Wahitimu wa kidato cha sita mwaka 2023 wametakiwa kuripoti katika kambi za Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kuanzia Juni Mosi hadi Juni 11, 2023 kuanza mafunzo kwa mujibu wa sheria.
Mkuu wa Tawi la Utawala JKT Brigedia Jenerali Hassan Mabena amesema kwa mara ya kwanza tangu kurejeshwa mafunzo ya mujibu wa sheria mwaka 2013, vijana wote waliohitimu kidato cha sita mwaka huu watajiunga na mafunzo hayo.
Brigedia Jenerali Mabena ameongeza kuwa JKT inaendelea na mazungumzo na wizara na taasisi za kisekta ili kuongeza muda wa mafunzo ya mujibu wa sheria kutoka miezi mitatu ya sasa hadi angalau miezi sita.
Mafunzo ya JKT yanalenga kuwajengea vijana Uzalendo, Umoja wa Kitaifa, kuwafundisha stadi za kazi pamoja na kupandikizwa utayari wa kulijenga na kulitumikia Taifa lao.
Vijana waliotwa kujiunga na mafunzo hayo wanatakiwa kutembelea tovuti ya JKT ili kuona kambi walizopangiwa.