Kanisa Katoliki halina ugomvi na serikali – Askofu Ruwa’ichi


• Akanusha waraka wa semina ya walei Oktoba 29, 2025

Ataka wamumini wawe makini kubaini vyanzo vya taarifa
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
ASKOFU Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Jude Thaddaeus Ruwa’ichi, amesema Kanisa Katoliki halina ugomvi na serikali na kuwataka wanaohangaika kudhani kwamba lina mpango wa kushikana mieleka na serikali watambue hivyo.
Askofu Mkuu Ruwa’ichi amesema hayo wakati akihitimisha adhimisho la Misa Takatifu ya Jubilei ya mapadre wa jimbo hilo, iliyofanyika katika Parokia Ya Bikira Maria wa Fatima, Msimbazi jijini Dar es Salaam.
“Kwa hiyo wale wanaohaingaika wakidhani kwamba Kanisa Katoliki linataka kushindana, kulumbana au kushikana mieleka na serikali watambue kwamba sisi hatuna mpango huo. Kwa hiyo tamko hili langu liwasaidie muwe na uelewa sahihi na mfuate msimamo sahihi,” amesema Askofu Mkuu Ruwa’ichi.
]

Aidha Askofu Mkuu Ruwa’ichi amekanusha waraka uliosambazwa mitandaoni ukieleza kwamba Oktoba 29, Jimbo Kuu la Dar es Salaam limeandaa Semina ya Walei itakatofanyika katika Parokia ya Kristo Mfalme, Tabata kuwa ni taarifa za kughushi hazitoki katika ofisi yake.

“Ninaomba kutamka pia jambo lifuatalo, wale mnaotumia vilonga longa, wale mnaopita pita kwenye mitandao, mtafahamu kwamba kuna jambo ambalo kwa siku hivi karibuni limekuwa likisambaa katika mitandao, ni tangazo lililotolewa kuhusu semina ya walei. Naomba nitamke awali ya yote kwamba tangazo hilo halikutolewa na ofisi yangu,” alisema na kuongeza kwamba.
“Kwa hiyo siyo tangazo linalobeb sahihi yangu au lililotangazwa kupitia kwa chancellor au Katibu Mkuu, hilo liwafanye mtambue kwamba siyo tangazo rasmi.”
Amefafanua zaidi kwamba semina hiyo iliyoelezwa katika tangazo hilo feki kwa mujibu wa kalenda ya Jimbo, imepangwa kufanyika Novemba 29, mwaka huu na siyo Oktoba kama ilivyoelezwa katika tangazo hilo.


Amewaasa waumini kuwa makini wanapopata taarifa za mitandaoni kuzichunguza na kwa umakini zaidi, “Pia mnapoona matangazo yametolewa kwenye vyombo vya habari yachunguzeni vizuri kabla hamjaanza kuhaha maana yake siku hizi kumekuwa na kuhaha kwingi, na huko ni kutokana na kutokuwa makini, kutokana na kutochambua na kubainisha uhalisia wa jambo linalotangazwa”.

Hivi karibuni kumekuwa na waraka uliokuwa ukisambazwa kwenye mitandao ya kijamii ukieleza kwamba waumini wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam watakuwa na semina itakayofanyika Oktoba 29, 2025 ambayo siku hiyo imepangwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kwa ajili ya kupiga kura kuwachangua Rais, wabunge na madiwani.

Tangazo hilo lilizua taharuki miongoni mwa waumini wa kanisa hilo na wanachi kwa ujumla wakishindwa kuelewa ni kipi hasa kinachoendelea.

“Katika hili Baba Askofu Mkuu ametuweka huru, tulikuwa na utata mwingine ingawa kweli tangazo jenyewe kwa kuliangalia tu lilikuwa na viashiria vyote vya kuwa feki,” amesema James Kweka, muumini wa Parokia ya Mwenye Kheri Isdori Bakanja Boko.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *