Maambukizi mapya VVU yapungua-Utafiti

Na Sarah Moses, Dodoma

TAARIFA za Utafiti wa Viashiria na Matokeo ya VVU na UKIMWI nchini mwaka 2022/2023 zimekamilika, zinatarajiwa kutolewa Desemba Mosi, 2023 mkoani Morogoro katika Siku ya UKIMWI Duniani.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu,Sera,Bunge na  Uratibu, Jenista Mhagama, aliyasema hayo jana jijini Dodoma alipozungumza na wanahabari.

Utafiti huo unaonesha Tanzania imepata matokeo chanya kutokana maambukizi mapya ya Virusi vya UKIMWI kuendelea kupungua ikilinganishwa na utafiti uliofanywa 2016/2017.

Alisema hayo ni mafanikio mazuri ambayo Serikali ya Awamu ya Sita imeyafikia kuelekea kufikia malengo ya kitaifa ya kufikia SIFURI TATU yaani kutokuwa na maambukizi mapya, kutokuwa na unyanyapaa, ubaguzi, kutokuwa na vifo vitokanavyo na UKIMWI. 

Lengo la utafiti huo ni kupima mwenendo wa maambukizi mapya  ya Virusi vya UKIMWI nchini, kuisaidia nchi kuchukua hatua katika mapambano dhidi ya virusi vya UKIMWI na UKIMWI, kujitathimi. 

“Pia lengo lingine ni kupima matokeo ya juhudi za mapambano dhidi ya UKIMWI, kupitia utafiti huu, tutapata taarifa kuhusu viashiria na matokeo ya VVU/UKIMWI katika nchi yetu 2022/23.

“Hivi ni takwimu muhimu kuhusu hali ya UKIMWI nchini,” aliongeza.

Mhagama alisema, utafiti uliokamilika ni wa tano, nchi hufanya tafiti kila baada ya miaka mitano ili kujipima katika mapambano dhidi ya UKIMWI.

Utafiti huo umeshirikisha Wataalam mbalimbali wa Tanzania Bara, Zanzibar na kutoka nje ya nchi.

“Kwa taratibu zilizopo, huwa tunaanza kutoa taarifa kisha baada ya muda tunatoa matokeo, kwa Serikali yetu huu utafiti si wa kwanza imekuwa ikifanya utafiti kila baada ya miaka mitano.

“Utafiti wa mwisho ulifanyika 2016/2017 lengo ni kujaribu kupima matokeo ya juhudi zero ndani ya taifa, kupambana dhidi ya UKIMWI,” aliongeza.

Alibainisha kuwa, utafiti huo umefanywa na Serikali ya Tanzania kupitia Tume ya Taifa ya Kudhibiti UKIMWI, Tume ya Kudhibiti UKIMWI Zanzibar, Ofisi ya Taifa ya Takwimu,Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Zanzibar kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali za ndani na nje ya Serikali zikiwemo Kituo cha Kudhibiti Magonjwa na Kinga na Chuo Kikuu cha Columbia.

Hata hivyo, aliwataja wadau wengine ni Mpango wa Taifa wa Kudhibiti UKIMWI na Mpango Jumuishi wa kupambana na UKIMWI, Homa ya Ini, Kifua Kikuu na Ukoma akifafanua kuwa, kazi hiyo imefanyika kwa ufadhili wa Mpango wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kudhibiti UKIMWI. 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *