango Bahari mitatu ambayo ni Mombasa, Beira na Durban lakini upande wa Magharibi kuna milango ya Bahari ya Walvis Bay na Lobito. Maana yake ni kwamba, wanaotaka mizigo yao ifike, wana uwezo wa kuchagua Bandari yoyote wakaitumia. Kinachotupa sisi turufu dhidi ya washindani wetu ni bahati ya Mlango Bahari wetu kuwa na masafa mafupi kuingia nchi za jirani na tunafikika na nchi nyingi kwa kutumia mpaka mmoja tu ikilinganishwa na milango bahari mingine. Ukaribu pekee siyo hoja ya kutosha, hivyo ni muhimu kuangalia ufanisi kwani wafanyabiashara hutazama pia ufanisi na gharama,” alisema.

Kwa upande mwingine, Makamu wa Rais, Dkt. Phillip Isdor Mpango, alionya kwamba Bandari isiwagawe Watanzania na kubainisha kwamba, hata waliopinga uwekezaji huo, wamekwenda kushirikiana na Serikali.

“Tuendelee kutunza amani yetu, tuendelee sana kulinda uzalendo kwa Mama Tanzania. Tuboreshe pale panapopaswa ili twende mbele kwa pamoja, kamwe isiwe sababu ya kutugawanya, na mimi nimefurahi kama wengine walivyosema kwamba hata wale wengine waliotoa maoni ya kuonyesha pale palipokuwa na mapungufu wamekuja kushirikiana nasi kwa manufaa ya Mama Tanzania,” alisema Dkt. Mpango.

Akaongeza: “Asilimia 26 ya Watanzania wanaishi chini ya kiwango cha umasikini. Kwa hesabu rahisi ni Watanzania wasiopungua milioni 13. Ni wengi mno. Lakini wakati huo huo, Mwenyezi Mungu aliipendelea nchi yetu. Kwanza kwa idadi kubwa ya watu, lakini vile vile kwa rasilimali nyingi. Tanzania kuna rasilimali za kila aina ikiwemo bandari, kwa hiyo umasikini wa watu wetu asilimia 26 hauendani kabisa na upendeleo mwenyezi Mungu aliotupatia, kutupatia rasilimali nyingi.

“Tumeazimia kuwa Taifa letu tupeleke kuwa Taifa lenye kiwango cha juu cha kati cha kipato haraka iwezekanavyo ili tuweze kuwatoa hawa wenzetu milioni 13 kutoka kwenye lindi la umasikini. Hatuwezi kuwatoa kwa kuendelea kukalia rasilimali za nchi bila kuzifanyia kazi. Sasa kwa rasilimali ya Bandari, naomba tu niwaambie viongozi na Watanzania wenzangu, Dunia ya leo imejaa ushindani mkali. Kwa hiyo hapa tulipo napo tuna Bandari ya Dar es Salaam, lakini pia mmesikia jirani yetu Kenya ana bandari kubwa ya Mombasa lakini anaendelea kujenga na nyingine.

“Bandari yetu isipokuwa na tija, biashara inakwenda huko kwingine. Kwa hiyo ni lazima tujidhatiti, tupambane kiushinddani. Na tukio hili la leo, mheshimiwa Rais wewe ni jasiri kweli kweli. Tukio la leo ni kuipeleka nchi yetu ili tukashindane kibiashara kwenye bandari. Mheshimiwa Rais katika miezi michache iliyopita, pamekuwa na maneno mengi nchini. Kuhusu makubaliano tuliyoanza nayo na ninajua kabisa pengine yataendelea hata baada ya siku ya leo,” alisema Dkt. Mpango.

Ufanisi hauridhishi

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Plasduce Mbossa, alisema kwamba, pamoja na kuchukua hatua mbalimbali za maboresho katika Bandari ya Dar es Salaam, bado ufanisi wa utoaji huduma za bandari haujafikia viwango vya kimataifa.

Anasema, hali ya sasa ya utendaji wa Bandari ya Dar es Salaam imeendelea kuwa ya kiwango cha chini ikilinganishwa na bandari shindani kikanda.

Alisema kwamba, ufanisi mdogo katika Bandari unaongeza gharama.

“Athari za kutokuwa na ufanisi katika Bandari ya Dar es Salaam ni pamoja na meli kusubiri muda mrefu nangani jambo ambalo linatokea mpaka sasa, ambapo linasababisha kuongezeka kwa gharama za kutumia Bandari ya Dar es Salaam,” alisema Mbossa.

Alisema kwamba, kutokana na meli kusubiri siku nyingi nangani bila kupakua au kupakia mizigo, Serikali inalazimika kulipa Shs. milioni 58 kwa siku kwa meli kusubiri nangani.

“Gharama ya meli kusubiri nangani kwa siku moja ni takribani Dola za Kimarekani 25,000 ambayo ni sawasawa na Shs. milioni 58 kwa siku, maana yake kwa meli 30 tulizonazo sasa nangani maana yake ni kwamba kwa mwezi mmoja tunalipa Dola milioni 22.5 (takriban shilingi bilioni 56.25) kutokana na meli kusubiri nangani, na fedha hizi zinalipwa kwa fedha za kigeni,” alisema.

