Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
RAIS mstaafu wa Awamu ya Nne, Dkt. Jakaya Kikwete amesema anataka kuiona Tanga School ikiwa miongoni mwa shule zinazoshika nafasi ya juu nchini.
Dkt. Kikwete alisema hayo jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa umoja wa wanafunzi waliosoma katika shule hiyo kuanzia miaka ya 1960 hadi sasa.
Amesema shule hiyo ambayo kwa sasa inajulikana kama Tanga Technical School, alisoma hapo kidato cha tano na sita pia imetoa watu mashuhuri mbalimbali nchini ikiwa ni pamoja na wenye taaluma mbalimbali.
“Tunataka kuiona Tanga School ikiingia shule bora zenye ufaulu wa juu, tutakaa na uongozi wa shule, tujue nini tuchangie ili lengo letu liweze kutimia,” alisema.
Aliongeza kuwa, haitapendeza shule hiyo ambayo ni ya sekondari ya kwanza nchini ipotee katika ramani ya elimu.
Dkt. Kikwete alisema kupitia umoja waliouanzisha, wataiwezesha shule hiyo iwe na maktaba mtandao, vifaa vya kufundishia, kujifunzia.
Awali Mwenyekiti wa umoja huo, Meja Jenerali Khamis Semfuko, alisema haikuwa kazi rahisi kukusanya dhamira za waliosoma miaka ya 1960, kuziunganisha na dhamira za vijana wa sasa waliopita shuleni hapo mpaka kufikia kuunda taasisi rasmi.
“Hatua hii inalenga kuboresha kiwango cha ufaulu Tanga School, ni chachu ya mageuzi makubwa ya maboresho ya miundombinu ya kuinua viwango vya taaluma kulingana na kasi ya teknolojia ya sasa,” alisema.
Kwa upande wake, Mkuu wa Shule, Mackmaster Mnondw, alisema atahakikisha shule hiyo inashika nafasi ya kumi bora kama umoja huo ulivyokusudia pamoja na ubora wa elimu.
Alisema shule hiyo yenye wanafunzi 1126, kati ya hao wanawake 194, wanaume 932, kidato cha tano wako 279 na wenye mahitaji maalum 163.
Mwaka 2022, ufaulu katika shule hiyo daraja la kwanza walikuwa 94, daraja la pili 42, daraja la tatu 27, la nne 28 na daraja O walikuwa 10.