Kocha Taifa Stars ajivunia kambi ya Misri kujiandaa na AFCON

Na Badrudin Yahaya

Kocha wa kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, Adel Amrouche, amesema kambi ya Misri itawasaidia kujenga vyema kikosi chao ili kiweze kushiriki vyema michuano ya Afcon inayotarajiwa kuanza mapema mwezi huu.

Stars wanatarajia kutupa karata yao ya kwanza kwa kucheza na Morocco, Januari 17 kisha watavaana na Zambia, Januari 21 na kumaliza mechi za makundi Januari 24 kwa kucheza na DRC.

Akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam, Amrouche amesema maandalizi yao kwasasa nchini Tanzania yanaendelea vizuri lakini kambi ya Misri itawajenga zaidi kwakuwa pia watapata nafasi ya kucheza mechi ya kirafiki na wenyeji ambao nao ni washiriki wa michuano hiyo.

Kocha huyo hakusita pia kuipongeza serikali kwa jitihada zake katika kuhakikisha timu ya taifa inapata mahitaji yote muhimu kuelekea michuano hiyo.

“Kambi ya Misri itatuongezea kitu kikubwa kwasababu pia tutacheza mechi za kirafiki,” amesema.

Katika mkutano huo pia kocha ametangaza kikosi cha wachezaji 31 ambao watakuwa katika maandalizi kuanzia sasa mara baada ya kutoka Zanzibar.

Stars ilikuwa na kundi la wachezaji 53 kikosi cha awali lakini tayari wachezaji 22 wamekatwa na zoezi hilo litaendelea kwa kuwapunguza wengine wanne ili kuendana na mahitaji ya CAF ya wachezaji 27 kwenye michuano hiyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *