Na Mwandishi Wetu
BONDIA wa Tanzania, Twaha Kiduku, ameshindwa kutamba nchini Ujerumani baada ya kupigwa kwa pointi dhidi na Juergen Doberstein katika pambano la raundi 12 la kuwania mkanda wa Dunia wa GBC Super Middleweight lililofanyika usiku wa kuamkia jana.
Kwa mujibu wa matokeo, jaji namba moja alitoa pointi 107-120, jaji namba mbili 107-120 na jaji namba tatu alitoa alama 108-199 na hivyo kuwa ni ‘anonymous decision’.
Hili lilikuwa ni pambano la kwanza kwa Kiduku kutoka nje ya Tanzania tangu alipofanya hivyo Mei, 2021 ambapo pia alipoteza kwa pointi dhidi ya Mrusi, Bek Nurmaganbet katika pambano ambalo lilifanyika Urusi.
Kwa ujumla hili ni pambano la 9 kwa Kiduku kupigana nje ya nchi, kati ya hayo 8 amepoteza huku akiwa na rekodi ya kushinda pambano moja dhidi ya Mzambia, Mbiya Kanku, mwaka 2016 na pambano hilo lilifanyika jijini Lusaka, Zambia.
Kiduku alikuwa na muendelezo wa ushindi katika mapambano yake mawili ambayo yote yalifanyika Tanzania ambapo mara ya mwisho alimpiga Muhindi, Harpreet Singh pambano ambalo lilifanyika Aprili 11, mwaka huu mkoani Morogoro.
Pia Kiduku alikuwa na kumbukumbu ya ushindi dhidi ya Mohamed Sebyala raia wa Uganda pambano ambalo lilifanyika Desemba 26, katika Ukumbi wa Ubungo Plaza, Dar es Salaam.
Mara ya mwisho Kiduku kupanda ulingoni kuwania mkanda ilikuwa ni Julai 29, 2023 ambapo alipoteza mbele ya Asemahle Wellem wa Afrika Kusini kwenye kuwania mkanda wa WBF Afrika.
Katika pambano lililofanyika Ujerumani, mpinzani wa Kiduku, ambaye anaitwa Doberstein ana rekodi ya kupanda ulingoni mara 38 ambapo alishinda 32, vipigo 5 na sare 1.