Na Mwandishi Wetu, Arusha
MTU mmoja aliyefahamika kwa jina la Ally Athumani Dangote anayedaiwa kuwa jambazi sugu aliyeua watu zaidi ya saba mkoani Arusha amekufa akiwa katika harakati za kutaka kuwatoroka polisi.
Vyanzo vya habari kutoka kwa raia wema na Jeshi la Polisi vilisema Dangote alikamatwa jana saa 5 asubuhi maeneo ya Ngarenaro, Kata ya Unga LTD.
Dangote alikuwa katika nyumba aliyokuwa akijificha baada ya kufanya matukio ya uhalifu.
Habari zilisema, baada ya polisi kupewa taarifa ya kuwemo katika nyumba hiyo kutoka kwa raia wema, waliweka mtego na kufanikiwa kumkamata akiwa hai ndani ya nyumba hiyo.
Baada ya kukamatwa, polisi walimuhoji na kumtaka alitaje kundi alilokuwa akifanya nalo vitendo vya uhalifu wa kupora mali, vitu vyenye thamani na baada ya kupora, hufanya mauaji katika matukio mbalimbali jijini Arusha.
Inaelezwa kuwa, Dangote alimtaja mtu mmoja ambaye alitambulika kwa jina la Omari, Mkazi wa Kata ya Lemara, jijini Arusha.
Chanzo kinasema, Dangote aliomba kutoa ushirikiano wa kuwaonesha polisi anapoishi Omari, msafara wa kwenda Lemara ulianza lakini walipofika Kata ya Themi karibu na Kiwanda cha Bia TBL, Dangote aliruka gari akiwa na lengo la kuwakimbia polisi.
Wakati akifanya jaribio la kuwatoroka polisi, inadaiwa alianguka sehemu mbaya iliyosababisha apasuke kichwa, kutokwa damu nyingi na kufa hapo hapo kwani gari la polisi lilikuwa katika mwendo mkali.
Habari zilisema, baada ya Dangote kufariki dunia, polisi waliuchukua mwili wake na kwenda kuuhifadhi katika chumba cha kuhifadhi maiti Hospital ya Mkoa Mount Meru kwa hatua zaidi za kiuchunguzi.
Kamanda wa Polisi mkoani Arusha, Justin Masejo hakuweza kupatikana kueleza tukio hilo kwani simu yake ya kiganjani ilikuwa haipatikani mara zote.