Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania Bara kuanza Des. 20

Na Badrudin Yahaya

LIGI Kuu ya Soka ya Wanawake ya Tanzania Bara, inatarajia kuanza Desemba 20 ambapo mabingwa watetezi, timu ya JKT Queens itafungua dimba kwa kuumana na Bunda Queens.

Mbali na mechi hiyo lakini kutakuwa na mechi nyingine nne za mzunguko wa kwanza ambapo Simba Queens itaumana na Ceasia Queens huku Allience Girls wakianza na Geita Gold Queens, Foutaine Gate Queens wao watacheza na Amani Queens na mechi zote hizi zitapigwa siku ya ufunguzi.

Mchezo wa mwisho kwa raundi ya kwanza utapigwa Desemba 21 ambapo Baobao Queens watawaalika Yanga Princess katika Uwanja wa Jamhuri, Dodoma.

Macho na masikio ya wengi yataelekezwa katika mechi ya Kariakoo Dabi kwa upande wanawake ambapo Januari 3, Simba Queens watakuwa ni wenyeje wa Yanga Princess.

Mchezo huo unatarajia kuvuta hisia za watu wengi wa soka nchini hasa ukikumbuka matokeo ya kichapo cha mabao 5-1 walichopata Simba kutoka kwa Yanga katika mechi za timu za wanaume.

Wawili hao watarudiana tena Machi 22 mwakani ambapo Yanga Princess watakuwa wenyeji katika mchezo huo.

Ligi hiyo inatarajia kufika tamati Mei 17 ambapo Yanga Princess watafunga dimba dhidi ya Allience huku Simba Queens wakifunga dimba na Geita Gold Queens.

JKT Queens ndio mabingwa watetezi wa michuano hiyo na hivi karibuni wametoka kuiwakilisha nchi katika michuano ya ligi ya mabingwa Afrika upande wa wanawake.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *