MKUU wa Wilaya ya Mbinga, Aziza Mangosongo amezindua kampeni maalumu ya utoaji elimu ya lishe na utekelezaji wa afua za lishe kwa kundi la vijana balehe wa shule zote za sekondari za Halmashauri ya Mji wa Mbinga.
Mangosongo amezindua kampeni hiyo yenye kauli mbiu ya “Lishe ni Mtaji wa Maendeleo na Chachu ya Ukuaji wa Uchumi” jana katika ukumbi wa shule ya sekondari Makita, iliyopo Halmashauri ya Mji wa Mbinga.
Wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo, Aziza amesema kwamba kutopata chakula chenye lishe bora hupelekea kupata udumavu na utapiamlo.
Ameongeza kuwa ni muhimu kwa kundi la vijana balehe kupata uelewa juu ya masuala yahusuyo lishe ili waweze kuepuka udumavu na utapiamlo.
Amewataka wataalamu wa masuala ya lishe kutoa elimu kwa shule zote juu ya kula chakula kilichokamilika na kujumuisha makundi yote ya chakula.