Kadi za CCM kutumika kwenye bima na ATM

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimesema kiko kwenye hatua za mwisho kuhakikisha kila mwanachama wa CCM aliyejiandikisha kwenye mfumo wa kupata kadi ya kielektroniki ya Chama hiko anapata lakini zaidi kuunganisha kadi hizo na huduma zingine muhimu za kijamii kama bima, kutoa fedha kwenye ATM na huduma zingine.

Hayo yameeleezwa na Katibu wa Oganaizesheni wa CCM Ndugu Issa Haji Gavu wakati akizungumza na wanachama wa CCM kwenye mkutano wa hadhara mkoani Iringa kwenye mwendelezo wa ziara ya Katibu Mkuu wa Chama hicho Ndugu Daniel Chongolo.

“Tunakwenda kutengeneza kadi, kabla ya kufika mwezi wa 8 mwaka huu hakuna Mtanzania ama mwana- CCM ambaye hatakuwa na kadi ya kielektroniki ya CCM. Kadi zinazokuja zinakuwezesha kupata huduma zingine na badala ya Mama kubeba pochi la vitambulisho kadi ya CCM inaweza kutoa huduma 11 za kijamii.” Alisema Gavu.

“Kadi ya CCM itakuwa na uwezo wa kusoma mfumo wa bima ya afya kwa maana ukiwa na kadi ya CCM ukipeleka kwenye mfumo wa bima ya afya haudaiwi kitambulisho kingine msingi uwe umesajiliwa katika mfumo wa bima. Kama wewe mwanachama wa NSSF na unalipia, ukiwa na kadi ya CCM huna haja ya kuwa na kadi nyingine. Ukiwa una hela zako benki na una kadi ya CCM huna haja ya kubeba kadi nyingine kupata huduma ya ATM, ile ya CCM itakuwa na uwezo wa kutoa fedha.”

Gavu amesema CCM imejipanga na kujizatiti na kuwataka wanachama wote kuwa na subira kwani licha ya kadi hizo za kielektroniki kuchelewa lakini zilikuwa zinaunganishwa na mifumo hiyo ya kijamii.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *