INEC yahadharisha wanawake kuepuka vurugu wakati wa kampeni za uchaguzi

Na Salha Mohamed, Dar es Salaam

TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi(INEC), imewataka wanawake katika kipindi cha kampeni za Uchaguzi Mkuu, 2025 kuhimizana kupitia majukwaa yao kuwa makini kuhakikisha hawawi chanzo cha kuvuruga amani na utulivu wa nchi.

Hayo yamebainishwa leo Julai 31, 2025, jijini Dar es Salaam na Makamu Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji (Mstaafu) Mbarouk Mbarouk kwa niaba ya Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji (Rufani), Jacobs Mwambegele, wakati wa Mkutano uliokutanisha INEC na wawakilishi wa wanawake kuhusu Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025.

Amesema katika kipindi cha kampeni, Vyama vya Siasa vitapata fursa ya kuwanadi wagombea na kueleza Sera na Ilani za Uchaguzi za Vyama vyao.

“Katika eneo hili, uzoefu inaonesha kuwa kipindi cha kampeni kuna kuwa na joto la kisiasa linalotokana na baadhi ya watu kukosoa uvumilivu wa kisiasa hali ambayo inaweza kuhatarisha amani na utulivu wa nchi,”anasema.

Jaji Mbarouk aliwasihi Wanawake hao kusoma Sheria,kanuni na maelekezo ya Uchaguzi ili ushiriki wao katika mchakato wa Uchaguzi uweze kufanyika kwa kuzingatia masharti na matakwa ya Sheria,kanuni na maelekezo husika.

Alisema Tume itaendelea kuwashirikisha kwa kadri itakavyowezekana na kusimamia uchaguzi huo kwa kuzingatia Katiba, Sheria na Kanuni na taratibu mbalimbali zinazosimamia uendeshaji wa uchaguzi.

“Lengo likiwa ni kuhakikisha Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 unakua huru na wa wazi, wa haki na wa kuaminika kwa kuweka mazingira sawa ya ushindani kwa wagombea wa vyama vyote vya siasa vitakavyoshiriki,”anasema.

Kwa upande wa washiriki wa mkutano huo, walipata elimu ya namna bora ya kutoa elimu ya mpiga kura kwa jamii kwa kufuata kanuni, Katiba, mionozo na taratibu zinazokubalika.

Mkurugenzi Mtendaji Taasisi ya Kitango iliyopo Temeke, Dar es Salaam, Batuli Kiwanda “Wengi wetu tupo hapa hatujawahi kutoa elimu kwahiyo kupitia mafunzo haya yatatupa uwezo ili tunapokwenda kwa jamii tuweze kutoa elimu iliyo sahihi,”alisema.

Anasema kupitia taasisi yao wamejikita kuwajengea uwezo wakina mama hivyo watawashawishi wanawake kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi mbalimbali za uongozi na kupiga kura.

“Tutawahimiza wasirudi nyuma kwasababu kuna baadhi ya mila na desturi, mfumo dume uliopo unawafanya wanawake wanashindwa kujitokeza kwa kukatazwa ama vinginevyo,”alisema.

Anatoa wito kwa wanaume kuwaruhusu wake zao kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika jamii zao na kupiga kura kuchagua viongozi ambao wanawafaa.

Aidha Mkurugenzi wa Shirika lisilo la kiserikali la WISE, Dkt. Astronaut Bagile, ameishukuru Tume kuona umuhimu wa wanawake katika kuelekea uchaguzi mkuu 2025 lengo likiwa kuhamasisha kundi ambalo wataliwakilisha kwenye jamii kujua umuhimu, faida za kupiga kura.

“Tunaishukuru Tume kuona umuhimu wa kundi hili ambalo tupo asilimia 51 nchini, kuhimiza wanawake wenzetu kujitokeza kuanzia kwenye kampeni kusikiliza sera, kupiga kura na kushiriki mchakato wote.

“Pia kuhamasisha wanawake kumpa kura atakayewashawishi kumchagua, wanawake wawafikirie wanawake wenzao ili waweze kuwawakilisha kwenye meza ya maamuzi,”alisema.

Anasema wapo tayari kwa usghiriki katika uchaguzi Mkuu 2025 kwa kupigiwa kura na kupiga kura.

Mratibu wa kitaifa wa Taasisi ya Ulingo, Avemaria Semakafu anatoa wito kwa INEC kutengeneza kanuni ambayo itawezesha eneo maalum la watu wenye ulemavu kukaa lenye ulinzi wa ziada wakati wa kampeni.

Aidha kwa Mamlaka iliyopewa INEC chini ya masharti ya Ibara ya 41(4) ya Katiba ya Tanzania yam waka 1977, ikisomwa pamoja na Kifungu cha 49(1)(a) na 68(1) vya Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na. 1 ya mwaka 2024, ilitangaza ratiba ya Uchaguzi Mkuu wa Rais na wabunge katika Jamhuri ya Muungano na Madiwani kwa Tanzania Bara mwaka 2025.

Kwa mujibu wa raitba, Utoaji wa fomu utaanza Agosti 9,2025 hadi Agosti 27,2025 kwa wagombea wa kiti cha Rais na Makamu wa Rais na kuanzia Agosti 14,2025 hadi Agosti 27,2025 ni utoaji wa fomu za wagombea wa Ubunge na Udiwani na uteuzi utafanyika Agosti 27,2025.

Kampeni za uchaguzi zitaanza Agosti 28,2025 hadi Oktoba 28,2025 kwa Tanzania Bara na kuanzia Agosti 28,2025 hadi Oktoba 27,2025 kwa upande wa Tanzania Zanzibar.

Aidha jumla ya majimbo 272 yatatumika kwenye uchaguzi Mkuu 2025, ambapo Tanzania Bara yapo Majimbo 222 na Tanzania Zanzibar Majimbo 50 kukiwa na ongezeko la Majimbo 8 yaliyoanzishwa Tanzania Bara.

Jumla ya Kata 3,960 zitafanya uchaguzi wa Madiwani, kukiwa na ongezeko la Kata 5 zilizoongezeka baada ya Ofisi ya TRais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(Tamisemi) kuanzisha.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *