Ikikupendeza Rais Samia, kirejeshe Kikosi Kazi kilichokomesha mauaji ya albino 2015

Na Daniel Mbega, Kisarawe

KIFO cha kusikitisha cha mtoto Asimwe Novart (2), mkazi wa Kitongoji cha Mbale, Kijiji cha Bulamula, Kata ya Kamachumu, Wilaya ya Muleba mkoani Kagera, kimewaibua watu wengi wakiwemo wanaharakati wa kutetea haki za binadamu nchini.

Lakini pia yumo mwenyekiti mstaafu wa Chama cha Albino Tanzania (TAS), Ernest Kimaya, ambaye anapendekeza kwamba, jitihada zilizofanywa mwaka 2015 na Kikosi Kazi zirejeshwe kama na ikiwezekana kuwarejesha hata baadhi ya wajumbe waliokuwemo kwenye Kikosi Kazi hicho.

Anasema kwamba, hali ya usalama kwa watu wenye ualbino iliboreshwa zaidi mwaka 2015 hadi mwanzoni mwa 2016 ambapo hakukuripotiwa matukio makubwa ya ukatili dhidi yao.

“Kile Kikosi Kazi kingesaidia zaidi kwa sababu katika kipindi kile japo matukio yalitokea, lakini kwa kuwa operesheni ilikuwa ikiendelea, wahusika walikamatwa haraka na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria,” anakumbuka Kimaya, ambaye wakati huo ndiye alikuwa akiiongoza TAS.

Kikosi hicho, anasema, kiliundwa kufuatia agizo la Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete, baada ya kuwepo kwa mfululizo wa matukio ya kuwadhuru albino nchini.

“Tulichoshwa na matukio yale ambayo yalitufanya tuishi kwa hofu, wanachama wetu wakatutuhumu viongozi kwamba tulikuwa tukiyafumbia macho, sisi tukaituhumu Serikali kwamba ilikuwa inazembea hata kuwakamata watuhumiwa katika kesi za kuwadhuru albino, zikiwemo za mauaji.

“Mbaya zaidi ni kwamba, watu wenye ualbino walitishia kufanya maandamano nchini, hali ambayo ingeweza kuzusha taharuki, hivyo Serikali ikaamua kufanya jambo,” anasema.

Kimaya anasema, kulikuwa na matukio mfululizo ya mauaji yakiwemo ya Lugolola Bunzari (7) mkazi wa Kitongoji cha Kinondoni, Kata ya Kanoge, Tarafa ya Ulyankulu, Wilaya ya Kaliua, Mkoa wa Tabora lililotokea mwaka 2013; tukio la kumjeruhi Pendo Sengerema (15) mkazi wa Ugasa, Kata ya Usinge, Wilaya ya Kaliua mkoani Tabora lililotokea mwaka 2013; tukio la kumteka nyara mtoto Pendo Emmanuel Nundi (3), mkazi wa Kijiji cha Ndamhi wilayani Kwimba lililotokea Desemba 27, 2014; na tukio la kujaribu kumuua Muungu Msaga Gedi, mkazi wa Kitongoji cha Mkuyuni, Kijiji cha Buhekela, Kata ya Igoweko, Tarafa ya Simbo, Wilaya ya Igunga ambalo liliambatana pia na mauaji ya mumewe Mapambo Mashili aliyekuwa akipambana na wahusika wasimdhuru mkewe.

Anasema, ililazimu kuundwa kwa Kikosi Kazi ambacho majukumu yao yalikuwa kufanya upelelezi kwa kesi zote za nyuma ambazo zilikuwa hazijapata watuhumiwa pamoja na kuendelea kupambana na matukio mengine kama hayo.

“Kikosi Kazi kile kama kisingesimamisha operesheni zake, leo hii hata watuhumiwa katika kesi ambazo zinalegalega wangekuwa wamekamatwa na kufikishwa kwenye mikono ya sheria.

Lakini pia vitendo hivyo huenda visingekuwepo kwa sababu maofisa wa kikosi hicho, katika kipindi ambacho mimi nilikuwa mwenyekiti na kumshauri Rais Kikwete atusaidie, walikuwa na mpango kazi endelevu uliosaidia kuwapata watuhumiwa hata kati kesi za miaka ya nyuma. Naomba Mama Samia, Rais wetu mpendwa, akirejeshe kikosi hiki kutunusuru,” anasema.

Kimaya anakumbuka kwamba, mara baada ya kuteuliwa, Kikosi Kazi hicho kilikumbana na tukio linalofanana na la mtoto Asimwe, ambapo mnamo Jumapili usiku, Februari 15, 2015, mtoto mwenye ualbino Yohana Bahati (mwaka mmoja) aliyenyakuliwa kutoka mgongoni mwa mamaye huku mama huyo akinusurika kifo baada ya kukatwa mapanga kichwani na usoni wakati akipambana mwanawe asitwaliwe.

“Kikosi Kazi hicho kilitumia siku mbili tu kuupata mwili wa marehemu ukiwa umefukiwa katika shamba moja huko Shilabela – Mapinduzi jirani na Msitu wa Biharamulo,” anakumbuka Kimaya.

Mbali ya hivyo, kikosi hicho kilifanikiwa kuwakamata watuhumiwa wote watano waliohusika na kitendo cha kukatwa kiganjwa cha Baraka Cosmas Songoloka (4) wa Kipeta, Sumbawanga na kukipata kiganja chenyewe.

Aidha, kikosi hicho kilifanikiwa pia kukamata watuhumiwa wakiwa na mifupa ambayo ilithibitika kwamba ni ya Muungu Msaga Gedi, wakiwa katika harakati za kumuuzia mtu mmoja aliyekuwa akijiandaa kwenda kugombea ubunge mwaka huo.

Si hivyo tu, bali walifanikiwa kumnasa Masanja Mwinamila (44) wa Kitongoji cha Kona Nne, Kijiji cha Ugembe II, Kata ya Mwakashanhala, Tarafa ya Puge, wilayani Nzega mkoani Tabora, aliyekuwa anamuuza hai binti wa dada yake, Margreth Hamis (6), mwenye ualbino.

“Kikosi Kazi kile kilianzisha Operesheni ya Kukamata Waganga nchi nzima wanaopiga ramli chonganishi pamoja na wanaofanya kazi za uganga bila vibali, zoezi ambalo lilisababisha kwa kiasi kikubwa kupunguza kasi ya matukio hayo nchini,” anasema Kimaya.

Akizungumzia sababu sababu za kusitishwa kwa operesheni hizo, anasema kwamba, sababu kubwa ilikuwa wajumbe warejee kwenye vituo vyao vya kazi na wajiandikishe kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu.

“Lakini ghafla kimbunga cha uchaguzi kilichoanzia CCM kikaanza, na baada ya Edward Lowassa kuhamia upinzani, ikawa vigumu kukirejesha kikosi kwenye operesheni zake,” anasema.

Anaongeza kwamba, matokeo ya kutorejea kwa kikosi hicho, ndiyo yaliyosababisha kurejea kidogo kidogo kwa matukio hayo na sasa yanaonekana kushika kasi.

“Mwezi Oktoba, 2015, siku chache kabla ya uchaguzi mkuu, Mohammed Said (35), mkazi wa Mkuranga, alivamiwa na watu wasiojulikana na kushambuliwa kwa kumkata panga kichwani.

“Januari 3, 2017 majira ya saa 3:00 usiku katika Kitongoji cha Songambele, Kijiji cha Mumba, Kata ya Masoko katika Wilaya ya Mbeya Vijijini mkoani Mbeya, kundi la watu watano lilivamia na kuchimbua kaburi ulimozikwa mwili wa Sisala Simwali, aliyekuwa na ualbino, ambaye alifariki dunia Februari 28, 2008 baada ya kuugua na kuzikwa Februari 29, 2008 katika makaburi ya familia.

“Mnamo Oktoba 3, 2017, Nassoro Msingili (75), mkazi wa Kijiji cha Nyarutanga, Kata ya Kisaki, Wilaya ya Morogoro, alikatwa mkono na watu wasiojulikana.

“Jumatano, Novemba 2, 2022 majira ya saa 4:00 usiku, katika Kijiji na Kata ya Ngula wilayani Kwimba mkoani Mwanza, James Masholola (49), ambaye ni albino, aliuawa kwa kukatwa mapanga na wahusika wakakata mkono wake wa kulia na kuondoka nao. Lakini pia mwaka huo 2022 Getrude Dotto, mkazi wa Sengerema ambaye ana ualbino, aliuawa na watu wasiojulikana,” anasimulia Kimaya kwa kuweka sawa takwimu.

Kama alivyosema Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Khadija Taya ‘Keysha’, vitendo vya kuwadhuru albino vinatishia usalama wao kwa sababu kabla ya tukio la Asimwe, pia Mei 4, 2024 mtoto Julius Kazungu (10) ambaye ana ualbino alijeruhiwa na kitu chenye ncha kali kichwani na mikononi huko Katoro, Wilaya ya Geita, mkoani Geita.

Kwa mujibu wa jarida la Shirika lisilo la kiserikali linalohusika na utetezi na ustawi wa watu wenye ualbino nchini la Under The Same Sun matukio ya ukatili, ukatwaji au unyofolewaji wa viungo vya mwili au ufukuaji wa makaburi na mauaji ya kinyama dhidi ya watu wenye ualbino yalianza kuripotiwa na vyombo vya habari mwaka 2006 kwa kuhusishwa na imani za kishirikina.

Juhudi mbalimbali zilianza kuchukuliwa kwa kushirikiana na Serikali ambazo ni pamoja na kuanzishwa kwa kambi za watu wenye ualbino ikiwemo kambi ya Kabanga (Kigoma), Buhangija (Shinyanga), Mitindo (Mwanza), Pongwe (Tanga), Kitengule (Tabora) na Mugeza (Kagera).

Hata hivyo, baadhi ya watu wenye ualbino wakiwemo watoto waliokuwa katika kambi hizo wakati wa matukio hayo walianza kurejea makwao baada ya hali ya usalama kuonekana kuwa imeimarishwa.

Kwa mujibu wa Under The Same Sun kwa Tanzania na Afrika Mashariki mtu mmoja kati ya watu 1,400 ana ualbino.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *