Kuziona Yanga, Kaizer Chiefs ‘buku 10’

Na Asha Kigundula

KLABU ya Yanga, imeweka wazi viingilio vya mchezo wao wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini kuwa cha chini ni sh. 10,000 katika kilele ya Tamasha la Wiki ya Wananchi.

Tamasha hilo litafanyika Julai 22 Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam ikiwa maalum kwa ajili ya kutambulisha wachezaji wao wapya.

Akizungumza Dar es Salaam jana wakati wa utiaji saini wa ushirikiano baina yao na Benki ya CRDB katika Wiki ya Wananchi, Ofisa Habari wa timu hiyo, Ally Kamwe, amesema wiki hiyo itazinduliwa jijini Mwanza kuanzia Julai 15.

Amesema wiki hiyo itakuwa na matukio mbalimbali kabla ya kufika kilele chake ambapo kutakuwa na mechi hiyo ya kirafiki ya kimataifa.

“Viingilio katika mchezo huo ni sh. 10,000 kwa mzunguko, VIP C-2 sh. 20,000 na VIP C-1 sh. 30,000, VIP B sh. 40,000, VIP A sh. 100,000, Royal sh.300,000 na VVIP sh. 500,000,” amesema Kamwe.

Amewataja baadhi ya wasanii watakaotoa burudani siku hiyo ni Sholo Mwamba, Madee Ali, Billnass na Rayvanny.

Akizungumza kwa niaba ya wasanii wenzake, Billnass, amesema kikubwa mashabiki wake na wa timu ya Yanga wakutane katika Viwanja wa Furahisha jijini Mwanza kwa ajili ya ufunguzi wa Wiki ya Wananchi kwani atatoa burudani ya nguvu.

Kwa upande wa Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo, Andrew Mtine, amesema wameingia makubaliano hayo na CRDB kwaajili ya Wiki ya Wananchi ambayo kilele chake kitakuwa ni Julai 22 na siku hiyo watakuwa wameandaa mambo mengi mazuri ambayo huwa yanafanyika kama kawaida.

Amesema mashabiki waje kuona timu yao inavyotambulisha wachezaji wapya katika kilele cha siku hiyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *