Na Kija Elias, Kilimanjaro
SHERIA inamtambua mwenye ulemavu ni mtu mwenye udhaifu au upungufu wa viungo, fahamu au akili na ambaye uwezo wake wa utendaji kazi umepungua kutokana na vikwazo vya kimtazamo, kimazingira na kitaasisi.
Sheria hiyo imetoa wajibu kwa serikali kupitia wizara husika, Serikali za Mitaa, taasisi mbalimbali na jamii kwa ujumla kutambua na kuzilinda haki za watu wenye ulemavu ili kutokomeza vitendo vya ubaguzi na vya kikatili dhidi yao.
Aidha, Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Watu wenye Ulemavu unatambua kwamba, katika Tamko la Dunia la Haki za Binadamu na Mikataba ya Kimataifa ya Haki za Binadamu, Umoja wa Mataifa umetangaza na kukubali kwamba kila mmoja anastahili kupata haki zote na uhuru kama zinavyoelezwa humo, bila tofauti ya aina yoyote.
Vilevile mkataba huo unatambua hadhi ya asili, thamani, usawa na haki zisizopokonyeka za watu wote ambao ni wa jamii ya binadamu kama uhuru wa msingi, haki na amani duniani.
Hivyo basi, kila mtu ana wajibu wa kujali utu wa mtu, na unapojitolea kuihudumia jamii maana yake unafanya kazi ambazo zinaweza kufanywa na mtu, kundi la watu, au taasisi yoyote bila ya kutarajia kupata malipo kutoka katika jamii au wale wanaowafanyia kazi hiyo.
Kujitolea huko huwa sehemu ya kuongeza na kukuza maarifa pamoja na kuendeleza matendo mema katika kuudhihirisha utu na ubinadamu, mtu anayejitolea mara nyingi hupata matokeo mazuri kutoka katika jamii yake, hasa ile anayoihudumia.
Himatlal Devchand Shah (85), mkazi wa Moshi mkoani Kilimanjaro, amekuwa mstari wa mbele katika kujitolea kuwasaidia watu wenye ulemavu.
Devchand anasema kuwa, mlemavu ni mtu ambaye anaweza kuchangia kwa kiwango kikubwa kuliko hata watu wasio na ulemavu.
Anasema, wenye ulemavu ni sehemu ya jamii yetu, na wakiwezeshwa na kuthaminiwa wanaweza, kwani ni rasilimali watu ya taifa kama wale wasio na ulemavu.
Shah, ambaye ni Mkurugenzi wa kiwanda cha kutengeneza vifaa vya ngozi, katika maendeleo yake kimetoa ajira kwa watu takriban 302, wakiwemo 56 wenye ulemavu wa aina mbalimbali ukiwemo ulemavu wa kuoona, viziwi, pamoja na walemavu wa ngozi.
Shah anasema, kutokana na imani potofu, wenye ulemavu mara nyingi wamekuwa wakikumbana na vikwazo vingi kutoka katika ngazi za familia na jamii kwa ujumla katika kuendesha shughuli zao na kuendeleza maisha yao.
Anasema, baada ya kuanzisha kiwanda hicho mwaka 1976 ulikuwa wa mafanikio katika maisha yake kwani aliajiri mtu wa kwanza mwenye ulemavu katika kazi zake.
“Niliajiri mtu wa kwanza mwenye ulemavu, ambaye alifanya kazi kwa miaka 40, kwangu alikuwa mtu mwenye uwezo mkubwa na aliweza kuwafundisha na watu wengine wasio na ulemavu,” anasema Devchand.
Kitendo cha mwenye ulemavu huyo kuwa na uwezo mkubwa wa kufanya kazi, Devchand anasema, kiliamsha hisia zake kwa kuajiri watu wengi zaidi wenye ulemavu akiwamo Pastory Munishi ambaye ni mlemavu wa ngozi (Albino).
“Kutokana na changamoto ambazo walikuwa wakizipitia watu wenye ulemavu kutoka katika jamii iliyowazunguka, ilikuwa ikiwaona sio watu muhimu katika maisha ya kila siku, mimi niliwasaidia kwa kuwapatia ajira kwenye kiwanda changu,” anasema.
Akimzungumzia Munishi, Devchand anasema, kutokana na uaminifu wake na utendaji kazi wake mzuri alitafuta marafiki zake mbalimbali wa Alliance Club ambao walimchangia fedha ambazo ameamua kumjengea nyumba ya kuishi yenye vyumba vinne.
“Baada ya kuona utendaji kazi wake mzuri, baada ya kustaafu kazi kwangu Pastory, na kutokana na uaminifu aliouonesha katika utendaji kazi wake, niliona siyo vema kumwacha hivi hivi, nimeamua kufanya jambo la kiutu la kumjengea nyumba ya kuishi yeye na familia yake,” anasema.
Anaongeza: “Pamoja na ulemavu wake alikuwa ni mtu mwenye uwezo mkubwa, kwa kipindi kirefu nimefanya naye kazi imefikiwa wakati sasa wa kumpatia zawadi ya kumjengea nyumba yake ya kuishi, nimepata fedha kutoka kwa marafiki zangu na kuweza kumjengea nyumba yake ya kuishi.”
Anafafanua kuwa, hadi sasa watu saba wenye ulemavu ambao waliwahi kufanya kazi kwake na kustaafu ameshawajengea nyumba na wanaishi na familia zao.
Devchand anazidi kufafanua kwamba, katika kiwanda chake kilichopo mjini Moshi, aliajiri watu wenye ulemavu wapatao 56 kati ya watu 302 na kwamba wale walioonyesha kujituma zaidi na wao pia aliwajengea nyumba za kuishi katika maeneo tofauti kwa vipindi tofauti.
Devchand, ambaye aliwahi kuwa Gavana wa Alliance Club katika nchi za Uganda, Kenya, Ethiopia, Tanzania na Shelisheli, ambapo pia aliwahi kuwa Mkufunzi wa Chuo cha Alliance Club, anatoa wito kwa jamii kuhusu kuishi vizuri na watu wenye ulemavu.
“Kila mmoja ana uwezo wake, kama ni mlemavu wa kutoona lakini anasikia vizuri, yule ambaye hasikii vizuri lakini macho yake yanaona anafanya kazi, tusiwatenge wala kuwabagua watu hawa kutokana tu na ulemavu wao,” anasema Devchand.
Kwa upande, Pastory Pius Munishi, mkazi wa Katanini, Kata ya Karanga Manispaa ya Moshi, anasema alikuwa na changamoto katika suala la makazi kwa sasa anamshukuru Devchand kwa kujitolea kwake kuwahudumia wenye ulemavu kama yeye.
“Namshukuru sana Devchand na familia yake kwa kunijengea nyumba ya kuishi mimi na familia yagu, nilikuwa na changamoto ya maeneo ya kuishi, lakini sasa nitaishi hapa mimi na familia yangu,” anasema Munishi.
Munishi anasema, baada ya kustaafu alirudi kijijini na familia yake ya watoto saba na kuongeza kwamba Devchand amemsaidia kumsomeshea pia watoto wake.
“Nimefanya kazi kwa Shah (Devchand) kwa miaka 40 nikiwa kama mtunza stoo na kuwa mfanyakazi bora kwa vipindi vinne mfululizo, kwa uaminifu niliwahi pia kuwa kiongozi wa Chama cha Walemavu Tanzania ndiye mwanzilishi wa hiki chama,” anaongeza Munishi.
Daudi Mruma, fundi anayejenga nyumba ya Munishi, anasema: “Ni watu wachache wenye moyo kama wa Shah, amekuwa akisaidia watu wengi wenye uhitaji, wito wangu watu wanapofanya kazi kwa uaminifu, wajenge utaratibu wa kuwasaidia kuliko mtu anafanya kazi kwa mtu miaka yote halafu akitaka kuondoka anabebeshwa lawama kwamba amemuibia, jambo ambalo sio jema.”
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maridhiano Mkoa wa Kilimanjaro, Askofu Jones Mola na Mkuu wa Kanisa la Furaha Tanzania akinukuu katika Biblia, anasema: “Kitabu cha Mithali 22: 9 amesema…Mwenye jicho la ukarimu atabarikiwa kwa maana amempa mtu wa hali ya chini chakula chake.”
Anasisitiza: “Mtendee kila mtu kama vile ungependa kutendewa. Fikiria mtu kwanza, sio ulemavu wake. Usiepuke watu wenye ulemavu. Hivi ndivyo Himatlal Devchand Shah alivyowachukulia watu wenye ulemavu.”