Na Mwandishi Wetu,
Mbinga
NAIBU Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis amewataka wachimbaji wa makaa ya mawe kuzingatia sheria kwa kufukia mashimo baada ya shughuli hiyo.
Ametoa kauli hiyo alipofanya kikao na uongozi wa Wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma wakati wa ziara ya kufuatilia utekelezaji wa Mradi wa Kuhifadhi Ardhi katika Bonde la Ziwa Nyasa unaoratibiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais.
Kutokana na changamoto hiyo, Khamis aliwataka viongozi kusimamia maelekezo yaliyotolewa na Serikali kuhakikisha wamiliki wa migodi hiyo pamoja na kuwa wanawekeza lakini wanapaswa kujali mazingira.
Pia, aliwataka wenye magari yanayobeba makaa ya mawe kuyafunika ili kuepusha vumbi linaloweza kusambaa na kusababisha madhara kiafya na mazingira kwa ujumla.
Alisema kuwa, ni kweli Serikali inawathamini wawekezaji mbalimbali wakiwemo wa sekta ya madini lakini wanapaswa kufuata sheria ili kunusuru mazingira kwa maendeleo endelevu ya nchi.
Awali, Mkuu wa Wilaya ya Mbinga, Aziza Mangosongo, alisema bado kuna changamoto ya wananchi kufanya shughuli za kibinadamu kando ya mito na kusababisha uharibifu wa mazingira.
Pia, alisema baadhi ya wenye migodi hukata miti kwa matumizi yao wakidai kuwa leseni ya uchimbaji inawapa kibali cha kutumia kila kitu wanachokikuta katika eneo walilopewa kufanya uwekezaji huo, hali inasavavisha uharibifu wa mazingira.