Kupitishwa kwa Sheria ya Uwekezaji wa Umma kutasukuma maendeleo nchini

Na Daniel Mbega, Dar es Salaam

“WAZIRI kaniambia ile Sheria ya Msajili wa Hazina tayari imeshakamilika na iko tayari kusomwa kwa mara ya pili Bungeni. Kwahiyo naomba wabunge nendeni kaijadilini, mnapoona hapako vizuri turekebisheni, lakini ile sheria ipite ili apate mwongozo wa kumwongoza huyu (Msajili wa Hazina).

“Lakini jingine tuweze kuwa na uwezo sasa wa kuanzisha Mfuko wa Uwekezaji. Tutakapoanzisha Mfuko wa Uwekezaji nchini, wetu, ndipo mashirika yetu haya ambayo yako 100% ya Serikali wanaweza kupata mtaji na kuweza kuendelea na kazi zao. Mtaji wenye usalama kabisa.”

Haya ni maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan, aliyoyatoa jijini Dar es Salaam Juni 11, 2024 wakati akipokea Gawio la Serikali kutoka kwa Mashirika ya Umma na Taasisi ambazo Serikali ina hisa kidogo.

Rais Samia, ambaye ni muumini wa mageuzi ya kiuchumi, alitoa kauli hiyo wakati akirejelea takwimu zilizotolewa siku hiyo wakati anapokea gawio la jumla ya Shs. 637,122,914,887.59 ikijumuisha gawio la Shs. 278,868,961,122.85 kutoka katika mashirika ya biashara na michango Shs. 358,253,953,764.74 kutoka katika taasisi nyingine, yakiwa ni makusanyo kwa kipindi cha Julai 2023 hadi mwezi Mei 2024.

Na alisema hivyo huku akiyahimiza mashirika ambayo yana umiliki wa asilimia 100 wa Serikali, hasa yanayofanya biashara, yaongeze jitihada na ubunifu katika kuzalisha ili yalete tija kama yale ambayo Serikali ina hisa chache.

Si hivyo tu, pia alihimiza Bodi za Mashirika ya Umma ziwajibike na kuyasimamia mashirika hayo kwa weledi, ili hatimaye faida ya uwepo wa mashirika hayo ionekane.

Lakini pia akaridhia maombi ya Msajili wa Hazina, Nehemia Mchechu, na Mwakilishi wa Wenyeviti wa Bodi za Mashirika ya Umma, Mkuu wa Majeshi mstaafu Jenerali Venance Mabeyo, la kutaka Wajumbe wa Bodi za Mashirika ya Umma waombe na wafanyiwe usaili ili kuwezesha mashirika kupata wajumbe watakaoongeza tija katika usimamizi wa taasisi hizo.

“Wajumbe wa bodi watashindana kupata nafasi ya bodi. Ile mambo ya angalau hata bodi yasiwepo… mimi mtaniachia uteuzi wa wenyeviti, ili ziwe na watu ambao wanajua mambo yanayoendelea,” akasema.

Muswada wa Sheria Mpya ya Uwekezaji wa Umma ulisomwa Bungeni kwa mara ya kwanza Ijumaa, Novemba 10, 2023, na kupitishwa kwake kuwa Sheria siyo tu kutampa mamlaka Msajili wa Hazina wa kuyasimamia kwa tija, lakini pia utaondoa ukiritimba ambao mara nyingi unakwambia ufanisi kwenye mashirika hayo.

Uwekezaji wa Serikali upo katika taasisi na mashirika takriban 298, ambapo kati ya hayo, 248 ni taasisi, mashirika ya umma na wakala za Serikali ambapo zote ziko ndani ya nchi, na 50 ni kampuni ambazo Serikali ina hisa chache, kati yake 40 ziko ndani ya nchi na 10 ziko nje ya nchi.

Uchunguzi unaonyesha kwamba, taasisi, mashirika na wakala za Serikali 213 zinajihusisha na utoaji wa huduma wakati 35 zinafanya biashara, wakati ambapo kampuni 50 zote ambazo Serikali ina hisa kidogo, zinajihusisha na biashara.

Serikali imefanya uwekezaji wa Shs. trillioni 73 katika taasisi, mashirika ya umma na Wakala za Serikali 298 zinazofanya shughuli mbalimbali.

Endapo Sheria hiyo itapitishwa, ni dhahiri kwamba, baada ya miaka mitano, baadhi mashariki yanakwenda kufanya vizuri, watendaji wa mashirika hayo watapimwa kwa ufanisi wa kazi ili kuhakikisha wanafikia malengo yaliyowekwa.

Vipengele vilivyomo kwenye Muswada huo ambao ukipitishwa utakuwa Sheria vinawataka wakurugenzi wa mashirika ya umma kufanya kazi wa weledi ili kuhakikisha wanapata mafanikio katika utendaji wao.

Sheria hiyo inapaswa kuipa Mamlaka ya Uwekezaji wa Umma, mamlaka ya kuidhinisha stahili za wajumbe wa Bodi za Taasisi, kwa sababu kwa sasa Msajili wa Hazina hana mamlaka ya kuidhinisha viwango vya stahili za wajumbe wa Bodi, na hivyo kushindwa kutoa motisha kwa Bodi zenye ufanisi na hivyo kuathiri utendaji.

Sheria inayopendekezwa inapaswa kujumuisha majukumu yaliyorithiwa kutoka Consolidated Holding Corporation (CHC), ambayo yalihamishiwa Ofisi ya Msajili wa Hazina kupitia Tangazo la Serikali Na. 203 la Mwaka 2014, haya hivyo hadi sasa majukumu hayo hayajajumuishwa kwenye Sheria.

Sheria inayopendekeza inapaswa kuipa Mamlaka ya Uwekezaji wa Umma, mamlaka ya kutoa miongozo ya usimamizi na uendeshaji wa Taasisi kwani kwa sasa Ofisi ya Msajili wa Hazina haina mamlaka ya kutoa miongozo ya kusimamia utendaji na uendeshaji wa Taasisi, badala yake Msajili wa Hazina ana uwezo wa kutoa miongozo ya kiutumishi tu kwa mujibu wa Kanuni za Utumishi wa Umma.

Kutoogopa kelele

Katika ‘kumkabidhi rasmi rungu’ Msajili wa Hazina, Rais Samia alimtaka afanye kazi bila kuogopa vikwazo anavyowekewa au kelele anazopigiwa.

“Kwenye mageuzi haya Mchechu na Waziri wako lazima muwe unpopular, sijawahi kusikia Waziri wa Fedha akasifiwa hata siku moja, siku zote Waziri wa Fedha analaaniwa, kwahiyo Mchechu na wewe utalaaniwa tu hapa, na nyingine zitakuja personal, nyingine kikazi, lakini hii ndiyo kazi niliyokupa, simama na ifanye,” akasema.

Akasema, yeye binafsi anatukanwa sana mitandaoni, lakini amejigeuza chura anajifanya hasikii na wala hatojibu bali anachotaka yeye ni mageuzi ya kiuchumi ili kuipeleka Tanzania mbele.

Lakini Rais Samia akatoa mifano ya jitihada zake namna zinavyozaa matunda, huku Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), ambayo wengi walimbeza na kuzua taharuki alipokaribisha uwekezaji wa kampuni ya DP World kutoka Dubai, ikiwa kinara katika ongezeko la gawio mwaka huu.

Akasema: “Wale waliopiga kelele Mama kauza bahari, Mama kauza bandari, Mama kauza nini – mauzo yale faida yake ni hii leo (TPA kuongeza mapato). Huu ni mwanzo, tunatarajia mtapata faida kubwa zaidi kwa bandari zetu kubwa zote ambazo ziko nchini.”

TPA iliongoza kundi la taasisi zisizo za biashara lilonajumuisha Mashirika ambayo kwa mujibu wa Sheria ya Msajili wa Hazina na Sheria ya Mashirika ya Umma zinawajibika kutoa michango ya asilimia 15 ya mapato ghafi baada ya kutoa gawio la Shs. bilioni 153.9, ikifuatiwa kwa mbali sana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) iliyotoa Shs. bilioni 34.7, Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) iliyotoa Shs. bilioni 21.3, Wakala wa Huduma za Meli (TASAC) ilitoa Shs. bilioni 19.1, na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) ukatoa Shs. bilioni 18.9.

Kwa kundi la taasisi za kibiashara linalojumuisha Mashirika na Kampuni ambazo kwa mujibu wa Sheria ya Mashirika ya Umma na Sheria ya Makampuni, zinawajibika kutoa gawio kwa wanahisa, Benki ya NMB ndiyo iliyoongoza kwa kutoa Shs. bilioni 54.5, ikifuatiwa na Twiga Minerals (ya ubia baina ya Serikali na Barrick Gold) iliyotoa Shs. bilioni 53.4, Airtel Tanzania (Shs. bilioni 40.8), Puma Energy (Shs. bilioni 12.2), na Kiwanda cha Sukari cha TPC Moshi kilitoa Shs. bilioni 10.2.

Hali siyo nzuri

Kwa upande wake, Msajili wa Hazina, Nehemia Mchechu, alisema hali siyo nzuri kwa mashirika na taasisi za umma kwa sababu kati ya mashirika 304, ni mashirika 145 pekee yaliyotoa gawio la Shs. bilioni 637 kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali ilhali mashirika 159 hayakutoa kitu kabisa.

Akasema pia kwamba, mwaka 2023 jumla ya mashirika 109 ndiyo yaliyotoa gawio, hivyo mwaka huu kuna ongezeko la mashirika 36 huku akisisitiza kwamba, hali hiyo hairidhishi.

Akasema mafanikio hayo ni somo ambalo Serikali ina kila sababu ya kujifunza namna taasisi zake zinavyoendeshwa kwa sababu uwekezaji wa Serikali katika kampuni na mashirika hayo ni Shs. 3 trilioni. Kwa ujumla, Serikali imewekeza Shs. 76 trilioni kwenye mashirika na taasisi mbalimbali.

Mchechu akasema, mwaka 2019/2020, 2020/2021, na 2021/2022 mashirika ya umma yalichangia Shs. 255 bilioni, Shs. 161 bilioni na Shs. 207 bilioni, mtawalia, huku kampuni na mashirika ambayo Serikali ina hisa chache yakichangia gawio dogo la Shs. 44 bilioni, Shs. 147 bilioni na Shs. 10 bilioni mtawalia.

Lakini akasema, kwa miaka miwili 2022/2023 na 2023/2024 gawio kwa mashirika ya umma yanayofanya biashara lilikuwa Shs. 109 bilioni na Shs. 110 bilioni mtawalia; huku ambako Serikali ina hisa chache yakichangia Shs. 219 bilioni na Shs. 168 bilioni kwa kipindi hicho.

“Matokeo haya kwetu yanaleta fikra mchanganyiko, ni habari njema kwa kuwa inaonyesha uwezeshaji unaofanywa na Serikali kuendeleza mazingira wezeshi ya biashara, kampuni binafsi inapofanya kazi na kupata faida, mazingira ni mema,” akasema Mchechu.

Akasema, faida katika biashara ya sekta binafsi ni kipimajoto cha mafanikio ya Serikali kuboresha mazingira ya biashara na sera za kiuchumi huku akiwataka viongozi waliochaguliwa kuongoza mashirika ya umma kufanya vizuri zaidi kwa faida ya Taifa na wananchi.

“Kama tutazingatia Shs. 850 bilioni mwaka hadi mwaka inawezekana tukawa na furaha, lakini kama tutaangalia kiwango hiki tunachotoa sasa kwa malengo tuliyopatiwa tukiwa Arusha ya mapato yasiyo ya kikodi yafikie asilimia 10 ya kikodi tuko mbali sana, mwaka jana tulikuwa asilimia tatu na mwaka huu tupo asilimia tatu,” akasema.

Mchechu akasema ni lazima ukuaji uwe wa wastani wa asilimia kati ya 60 hadi 70 ili kufikia malengo ya mapato yasiyo ya kikodi kwa asilimia 10.

“Hali si nzuri kwa sababu bado hatuendani na kasi na maono ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuleta maendeleo kwa kasi nchini, maendeleo yote yanategemea fedha, chanzo cha fedha ni vitu vitatu, Serikali kukopa, kukusanya kodi au kupata mapato yasiyo ya kikodi. Asilimia 90 ya mapato yasiyo ya kikodi hupatikana kupitia gawio,” akasema.

Mchechu alieleza baadhi ya mafanikio ambayo Ofisi ya Msajili wa Hazina imeyapata kwamba, imeendelea kushawishi kufanyika kwa mabadiliko katika sheria yake ili kuanzishwa kwa Mamlaka ya Uwekezaji wa Umma, muswada ambao ulipelekwa Bungeni na kusomwa kwa mara ya kwanza Novemba 10, 2023.

“Ni wazi kuwa tunahitaji sheria inayojitosheleza itakayoweza kusaidia kuleta tija katika uwekezaji mkubwa wa zaidi ya Shs. 76 trilioni uliofanywa na Serikali kwa niaba ya Umma wa Watanzania,” akasema Mchechu.

Mchechu alisema, katika kuimarisha utawala bora na tija ya mashirika ya umma, Ofisi ya Msajili imezindua na kuanza kutumia mfumo wa kidijitali wa kufanya tathmini ya bodi hali ambayo imewezesha kukamlisha tathmini kwa wakati na kwa mawanda tarajiwa.

Akasema, Ofisi imeanza kutumia vigezo vipya vya uendeshaji wa mashirika (Key Performance Indicators) vilivyoingiwa kwa njia ya mikataba baina ya wenyeviti wa Bodi na Msajili wa Hazina, vigezo ambavyo vimeboreshwa zaidi na vimezingatia mgawanyo wa kisekta na majukumu ya msingi ya taasisi.

“Tupo katika hatua za mwisho za kuwa na mfumo thabiti wa kuripoti (dashboard) taarifa za kiutendaji za wakuu wa taasisi kwa wakati na za kuaminika ili kuwezesha kufanyika maamuzi sahihi kwa wakati (informed decision making) kwa mamlaka za uteuzi.

“Ofisi pia imefanikiwa kupitia mikataba mbalimbali ya kibiashara na pia kufanya mazungumzo na wabia wetu kwenye sekta nyeti za uchumi; kwenye sekta ya madini kumekuwa na mzungumzo mbalimbali tukishirikiana na Wizara ya Madini na tumeweza kuongeza hisa za serikali katika baadhi ya kampuni, mathalani, tumeongeza hisa za serikali katika kampuni ya madini ya Sotta kutoka 16% hadi 20%, jambo litasaidia sana katika majadiliano ya mikataba mingine ambayo tupo katika mazungumzo.

“Pia tumekamilisha majadiliano na kuingia mikataba mipya ya wanahisa na makampuni kama NMB, NBC na MCCL kati ya mikataba mingi inayofanyiwa kazi, na kampuni ya MCCL imeweza hatimaye kupata faida mwaka huu na kutoa Gawio kwa wanahisa mwaka huu baada ya kipindi cha miaka 10,” akafafanua Mchechu.

Sheria madhubuti

Sheria ambayo Rais Samia analiomba Bunge liijadili na kuipitisha itakuwa msaada mkubwa wa kuimarika kwa uwekezaji nchini, hasa kwenye mashirika, taasisi na wakala mbalimbali na hivyo kuleta tija.

Siyo siri kwamba, ufanisi na tija inayopatikana kutoka baadhi ya taasisi haukidhi kabisa malengo ya uanzishaji wake na Serikali, kwa kifupi, haipati matokeo yanayotarajiwa kwenye uwekezaji wake.

Hii inatokana na upungufu uliomo katika Sheria ya Msajili wa Hazina, ambapo pamoja na mambo mengine, inakosa kifungu mahsusi kinachompa Msajili wa Hazina mamlaka ya kuwekeza katika maeneo kadha wa kadha, hususan maeneo ya kimkakati ili kuendana na mazingira ya sasa na mabadiliko ya kiuchumi duniani.

Lakini mapungufu mengine ni kukosa mamlaka ya kusimamia masuala muhimu kwenye uendeshaji wa Taasisi ili kupata matokeo chanya katika ufanisi na utawala bora kama vile Ofisi ya Msajili kutokushirikishwa kikamilifu katika mchakato wa uteuzi wa wajumbe wa Bodi na watendaji wakuu wa taasisi hizo.

Uchunguzi unaonyesha pia kwamba, hakuna chanzo cha uhakika na endelevu cha mitaji ya uwekezaji kwenye taasisi hizo na uendeshaji wa shughuli za ofisi, pamoja na wigo finyu wa uwekezaji ambao kimsingi unaathiri uwezo wa Serikali kupata na kutumia fursa za uwekezaji zinazojitokeza kwa wakati.

Ikiwa itakuwepo Sheria madhubuti ya Uwekezaji wa Umma, ni wazi kwamba kutakuwepo na muundo mpya wa taasisi husika au uimarishaji wake pamoja na kuwepo kwa Mfuko wa Uwekezaji, ambao utaipunguzia mzigo Serikali kwa namna moja au nyingine.

Kwa sasa, Sheria ya Mamlaka na Majukumu ya Msajili wa Hazina, Sura 370 haibainishi vyanzo vya fedha za mitaji kwa ajili ya uwekezaji katika Taasisi na maeneo mengine.

Faida za kuanzisha Mfuko wa Umma ni nyingi, lakini baadhi ni kwamba, Serikali itaweza kufanya uwekezaji wa kimkakati kwa wakati (Timely Strategic Investment Decision), itaongeza ufanisi wa uendeshaji (operational efficiency), itaokoa Mashirika ambayo bila Mfuko huo yanaweza kuanguka, na itawezesha Mashirika ya umma kustahimili ushindani.

Jambo muhimu hapa ni kwamba, Sheria hiyo ya Uwekezaji wa Umma lazima impe mamlaka Msajili wa Hazina katika usimamizi pamoja na mambo mengine, hali ambayo italeta ufanisi mkubwa na matokeo chanya.

Sheria hiyo lazima ibainishe mamlaka ya kusimamia masuala muhimu ya uwekezaji kwenye taasisi na kiwepo chanzo cha uhakika na endelevu cha mitaji ya uwekezaji.

Aidha, Sheria hiyo inapaswa pia kuwa na kipengele cha masharti ya uwajibikaji kwa Msajili wa Hazina na iondoe mwingiliano wa kimamlaka katika kutoa maelekezo ya jumla au mahsusi kwa taasisi.

Dhamira hiyo njema ya Serikali inamaanisha kwamba kwa Sheria mpya, Ofisi ya Msajili wa Hazina inaweza kubadilishwa jina na kuundwa kwa Mamlaka ya Uwekezaji wa Umma (Public Investment Authority – PIA) ili kuakisi majukumu na mwenendo wa ukuaji wa uchumi wa duniani, huku ikiendelea kusimamia utendaji wa taasisi zote za umma na kuwekeza katika taasisi na kusimamia uwekezaji huo, wigo ambao kwa sasa ni finyu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *