Jafo akabidhi tuzo wafugaji wanawake Watanzania COP28

Na Robert Hokororo, Dubai

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dkt. Selemani Jafo, amekabidhi Tuzo ya ‘Wanawake katika Uongozi’ kwa Baraza la Wanawake Wafugaji (PWC) Tanzania baada ya kuibuka washindi wa kwanza kati ya washindani 500 kutoka nchi mbalimbali duniani.

Tuzo hiyo imetolewa na Taasisi ya Global Centre on Adaptation (GCA) jijini Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu ambako kunafanyika Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP28).

Akikabidhi tuzo hiyo kwa kiongozi wa Baraza hilo kutoka jamii ya Kimasai Bi. Maanda Ngoitiko, Dkt. Jafo aliwapongeza kwa kuipatia Tanzania sifa.

“PWC wameiheshimisha sana Tanzania na kuifanya isikike duniani na nina uhakika kabisa tuzo hii imetokana na juhudi binafsi za dada yangu Maanda za kuimarisha uwezo wa uongozi wa wanawake wafugaji kwa kuwajengea uwezo kiasi cha kufikia usawa katika kutoa maamuzi katika jamii zao,” alisema Waziri Jafo.

Akishukuru kwa tuzo hiyo, Bi. Maanda alisema kuwa Baraza hilo linawahudumia wanawake na wasichana kutoka jamii za Wamasai, Wasonjo, Waakie na Wabarbaig (Wamang’ati).

Aliongeza kuwa, PWC ni shirika lisilo la kiserikali linalofanya kazi kaskazini mwa Tanzania kufikia usawa wa kijinsia na maendeleo ya jamii kupitia uwezeshaji wa wanawake na wasichana wa Kimasai.

Wakati huo Tanzania inaendelea kushiriki katika Mkutano wa COP 28 sanjari na mikutano ya pembezoni (side events), mikutano ya uwili (bilateral meetings) na warsha ambapo watu zaidi ya 81,000 kutoka nchi zaidi 190 wanahudhuria.

Tanzania imeandaa banda la maonesho katika viwanja vya Dubai Expo City likisheheni wizara na taasisi mbalimbali ambapo Ofisi ya Makamu wa Rais inawakilishwa na Waziri Jafo, Katibu Mkuu Bi. Mary Maganga na wataalamu kutoka Ofisi hiyo.

Aidha, Mkutano huo unaochagizwa na kaulimbiu ya kitaifa ‘Kuimarisha Kilimo Himilivu na Uchumi wa Bluu katika Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi’, ulifunguliwa rasmi Novemba 30 na unatarajiwa kuhitimishwa Desemba 12, 2023.

Desemba 5, 2023, Waziri Jafo alishiriki Mkutano wa Uwili kati ya Serikali ya Tanzania na Mfuko wa Kimataifa wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi (Adaptation Fund), ambapo aliutaka ukamilishe mchakato wa kupata ithibati ya pili kwa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC).

Kikao hicho kilishirikisha Mkuu wa Sekretariati ya Mfuko huo, Mikko Ollikainen, pamoja na timu yake pembezoni mwa Mkutano wa 28 wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP 28) unaoendelea Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu.

Dkt. Jafo alisema, NEMC ambayo ndiye msimamizi wa fedha za mfuko huo nchini Tanzania ilipitiwa na mchakato wa ithibati kwa takriban miaka miwili sasa hivyo inapaswa ikamilishiwe mchakato huo.

Vilevile, Waziri Jafo aliisisitiza Sekretariati ya mfuko huo kuongeza kasi katika kupitia taarifa za mwaka za miradi inayoendelea kutekelezwa, kuzipitisha na kuruhusu fedha za mwaka unaofuata kutolewa.

Mkutano huo umeleta manufaa ya haraka ambapo Mfuko umeahidi kutendea kazi masuala hayo na baadhi ya hayo yameanza kushugulikiwa muda mchache baada ya mkutano.

Dkt. Jafo alisema, Serikali itaendeelea kuhakikisha taasisi zote zinazoomba usajili katika Mfuko huo zinafanikiwa kupata usajili ili kunufaika na faida zake.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *