LONDON, England
KIUNGO Romeo Lavia, yupo tayari kujiunga na Chelsea licha ya Liverpool kuwa tayari kutoa pauni milioni 60 ili kumsajili nyota huyo wa Southampton.
Hakuna makubaliano yalifikiwa kati ya Southampton na Chelsea hadi sasa juu ya kiungo huyo lakini inaelezwa hakuna mazungumzo.
Vyanzo mbalimbali viliiambia Sky Sports News kuwa Liverpool na Soton walishakubaliana kila kitu kwa uhamisho uliokadiriwa kufikia thamani ya pauni milioni 60.
Liverpool tayari imeshindwa kumsajili Moises Caicedo ambaye amejiunga na Chelsea baada ya kiungo huyo wa Brighton kutimkia Stamford Bridge kwa uhamisho ulioweka rekodi Uingereza wa pauni milioni 115.
Miamba hiyo ya Anfield imekubali ofa ya pauni milioni 111 ambayo ilipokelewa na Brighton kwa nyota huyo, 21 ambaye aliweka wazi kuwa anataka kujiunga na Chelsea.
Southampton iliweka wazi kuwa thamani ya Lavia, 19 ni pauni milioni 50. Wiki iliyopita Chelsea iliwasilisha pauni milioni 48 wakati Liverpool ilishatuma ofa zao mara tatu na kukataliwa.
Chelsea inataka kusajili viungo wawili katika dirisha hili na mazungumzo kati ya yao na Leeds United juu ya kumsajili Tyler Adams yalivunjika wiki iliyopita baada ya pande hizo kushindwa kufikia mwafaka.
Lavia amebakiwa na mkataba wa miaka minne ndani ya Southampton baada ya kujiunga nayo akitokea Manchester City msimu uliopita ambapo anatarajia kuachana na Soton baada ya msimu uliopita kushuka daraja.
Nyota huyo wa kimataifa wa Ubelgiji, hakuingia wakati Soton ikiibuka na ushindi katika mchezo wao wa kwanza wa Championship dhidi ya Sheffield Wednesday huku pia akiwa si sehemu ya kikosi ambacho kilitoka sare ya mabao 4-4 na Norwich mwishoni mwa wiki.