Katambi: Dkt. Samia amedhamiria kuboresha sekta ya viwanda na biashara kuimarisha uchumi wa Taifa

Salha Mohamed

NAIBU Waziri wa Viwanda na Biashara, Patrobasi Katambi, amesema azma ya serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuboresha sekta ya viwanda na biashara ni njia ya kuimarisha uchumi wa taifa na kutoa ajira kwa wananchi, hususani vijana. 

Katambi ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam wakati alipotembelea Shirika la Taifa la Maendeleo(NDC) na kuzungumza na viongozi wa shirika hilo.

Amesema kuna haja ya Shirika hilo na sekta binafsi, kuona umuhimu wa ushirikiano wa karibu kati ya serikali na sekta binafsi (PPP) ili kufikia malengo ya maendeleo endelevu.

Katambi amesisitiza kwa kipindi cha pili cha awamu ya Rais Samia, serikali imejidhatiti kuendeleza sekta ya viwanda, kutoa fursa za ajira na kuongeza pato la taifa. 

Ameyataja viwanda vidogo na vya kati kuwa na mchango mkubwa katika kupunguza tatizo la ajira, hasa kwa vijana, na kuongeza fursa za biashara kwa Watanzania.

“Kwa niaba ya Rais Samia Suluhu Hassan, serikali inajitahidi kuweka mazingira bora ya biashara kwa watu wa sekta binafsi na vijana ili wajiunge katika shughuli za viwanda. Uwekezaji katika viwanda vidogo na vya kati utazalisha ajira na kutuwezesha kukuza uchumi wetu,” amesema Katambi.

Ushirikiano wa Serikali na Sekta Binafsi

Katambi amefafanua ushirikiano kati ya serikali na sekta binafsi ni muhimu kwa kufanikisha miradi ya maendeleo na kuongeza ufanisi wa viwanda. 

Amesema serikali inatambua umuhimu wa kuwa na sera nzuri, ambazo zitawezesha wawekezaji kuwekeza kwa wingi, huku sekta binafsi ikiendelea kuleta mapinduzi katika viwanda vya ndani.

“Sekta binafsi ina mchango mkubwa katika maendeleo ya viwanda, na serikali itahakikisha inatoa ushirikiano wa kutosha. Kazi yetu ni kuhakikisha kwamba sera na sheria zinalenga kuhamasisha sekta binafsi, na kwamba tunapunguza vikwazo vinavyoweza kuzuia maendeleo ya biashara,” ameongeza.

Malengo ya serikali ya kuimarisha uchumi wa viwanda

Katambi ametaja lengo kuu la serikali ni kuimarisha uchumi wa viwanda ili kutoa ajira kwa Watanzania na kuongeza bidhaa zinazozalishwa ndani ya nchi. 

“Tanzania inahitaji kuongeza uwezo wa viwanda vyake, ili kushindana na mataifa mengine duniani, na kutoa nafasi kubwa ya ajira kwa vijana, vijana wa makamu.

“Hatuwezi kuwa na maendeleo ya kweli bila kuwa na uchumi imara. Uchumi wa viwanda ni muhimu kwa ustawi wa taifa letu. Serikali yetu iko tayari kushirikiana na sekta binafsi kwa pamoja ili kuboresha hali ya uchumi wa viwanda, na mwisho wa siku wananchi wetu wawe na maisha bora,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *