Na Kija Elias, Kilimanjaro
UGONJWA wa Kifua Kikuu (TB) unatajwa kuwa ni kati ya magonjwa matatu yanayotokea sana kwa watu maskini duniani, huku magonjwa mengine yakiwa ni Malaria na Ukimwi.
Magonjwa haya matatu husababisha vifo asilimia 10 ya idadi ya watu wote duniani kwa ujumla, ambapo inakisiwa ugonjwa wa Kifua Kikuu huathiri asilimia 98 ya watu katika nchi zinazoendelea, Ukimwi asilimia 95 na Malaria asilimia 90.
Ugonjwa wa Kifua Kikuu husababishwa na Bakteria wanaojulikana kama Mycobacteria tuberculosis, licha ya kwamba kuna aina nyingi za jamii ya Mycobacterium kama Mycobacteria leprae ambaye (husababisha Kifua Kikuu), Mycobacteria leprae husababisha ugonjwa wa ukoma, Mycobacteria bovis huathiri ng’ombe na binadamu.
Ugonjwa wa kifua kikuu unaweza kuathiri mapafu, mishipa ya fahamu mishipa, mfumo wa mzunguko wa damu ngozi, na viunganishi vya mifupa
Vihatarishi vya ugonjwa wa Kifua Kikuu; ni kama kuzeeka, unywaji wa pombe kupindukia, kuishi sehemu zilizo na mrundikano wa watu kama mabweni, kambi za jeshi huku magonjwa mengine yanayoathiri kinga ya mwili ni kama kisukari.
Kukosekana kwa elimu ya wataalam wa afya waliobobea katika kuwahudumia wagonjwa kila siku, imewafanya baadhi ya Wananchi kwenda kwa Waganga wa kienyeji kupata tiba za ugonjwa wa Kifua Kikuu wakidhani kuwa wamerogwa.
Mkurugenzi wa Hospitali Maalumu ya Taifa ya Magonjwa Ambukizi Kibong’oto Dkt. Leonard Subi, amesema hayo wakati akizungumza kwenye ufunguzi wa zoezi la upimaji wa ugonjwa wa Kifua Kikuu, Virusi vya Ukimwi, shinikizo la damu, uelimishaji, ushauri na uchunguzi wa afya kwa wananchi wa Wilaya ya Siha.
Amesema kukosekana kwa elimu ya kutosha juu ya ugonjwa wa Kifua Kikuu umesababisha baadhi ya wananchi kukimbilia kwa waganga wa kienyeji wakidhani wamerogwa kabla hawajagundua kama wanaumwa Kifua Kikuu.
“Licha ya serikali kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kwenda kwenye vituo vya afya na hospitali kupima afya zao, pindi wanapoona dalili za Kifua Kikuu wako baadhi ya Wananchi huenda kwa waganga wa kienyeji kupata tiba hiyo, ndiyo maana Kibong’oto tumeamua kuitumia fursa hii kutoka ofisini na kuja vijijini kwa ajili ya kutoa elimu hii,” amesema Dkt. Subi.
Amesema takwimu ziaonyesha kuwa watu zaidi ya milioni 10.4 wanaugua Kifua Kikuu kila mwaka na kati yao watu milioni 1.6 wanafariki dunia kutokana na ugonjwa wa Kifua Kikuu huku nchi ya Tanzania ikitajwa kuwa ni miongoni mwa nchi duniani yenye maambukizi ya Kifua Kikuu ambayo yako juu.
“Pamoja na jitihada za ugonjwa wa Kifua Kikuu kupungua, bado tuna wagonjwa wa TB ambao wako kwenye jamii yetu na wale tunaowagundua ni asilimia 65 tu, huku asilimia 35 wako kwenye jamii na hawa ndiyo tunawatafuta ili waweze kupatikana na kuwaweka kwenye matibabu,” amesema Dkt. Subi.
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Siha Dkt. Paschal Mbota amesema Wilaya ya Siha ina vituo vya kutolea huduma za afya 27 na kati ya hivyo vituo 12 vinauwezo wa kupima ugonjwa wa Kifua Kikuu.
“Tunavyo vituo vingine 15 ambavyo vinaweza kuchukua sampuli na kuleta kwenye maeneo ambayo yanaweza kupima TB,” amesema Dkt. Mbota.
Dkt. Mbota amesema kadri wanavyofanya zoezi la upimaji wa Kifua Kikuu wamekuwa wakiwaibua wagonjwa wengi na kuwapatia matibabu jambo ambalo limesaidia kupunguza kasi ya kuenea kwa ugonjwa huo.
Amesema mwaka 2020 waliwaibua wagonjwa wa Kifua Kikuu 648 na kuwapa matibabu, mwaka 2021 waliwapata wagonjwa 635 na mwaka 2022 waliwapata wagonjwa 628 huku mwaka 2023 wamewaibua wagonjwa 560.
“Kadri tunavyofanya zoezi la upimaji kama hili tumekuwa tukiwaibua wagonjwa na kuwapatia matibabu jambo ambalo limesaidia kupunguza kasi ya kuenea kwa ugonjwa huo,” amesema.
Katibu wa CCM Wilaya ya Siha, Ally Kidunda, ametoa maelekezo kwa viongozi wake wote wa chama ngazi ya vijiji na kata kuhakikisha kwamba wanajitokeza kupima afya zao ili kujua namna ambavyo wanaweza kuishi.
Naye Diwani wa Kata ya Sanya Juu, Juma Jani, amewasihi wananchi wa kata hiyo kujitokeza kwa wingi kupima afya zao na kuachana na tabia ya kutumia dawa pasipo kupima afya.
“Nakushukuru sana Mkurugenzi wa Hospitali ya Kibong’oto Dkt. Leonard Subi kwa kuamua kutoka ofisini na kuja maeneo ya kijijini kutoa elimu upimaji wa Kifua Kikuu, Virusi vya Ukimwi, na shinikizo la damu, jambo hili litasaidia sana wananchi kutambua afya zao,” amesema Jani.
Aidha, amesema Serikali ya Awamu ya Sita imejipambanua kwa mambo manne muhimu ambayo ni kushughulika na afya za wananchi, elimu, maji na miundombinu ambapo kwa wilaya ya Siha itumepokea fedha nyingi hususani katika sekta ya afya.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Siha Dkt. Christopher Timbuka, Katibu Tawala wa Wilaya ya Siha Jane Chalamila wakati wa ufunguzi wa zoezi la upimaji wa ugonjwa wa Kifua Kikuu, Virusi vya Ukimwi, shinikizo la damu, amesema mazoezi kaha haya huwa yanafanyika kila mwaka wilayani humo, ambapo yalianza toka mwaka 2017 na takribani Wananchi zaidi ya elfu 10 walishafikiwa na huduma hiyo.
“Kwa kutambua umuhimu wa kulinda afya ya wananchi tumeona ni vyema kufanya uchunguzi huu ili kulinda usalama wa afya za wananchi wote na kuwapatia ushauri na matibabu sahihi kwa wakati.”
Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya wananchi wa Wilaya ya Siha waliojitokeza kupima afya afya ya ugonjwa wa Kifua Kikuu, Ukimwi na shinikizo la damu, wamesema ukosefu wa elimu juu ya magonjwa hao watu wengu hususani maeneo ya vijiji hukimbilia kwa tiba za asili wakidhani kuwa huko wanaweza wakapona zaidi.
Mkazi wa Kitongoji cha Orengetwa, Kijiji cha Sanya Juu, Faustine Ngowi, amesema kwa maeneo ya kijiji hakuna uhamasishaji wa wananchi kujitokeza kupima afya zao, hali ambayo imesababisha wengi wao kwenda kwa waganga wa kienyeji kupata tiba huko za asili.
“Mimi mweyewe ni mgonjwa wa TB niliwahi kwenda kwa mganga wa kienyeji kutibiwa, baada ya kuwa ninakohoa mfululizo, huku nyakati za usiku nikitokwa na jasho jingi sana, nilipofika huko niliambiwa nimerogwa na kupatiwa dawa ambazo niliendelea kuzitumia bila mafanikio ndipo nilipopelekwa hospitali ya Kibong’oto na kugundulika kuwa nina Kifua Kikuu.
“Ninaomba zoezi hili liwe endelevu hususani katika maeneo ya vijijini hadi kwenye ngazi ya kaya kwani wako wagonjwa wa Kifua Kikuu wengi sana katika maeneo haya, katika eneo langi mimi ninapoishi kuna mgonjwa yuko kitandani kwa zaidi ya miaka minne hawezi kutoka nje yeye ni kukohoa tu lakini bado anaendelea kutumia dawa za miti shamba,” amesema.
Fraten Lyimo, mkazi wa kata ya Sanya Juu, amesema elimu iliyotolewa na Mkurugenzi wa Kibong’oto kuhusiana na ugonjwa wa kifua kikuu imesaidia sana, hata mimi baada ya elimu hii kutolewa inenisaidia kutambua dalili za ugonjwa wa Kifua Kikuu kwani nilikuwa sizifahamu.
“Nawashukuru sana madaktari kwa kufika katika kijiji chetu na kutoa elimu ya kifua kikuu, niwaombe wazidi kutembelea watu huku vijijini wako wengi mno wanaougua ugonjwa huu,” amesema.
Naye mkazi mwingine wa Sanya Juu, Jumanne Mvungi, ameomba elimu hiyo iendelee kutolewa mara kwa mara ili kuwaelimisha Wananchi juu ya maradhi ya kuambukiza, kwani watu wengi sana hawana elimu hiyo na pindi mtu anapozindiwa huanzishiwa dawa za kienyeji pasipo kupima afya.