Alisema, kwa sasa meli zinasubiri nangani hadi siku 10 bila kuhudumiwa, jambo linaloongeza gharama za uendeshaji na kupunguza hata mapato kidogo inayopatikana.

“Meli nyingi husubiri nangani kwa muda mrefu kabla ya kuhudumiwa. Mpaka sasa tunazo meli 29 zinazosubiri kuingia bandarini. Lakini katika gati 12 ambazo tunazo, tuna meli 12 ambazo zilihudumiwa. Mheshimiwa Rais, wastani wa meli kusubiri nangani ni siku 5 kwa kiwango cha chini hadi siku 10 ikilinganishwa na bandari za wenzetu kama Mombasa ambao wastani ni siku 1.25, lakini kwa Bandari ya Durban ni siku 1.6,” alisema Mbossa.

Mbossa alisema, kukosekana kwa ufanisi bandarini kunaongeza gharama ya maisha kwa wananchi.

“Ushafirishaji wa mizigo ya ndani ya takribani Dola 6,000 kwa kasha, fedha hizo zinapolipwa hupelekwa kwa mlaji wa mwisho ambaye ni mwananchi wa kawaida, kwamba chochote kinachosafirishwa kikabeba gharama kubwa, basi kila mwananchi hulipia gharama ile wakati ananunua bidhaa iliyosafirishwa,” amesema.

Aidha, alisema, Tanzania haipakui mizigo kulingana na viwango vya kimataifa kutokana na ufanisi mdogo wa Bandari.

“Muda wa kupakua gatini ni siku tano ukilinganisha na siku moja moja inayokubalika kimataifa, na hili ni kutokana na uduni wa vifaa tulivyonavyo, lakini pia inapelekea meli kubwa kutokuja katika bandari yetu ya Dar es Salaam kwa sababu huduma hutolewa kwa muda mrefu,” anasema.

Alisema, hali hiyo imetokana na kukosekana kwa uwekezaji mkubwa kwa muda mrefu ambao ungeweza kuchochea kuongeza idadi ya gati.

“Tunazo gati 12 tu katika Bandari ya Dar es Salaam. Lakini tunazo meli 30 ambazo zinasubiri kuingia. Lakini pia ni lazima uhudumie meli zile kwa wakati ili uweze kuingiza meli nyingine,” anasema.

Akaongeza: “Kukosekana kwa mitambo ya kisasa ya kutosha ya kuhudumia shehena ambayo teknolojia yake inabadilika mara kwa mara pia ni sababu inayosababisha changamoto kubwa katika uendeshaji wa Bandari ya Dar es Salaam.”

Akaongeza: “Hali ya kukosekana kwa ufanisi katika Bandari ya Dar es Salaam inaongeza gharama katika mnyororo mzima wa usafirishaji kutoka nje ya nchini ukipitia katika bandari yetu kwenda katika nchi za jirani. Mfano, gharama ya kusafirisha kasha moja kutoka nje ya nchi kwenda DRC zinafikia takribani Dola za Kimarekani 12,000, hii ni gharama kubwa sana ukilinganisha na bandari shindani za Mombasa, Beira, Maputo na Durban, ambazo ni wastani wa nusu wa gharama ambazo tunatumia kupitisha mizigo katika Bandari ya Dar es Salaam.”

Mbossa, alisema, mkataba huo, ambao ni wa miaka 30, hauhusishi eneo lote la Bandari ya Dar es Salaam na akasisitiza kwamba, maslahi ya watumishi wa sasa wa TP yamezingatiwa na watakuwa na nafasi ya kuchagua kubaki TPA au kuhamia kwenye kampuni ya DP World, ambayo itahitaji rasilimali watu kutoka hapa nchini, kwa mujibu wa mikataba ya kimataifa.

“Mikataba hiyo mitatu imezingatia masuala mbalimbali ndani yake kwa ajili ya maslahi mapana ya nchi yetu. Moja, ni kuhusisha baadhi ya magati ya Bandari ya Dar es Salaam na siyo magati yote, pia haihusishi Bandari zingine za Mwambao wa Maziwa Makuu ya Victoria, Tanganyika na Nyasa,” alisema.

Katika suala la ulinzi na usalama, Mbossa alisema, eneo lote la Bandari na maeneo yale yaliyokodishwa katika kampuni ya DP World yataendelea kubaki chini ya uangalizi wa Serikali.

Aliongeza kwamba, mwekezaji atalipa kodi zote za Serikali kwa kuzingatia Sheria za Tanzania, na Sheria za Tanzania ndizo zitakazotumika katika utekelezaji wa mikataba yote hiyo.

“Pia Serikali ya Tanzania itakuwa na Haki ya kujiondoa pale itapoona inahitaji kufanya hivyo,” alisema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *