Na Daniel Mbega, Dar es Salaam
JUMAPILI, Julai 7, 2024, Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ilitangaza nafasi mpya za ajira 9,483 katika Sekta ya Afya, ukiwa ni mwendelezo wa utekelezaji wa mkakati mahsusi wa Rais Samia katika kuiboresha Sekta ya Afya.
Tangazo hilo lililotolewa na Katibu wa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma kwa niaba ya Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka ya Serikali za Mitaa lilieleza kuwataka Watanzania wenye sifa na uwezo wa kujaza nafasi hizo 9,483 kwenye sekta hiyo katika kada takriban 38.
Miongoni mwa nafasi hizo ni daktari bingwa wa kinywa na meno daraja la II, madaktari wa upasuaji wa kinywa na meno daraja la II 111, madaktari bingwa wa watoto 4, madaktari bingwa wa magonjwa ya ndani 7, madaktari bingwa wa magonjwa ya akina mama 9, Madaktari wa upasuaji 5, daktari bingwa wa masikio, pua na koo 1, madaktari (Medical officer II) 726 na wauguzi 2,282.
Wengine ni mafundi sanifu vifaa tiba 86, matabibu 1,239, tabibu wasaidizi 636, maofisa walezi wa watoto 2, maofisa wauguzi 301, maofisa wauguzi wasaidizi 1,016, wafamasia 128, maofisa teknolojia wa maabara 57, mafiziotherapia 83, matabibu wa kinywa na meno 210, makatibu wa afya 41, maofisa afya mazingira 124 na maofisa afya mazingira wasaidizi 276.
Kutolewa kwa tangazo hilo kunafuatia pia taarifa iliyotolewa na Serikali kupitia Ofisi ya Rais Tamisemi kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwamba inakusudia kuajiri watumishi wapya 46,000 katika kada ya Elimu, Afya na kada nyingine kabla ya mwezi Juni baada ya Rais kutoa kibali cha ajira hizo Aprili 16, 2024.
Azma ya Rais Samia ya kuhakikisha inaongeza watumishi katika sekta muhimu imejionyesha, siyo sasa, bali tangu ameingia madarakani, na kwa hatua hii inathibitisha wazi jinsi alivyodhamiria kuboresha sekta hizi muhimu.
Jumamosi, Januari 6, 2024, wakati Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohamed Mchengerwa, wakati alipofunga kikao kazi cha makatibu tawala wasaidizi elimu na maofisa elimu wa halmashauri kilichofanyika mkoani Morogoro, alisema kwamba Serikali ilikuwa imepanga kutoa ajira mpya za walimu na maofisa afya 23,000 katika kipindi cha Januari hadi Februari, 2024, wengi hawakuamini.
Lakini akasema kwamba, baada ya ajira 13,000 zilizotolewa kwa walimu walioajiriwa na kupangiwa maeneo, Serikali ilipanga kuongeza nyingine mpya. Hii ilitokana na kuongezwa shule mpya 302 na madarasa 1,668 ambayo yalipangwa kupokea wanafunzi Januari 8, 2024 wakati shule zilipofunguliwa.
Na ikumbukwe tu kwamba, hiyo yote ni maandalizi ya miradi ambayo imekuwa ikifanywa na Serikali, ikiwamo ya kuongeza shule na madarasa kupitia mradi wa kuimarisha na kuboresha elimu ya awali na msingi (Boost), ambapo Serikali imepanga kutumia Shs. 1.15 trilioni ili kuboresha miundombinu ya elimu ya awali na msingi katika kipindi cha miaka mitano.
Mradi huu ambao umebuniwa na Rais Samia unakusudia kujenga madarasa 12,000 na vyoo 6,000 ifikapo mwaka 2025.
Lakini kuna Shs. 1.2 trilioni ambazo tayari zimetumika kwa shule za sekondari, zikiwamo mpya 1,000 za Kata na 26 za wasichana za mikoa zilizojengwa na Januari 2024 zimepokea wanafunzi.
Na katika kuhakikisha mtoto wa Tanzania anapata elimu bure, Serikali imekuwa ikitumia takribani Shs. 33.3 bilioni kila mwezi katika ufadhili wa elimu bila ada, huku ikiboresha mazingira ya walimu kwa kuwapandisha madaraja 227,263 na kuwalipa wanaodai malimbikizo.
Wahudumu afya ngazi ya jamii
Serikali ya Rais Samia haijaangalia watendaji wa sekta ya afya ngazi ya juu pekee, bali wahudumu wa afya ngazi ya jamii ambapo mnamo Jumamosi, Aprili 6, 2024 ilitangaza nafasi za kazi kwa wahudumu wa afya ngazi ya jamii 8,900 watakaokwenda kutekeleza afua jumuishi za afya, lishe na ustawi wa jamii katika ngazi ya vitongoji na vijiji.
Taarifa ya Serikali iliyotolewa na Wizara ya Afya kwa ushirikiano na Ofisi ya Rais Tamisemi ilisema kwamba, hivi sasa Serikali inatekeleza mpango jumuishi wa wahudumu wa afya wa ngazi ya jamii nchini, ambapo kupitia mpango huo, Serikali imeweka utaratibu wa kuwapata wahudumu wenye sifa zilizowekwa kutoa mafunzo na kuwatumia wahudumu wa afya ngazi ya jamii katika utekelezaji wa afua hizo. Mpango huo unahitaji wahudumu wawili mwanamke na mwanaume.
Awamu ya kwanza ya mpango huo itaanza kwenye mikoa 10 na halmashauri mbili kwa kila mkoa na itakayonufaika ni Geita wahudumu 920, Kagera (878), Kigoma (1,094), Lindi (1,724), Mbeya (836), Njombe (746), Pwani (480), Songwe (774), Tabora (966) na Tanga (482).
Taarifa zilizopo zinasema, utekelezaji wa mpango huo utaendelea kwa awamu katika mikoa na halmashauri zote za Tanzania Bara, wananchi wenye sifa stahiki ndani ya mikoa 10 wanahimizwa kuomba nafasi za wahudumu wa afya ngazi ya jamii katika mitaa na vitongoji vyote ndani ya halmashauri zao.
Mnamo Januari 31, 2024, Makamu wa Rais, Dkt. Philip Mpango alisema Serikali imetenga Shs. 899.473 bilioni kwa ajili ya kutekeleza mpango wa kuajiri na kuwajengea uwezo jumla ya wahudumu wa afya ngazi ya jamii wapatao 137,294 katika mikoa yote 26 ya Tanzania Bara katika maeneo yao vijiji, vitongoji na mitaa.
Na akisema kuna upungufu wa asilimia 64 ya watoa huduma za afya, hivyo ni muhimu kuwatumia Watoa Huduma wa Afya Ngazi ya Jamii (CHW) ili kuimarisha huduma.
Baada ya kupata ajira, watoa huduma hao watajikita kutoa elimu ya afya kwa jamii, kutoa huduma za kinga, huduma tembezi na mkoba na huduma za awali za tiba kabla ya kumpa mgonjwa rufaa kwenda hospitali kupatiwa matibabu.
“Watoa huduma ya afya ngazi ya jamii watafanya uchunguzi wa awali wa magonjwa na kuyabaini katika hatua za awali, kutoa kinga na kuipunguzia Serikali gharama za ununuzi wa dawa ambayo kwa mwezi imefikia Shs. 200 bilioni,” akasema Dkt. Mpango.
Akasema CHW watachaguliwa kuanzia ngazi ya mitaa, vitongoji na vijiji hivyo wananchi waitumie fursa hiyo kupata ajira huku akisisitiza viongozi watakaosimamia upatikanaji wa watoa huduma hao wazingatie uadilifu na kuepuka rushwa ili wapatikane watoa huduma watakaofanikisha mpango huo wa Serikali.
Watumishi hao watakaoajiriwa watajikita kutoa elimu ya uzazi wa mpango, kubaini magonjwa ya kuambukiza na yasiyo ya kuambukiza katika hatua ya awali ndani ya jamii hasa kifua kikuu, malaria, matatizo yatokanayo na lishe, afya ya uzazi wa mama na mtoto pamoja na kuhamasisha usafi wa mazingira.
Hiki kinachofanywa na Serikali ni hatua kubwa sana ambayo itakwenda kuimarisha afya ya wananchi kwenye jamii, kwani tunafanya kazi kubwa kugundua matatizo kwa haraka na kuripoti kwa wataalamu.
Katika maagizo yake, Dkt. Mpango akazielekeza Wizara ya Afya na Ofisi ya Rais Tamisemi kuhakikisha usimamizi madhubuti wa mpango huo kwa kuweka mfumo mzuri wa uratibu na kuhakikisha taarifa za utekelezaji zinapatikana na kwamba, Wizara ya Afya ihakikishe inatoa elimu na hamasa kwa jamii kuhusu mpango huu ili kurahisisha utekelezaji wake, jamii nayo ipokee mpango huu na kuudhamini ili kulinda na kuboresha afya.
Waziri wa Afya, Ummy Ally Mwalimu, anasema kwamba watoa huduma lazima wazingatie weledi na wadau wa maendeleo waendelee kuiunga mkono Serikali katika utekelezaji wa mpango huo.
Anasema pia kwamba, CHW wamewekewa malengo ya kufikia kaya 25 kwa wiki na 100 kwa mwezi na wote watawajibika chini ya kituo cha afya kilichopo karibu nao chini ya mtendaji wa kata.
“Watoa huduma hao watawezeshwa vitendea kazi, mafunzo kwa miezi sita darasani na nje ya darasa pamoja na malipo yao kwa asilimia 100, Shirika la Globalfund litagharamia mafunzo kwa watoa huduma 500 kwa miaka mitano,” anasema Ummy.
Uamuzi huu wa Serikali unathibitisha kile kilichosemwa Oktoba 5, 2023 na Naibu Katibu Mkuu ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) anayeshughulikia afya, Dkt. Charles Mahera wakati akifunga Mkutano wa 10 wa Afya Tanzania (THS) wa siku tatu uliowakutanisha wataalamu, madaktari, watafiti na wadau mbalimbali wanaoshughulikia afya nchini.
Katika mkutano huo, Dkt. Mahera alitaja mambo manne yanayokwenda kufanyiwa kazi ambayo yaliibuliwa katika Mkutano huo, ikiwemo uwekezaji katika afya ya msingi kwa kuajiri wafanyakazi wa afya ngazi ya jamii 153,308 ili kufikia lengo la afya kwa wote.
“Haya ni maandalizi kuelekea afya kwa wote Serikali tumejipanga kuajiri kila mwaka 51,192, hivyo kwa kipindi cha miaka mitatu tutafikia lengo la kuhakikisha tunavifikia vitongoji 64,384 katika vijiji 12,300, hatuwezi kufanya peke yetu tunatoa wito kwa wadau kuongeza nguvu kushughulikia hili,” akasema.
Mahera akasema kuna umuhimu wa kuongeza nguvu na kuwekeza katika afya ya msingi kwani asilimia 85 ya Watanzania wanapata huduma katika ngazi za chini.
Jumatano, Machi 8, 2023, wakati wa Mkutano wa Kimataifa wa Mawaziri wa Afya wa Afrika uliofanyika jijini Kigali, Rwanda, kujadili mifumo endelevu na stahimilivu ya uimarishaji wa huduma za afya ikiwemo masuala ya kuwatumia wahudumu wa afya ngazi ya jamii, Waziri Ummy alisema Tanzania tayari inao Muundo wa Utumishi (Scheme of Service) unaoitambua kada ya wahudumu wa afya ngazi ya jamii na kwamba inatarajia kuajiri watumishi 15,000 kwa kipindi cha miaka mitatu 2023/2026.
Akasema, watumishi hao wataajiriwa katika kutekeleza majukumu yao kama wasaidizi wa afya (Health Assistants) ngazi ya vituo vya kutolea huduma za afya na katika ngazi ya jamii.
“Wizara yangu itajikita katika kutekeleza mpango huu kwa kuwajengea uwezo na kuwaajiri wahudumu 15,000 kwa kipindi cha miaka mitatu yaani mwaka 2023/24 hadi 2025/26 ambapo kwa kuanzia wahudumu wapatao 5,000 watapewa mafunzo kupitia vyuo vya afya vya kati kwa mwaka wa fedha 2023/24,” akasema.
Akasema wahudumu hao watatekeleza afua jumuishi ikiwemo afya ya mama na mtoto, lishe, magonjwa yasiyoambukiza, magonjwa ya mlipuko na magonjwa yanayoambukiza (VVU/Ukimwi, kifua kikuu na malaria).
Kwa ujumla, kinachofanywa na Serikali ya Rais Sami ani cha muhimu mno, kwani siyo tu anatekeleza majukumu yake kwa kuwapatia Watanzania ajira, lakini anawapelekea wananchi huduma karibu yao.