
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salam
BENKI ya Biashara Tanzania (TCB) imezindua kampeni mpya ya kitaifa iitwayo “Toboa Kidijitali,” yenye lengo la kuhamasisha matumizi ya mifumo ya kisasa ya kufanya miamala ya kifedha na kuongeza ujumuishi wa kifedha nchini.
Lengo pia ni kurudisha sehemu ya faida katika jamii na itadumu kwa kipindi cha miezi minne huku zawadi za Sh. milioni 200 zikitarajiwa kutolewa zikiwamo gari aina ya Mazda, simu, bajaji na pikipiki.

Uzinduzi wa kampeni hiyo, umefanyika jana Aprili 25, 2025 jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Wateja Binafsi na Wafanyabiashara Wadogo na wa Kati, Lilian Mtali, kwa niaba ya Ofisa Mtendaji Mkuu wa TCB, Adam Mihayo. a
Mtali mesema benki imewekeza zaidi ya Sh. milioni 200 katika kampeni hiyo kama sehemu ya kurudisha kwa jamii na pia kukuza matumizi ya huduma za kifedha kwanjia ya kidijiti.
“Zawadi zitakazokuwa zinatolewa Kwa wateja kupitia kampeni hii ni pamoja na gari aina ya Mazda, bajaji, pikipiki, simu aina ya Iphone 16 Pro Max,”amesema Mtali.

Amesema kuwa TCB inaendelea kuboresha huduma kama Popote Mobile App, Popote Visa Card na mfumo wa Lipa Popote, ili kuwawezesha wateja kufanya miamala bila usumbufu na kwa usalama.
Kwa upande wake, Ofisa Mkuu wa Huduma za Kidijiti na Ubunifu wa TCB, Jesse Jackson, amesema kampeni ya Toboa Kidijitali inatoa fursa kwa wateja kujishindia zawadi mbalimbali zikiwamo gari aina ya Mazda, simu ya iPhone 16 Pro Max.

“Pamoja na zawadi za bodaboda na bajaji za kila mwezi zitazotolewa kwa kipindi cha miezi minne, lengo la kampeni hii pia ni kuchochea matumizi ya mifumo ya kifedha ya kidijiti na kuvutia makundi mbalimbali ya Watanzania, hasa walioko vijijini na maeneo ya pembezoni,”amesema Jackson.
Jackson ameongeza kuwa ingawa kuna ongezeko la miamala ya kidijitali kutoka milioni 14 mwaka 2020 hadi milioni 21 mwaka 2024, bado Watanzania wengi hutegemea fedha taslimu, hivyo, TCB imeona umuhimu wa kutoa elimu na motisha kwa umma kupitia kampeni hii, ikiwa ni hatua muhimu katika kuimarisha ujumuishi wa kifedha na kupunguza utegemezi wa cash economy.
