Na Asha Kigundula
LIGI Kuu ya Tanzania Bara msimu wa 2023/24, itaanza rasmi Agosti 15, Bodi ya hiyo (TPLB), imetangaza.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na bodi hiyo Dar es Salaam jana kupitia Ofisa Habari wake, Karim Boimanda, ligi hiyo ambayo kwa ubora Afrika inashika nafasi ya 5 na duniani nafasi ya 39, itafikia tamati Mei 25, mwakani.
Amesema mbali na ligi hiyo ligi nyingine ni Championship ambayo yenyewe inatarajia kuanza rasmi Septemba 2 na kumalizika Mei 25, mwakani na First League itaanza Oktoba 22 na itamalizika Machi 23, mwakani.
Hata hivyo mchezo wa ufunguzi wa ligi hiyo ambao ni Ngao ya Jamii utachezwa Agosti 9 kwa kuzikutanisha timu za Yanga itakayoumana na Azam FC.
Mchezo mwingine utazikutanisha timu za Simba SC dhidi ya Singida Fountain Gate Agosti 10 ambapo timu itakayosonga mbele itacheza fainali na zile zilizofungwa zitawania mshindi wa tatu.
Hivi sasa klabu mbalimbali zinaendelea na kufanya maboresho kuelekea msimu mpya baada ya dirisha la usajili kufunguliwa rasmi Julai Mosi na linatarajia kufungwa Agosti 30.
Wakati msimu mpya ukienda kuanza, Yanga ndiye bingwa mtetezi wa Ligi Kuu Bara, Ngao ya Jamii na michuano ya ASFC.