Na Badrudin Yahaya
SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), limemfungia mechi nane Kocha wa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, Adel Amrouche.
Adhabu hiyo imetolewa mara baada ya CAF kupokea malalamiko kutoka kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Morocco (MRFF).
Amrouche ambaye yupo na kikosi cha Taifa Stars nchini Ivory Coast kabla ya kucheza mechi ya kwanza ya michuano hiyo dhidi ya Morocco, alitoa madai kuwa wapinzani wake hao huwa wanaushawishi ndani ya CAF kitu kinachofanya wanapendelewa katika baadhi ya maamuzi.
Madai hayo hayawakufurahisha Morocco ambao waliamua kuchukuwa hatua ya kumshitaki CAF na kisha kutolewa kwa adhabu hiyo.
Wakati huo huo, Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), kupitia Kamati yake ya Nidhamu, wamemsimamisha kazi kocha huyo kwa kipindi kisichojulikana.
Kutokana na uamuzi huo, TFF sasa wamemteua Kocha, Hemed Suleiman ‘Morocco’ kuwa Kaimu kocha Mkuu kwa michezo iliyobaki.
Stars ambao ilifungwa 3-0 na Morocco katika mechi ya kwanza ya AFCON, inatarajia kucheza dhidi ya Zambia Jumapili na kisha watavaana na DR Congo katika mchezo wa mwisho hatua ya makundi Januari 24.