Na Salha Mohamed, Dar es Salaam
SHIRIKA lisilo la kiserikali la Uzalendo na Uraia Tanzania, linatarajia kufanya kongamano la vijana kuhusu uzalendo litakalowakutanisha wanafunzi zaidi ya 500 wa vyuo vya elimu ya juu jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa shirika hilo, Musa Kitungi, aliyasema hayo jana wakati akizungumza na Tanzania Leo.
Alisema shirika hilo hutoa elimu ya maadili, kuhamasisha masuala ya uzalendo kwa vijana, elimu ya uongozi na kuelimisha watu kuhusu uraia.
Alieleza kuwa, kongamano hilo litafanyika kesho katika Ukumbi wa Nyerere Theatre I, uliopo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Mlimani.
“Walengwa ni wanafunzi wote wa elimu ya juu ambao ni wanafunzi na vijana ambao ndiyo tegemeo kubwa kwa taifa katika kuhamasisha masuala ya maadili, uzalendo katika taifa letu,” alisema.
Aliongeza kuwa, lengo la kongamano hilo ni kutoa elimu, mafunzo ya uzalendo na maadili kwa wanafunzi wa elimu ya juu katika Mkoa wa Dar es Salaam.
“Ili kulifanikisha na kuliendea lengo kuu, kuna malengo madogo madogo ya kufanyiwa kazi ambayo ni kutoa elimu na kuhamasisha uzalendo kwa vijana.
“Kutoa elimu na kuhamasisha maadili kwa vijana , kuonesha mchango wa ulendo na maadili katika amani, umoja, mshikamano , ulinzi, usalama wa nchi,” alieleza.
Kitungi aliwakumbusha wanafunzi wajibu wao wa kuelimisha wengine, kuhamasisha uzalendo na maadili nchini , kutengeneza daraja lenye tija kiutendaji kati ya wanafunzi wa elimu ya juu, jamii na serikali, kujenga uelewa kuhusu usalama wa masuala ya utawala bora.
Alifafanua kuwa, mada mbalimbali zitatolewa ikiwemo maadili kwa viongozi, matumizi ya mtandao, namna ya kujenga uzalendo na umuhimu wake kwa vijana, haki za binadamu, utawala bora kwa wanafunzi, rushwa katika taasisi za elimu ya juu, madhara yake, namna ya kuzuia.
“Tunaamini kongamano hili litapunguza mmomonyoko wa maadili nchini, vijana kuwa na uzo wa kutatua changamoto za kimaadili na uzalendo.
“Pia kurahisisha utendaji, ufanisi wa vyuo vya elimu ya juu katika kusimamia jukumu la elimu, malezi na maadili, kuandaa hazina ya vijana wazalendo wenye maadili ambao watachochea maendeleo ya nchi,” alisema.
Kitungi aliwakaribisha wanafunzi wa vyuo kujitokeza kwenye kongamano hilo ambalo ushiriki wake ni bure ambapo vyeti vitatolewa.