
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
RAIS wa Jumuiya ya Wanafunzi wa elimu ya Juu Tanzania (TAHLISO) ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kampeni ya Kitaifa ya Mama Asemewe, Geofrey Kiliba, amesema jumuiya hiyo kwa pamoja wameibeba ajenda ya kushiriki kikamilifu katika uchaguzi Mkuu wa Tanzania pamoja na kushiriki katika kuhakikisha amani, utulivu na usalama unakuwepo siku ya Oktoba 29, 2025.
Kiliba ameyasema hayo leo Oktoba 24, 2025 wakati wa kongamano la amani ililoandaliwa na jumuiya hiyo chini ya uratibu wake, akisisitiza kuwa hawajatishika kushiriki katika uchaguzi huo kutokana na kauli ya Rais Samia ambaye pia ni Amiri Jeshi Mkuu wa Tanzania, akisema wamekubaliana kuwa Oktoba 29 ni siku ya kuwajibu wale wote wanaotishia amani nchini.
“Mgeni rasmi nikuambie kuwa tumejipanga sisi vijana wa Vyuo na Vyuo Vikuu maarufu kama GenZ kuwa sisi tumebarikiwa maarifa, busara na ustaarabu na tumedhamiria kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama na serikali kuhakikisha tunavuka salama. Tunafahamu kuwa kuna matishio yanayoendelea lakini hatuna wasiwasi ma Vyombo vyetu vya ulinzi na usalama na tumemsikia pia Dkt. Samia akituhakikishia usalama.” amesisitiza Kiliba.
Akieleza kuwa wapo timamu na jasiri kuelekea Oktoba 29, 2025, Kiliba amesema wataitumia siku hiyo kurusha Makombora matatu ya kura kwa Diwani, Mbunge na Mgombea Urais wanayeona kuwa anawafaa ambaye ni Mgombea Urais Dkt. Samia Suluhu Hassan anayetokana na Chama Cha Mapinduzi (CCM), akisema makombora hayo yatakuwa jibu sahihi na muafaka litakalowaangamiza wale wote wanaoenda kinyume na ratiba za nchi na wenye kuhamasisha uvunjifu wa amani.





