Na Mwandishi Wetu, Dodoma
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, (Muungano na Mazingira), Dkt. Selemani Jafo, amesema wafugaji nchini hawana budi kuwa mabalozi wazuri na kuunga mkono juhudi za serikali za kuhifadhi mazingira kwa kufanya shughuli za ufugaji wenye tija kwa maendeleo endelevu.
Jafo ameyasema hayo jana wakati wa uzinduzi wa wiki ya Maonesho ya Ufugaji wenye Tija na Utunzaji wa Mazingira sanjari na kuzindua Chama cha Mazingira na Ufugaji Tija Tanzania (CHAMAUTA) katika viwanja vya Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete jijini Dodoma Oktoba 31, 2023
Amesema kuwa ufugaji endelevu usioathiri hifadhi ya mazingira utasaidia katika kuepusha migogoro baina ya wakulima na wafugaji nchini.
“Tuepuke migogoro baina ya wakulima na wafugaji ambayo tunashuhudia ikitokea katika baadhi ya mikoa nchini, husababisha kutoelewana kwa makundi hayo mawili hali inayoweza kusababisha uvunjifu wa amani na tuna wajibu wa kulinda amani,” amesisitiza.
Dkt. Jafo amewahimiza wafugaji ambao wamepata ufadhili kutumia fursa ya Mkutano wa 28 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Mabdiliko ya Tabianchi (COP 28) kushiriki kikamilifu.
Amesema kuwa mkutano huo unaotarajiwa kufanyika Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) Novemba 28 hadi Desemba 5, 2023 utakuwa ni adhimu ya kuitangaza nchi yetu namna Tanzania inavyofanya ufugaji rafiki wa mazingira.
Waziri Jafo ametoa wito kwa CHAMAUTA kulitumia Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kupata uelewa kuhusu kanuni na zinazosimamia mazingira ili kuepuka shughuli zinazoharibu mazingira.
Amewataka wafugaji nchini kuunga mkono juhudi za Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan ambaye anaendelea kuiletea nchi maendeleo ikiwamo kuendeleza sekta ya maji.
Amesema kupitia miradi mbalimbali serikali imekuwa ikichimba malambo kwaajili ya kunyweshea mifugo hususan katika maeneo yenye ukame hatua inayosaidia.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Remidius Mwema, ameyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, aliipongeza Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kusimamia utekelezaji wa uhifadhi wa vyanzo vya maji.
Amesema kuwa mikakati ya kuhifadhi vyanzo vya maji katika eneo la Makutupora inaendelea na kuwa tayari chanzo hicho kimeanza kutoa asilimia 61 ya mahitaji ya maji kwa mkoa.
Aidha, Mwema amesema kuwa serikali ya mkoa inaendelea na kampeni ya kukijanisha Dodoma ambapo inaendelea kuandaa vitalu vya miche ili kukabiliana na upungufu wa miche.
Naye Mwenyekiti wa CHAMAUTA amesema chama hicho kimemtunuku Waziri Jafo kadi ya uanachama wake na mlezi kumuomba kuwa mlezi wake kutokana mchango wake na ofisi kwa ujumla.