Na Daniel Mbega, Dar es Salaam
IJUMAA, Novemba 17, 2023, Katibu Mkuu wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Jokate Mwegelo, aliwatembelea wanafunzi wawili waliopata ujauzito na kuendelea na masomo yao ambao wote wamefanya mtihani wa kumaliza kidato cha nne 2023.
Na katika ziara hiyo, Jokate alitoa wito kwa wazazi na walezi kuhakikisha wanashirikiana kuwalea watoto katika misingi bora ili kuondoa uwezekano wa kuangukia kwenye hatari.
Kati ya mabinti hao, mmoja alitekelezwa na baba yao ambaye alimwacha mama yao kwa kuwa tu alikuwa amezaa watoto wa kike wakati yeye alitaka mtoto wa kiume.
Kwahiyo, mma yake, ambaye alifukuzwa bila kuambulia chochote licha ya kwamba walikuwa wamebahatika kujenga nyumba na mumewe, akakosa mwelekeo wa kuwatunza wanawe kwa kuwa hakuwa na kipato chochote, na hata mahali walipokuwa wakiishi walipewa hifadhi na wasamaria wema.
Mazingira hayo hatimaye yakamsababishia binti huyo kupata ujauzito kutokana na changamoto za ugumu wa maisha, ambapo amejifungua siku chache tu kabla ya kufanya mtihani wa kidato cha nne.
Binti mwingine yeye alijifungua miaka miwili iliyopita, lakini kisa chache hakitofautiana sana na mwenzake, kwani mama yao aliachika kwa mumewe na hakuwa na msaada wowote.
Kwa bahati mbaya, mama aliugua sana na kulazimika kwenda Arusha kupata matibabu huku binti akiachwa nyumbani peke yake bila msaada wowote huku akiwa anapaswa kwenda shule.
Binti alikuwa ndiye ajitafutie chakula na matumizi mengine. Hakuna aliyempa hata msaada wa mawazo. Matokeo yake akapata ujauzito.
Mama alirejea mwaka mmoja baadaye na kukuta binti yake ana mtoto na amechana na shule. Shukurani za pekee kwa Rais Samia Suluhu Hassan ambaye aliruhusu watoto wote waliopata ujauzito wakiwa shuleni waendelee na masomo ili kutimiza ndoto zao.
Hivi ni visa vya kuskitisha sana na ni mfano tu wa masahibu yaliyowapata mabinti wengi nchini ambao wamekatishwa ndoto zao za elimu kwa ujauzito kutokana tu na changamato zilizokuwa zikiwakumba ndani ya familia.
Mabinti hao kutoka Mbande wilayani Temeke ni miongoni mwa wanafunzi 1,907 waliopata mimba na kurejea shuleni hadi kufikia Januari 2023.
Kati ya wanafunzi hao, waliorudi katika Mfumo rasmi ni 562 na waliorejea Nje ya Mfumo Rasmi wa Elimu kupitia Mradi wa Kuimarisha Elimu ya Sekondari (SEQUIP) unaofadhiliwa na Benki ya Dunia ni 1,345.
Lakini takwimu nyingine zinaonyesha kwamba, katika kipindi cha mwaka 2022 na 2023, jumla ya wanafunzi wa kike waliorejesha shuleni baada ya kupata ujauzito na kujifungua ni 18,708 kwa shule za msingi na sekondari.
Inaelezwa kwamba, kwa mwaka 2022 wanafunzi 9,379 wa shule za msingi walirejea shuleni baada ya kujifungua huku wanafunzi wa shule za sekondari wakiwa ni 8,154 na kufanya jumla yao kuwa wanafunzi 17,532.
Aidha, mwaka 2023 wanafunzi wa kike 557 wa shule yza msingi walirejea huku wa shule za sekondari wakiwa 619 na kufanya jumla ya waliorudi shule kuwa 1,176.
Vyovyote iwavyo, idadi hii ya watoto waliorejea shuleni inatia moyo kwa maana watoto hawa wanapata nafasi nyingine ya kutimiza ndoto zao zilizokuwa zimetoweka.
Lakini ni idadi inayotisha kwa kuwa watoto hawa ni wengi, achilia mbali idadi isiyojulikana ya wale ambao hawakurudi shule.
Mnamo Novemba 24, 2021, Serikali, kupitia kwa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako, ilitaka ruksa ya watoto waliopata ujauzito wakiwa shuleni kurudi darasani kuendelea na msomo.
Na mnamo Novemba 29, 2021, Rais Samia akasema kwamba, fursa ya kurudi shule inawahusu wanafunzi wote waliopata changamoto za elimu huku akieleza kuwa wanafunzi wa shule za msingi wanaopata mimba wanaweza kuchagua kurudi shuleni au kwenda katika elimu mbadala kwa lengo la kutimiza ndoto zao.
Kiongozi huyo mkuu wa nchi akasema wanafunzi waliopata ujauzito wakiwa shule za msingi wana uchaguzi wa kurudi shule katika mfumo rasmi au kwenda katika elimu mbadala ikiwemo mafunzo ya ufundi stadi.
“Kwa kawaida mtoto wa kike akishakua mama, kama amekuwa mama darasa la sita hatarudi tena darasa la sita kuendelea na shule, hiyo ndiyo kawaida,” alisema Rais wakati wa uzinduzi wa Shule ya Msingi Museveni iliyopo Chato mkoani Geita.
“Si kawaida, tuna mifano mizuri nchi nyingine zimefanya hivyo, Zanzibar wamefanya hivyo. Na kawaida wote ambao wamepata (ujauzito) wakiwa msingi hawarudi shule wanakwenda kwenye mkondo mbadala,” akasisitiza Rais huku akitaka mijadala kuhusu suala hilo ijikite katika misingi hiyo.
Baadhi ya wanaharakati na wadau wa elimu walikuwa wakishinikiza wanafunzi wanaopata mimba wakiwa shule za msingi au sekondari waruhusiwe kurudi katika mfumo rasmi kwa sababu ni haki yao kuelimika.
Kuhusu wanafunzi watakaopata mimba wakiwa sekondari, Rais Samia alisema; “lakini wale wanaopata bahati mbaya wakiwa sekondari wale wanarudi na wanarudi wanaendelea na masomo yao vizuri, wengine wanafika mpaka chuo kikuu.”
Kwa muda mrefu sasa Serikali ilikuwa imepiga marufuku kwa wanafunzi waliopata ujauzito kurejea shuleni baada ya kujifungua.
Msimamo huo wa Serikali ulichagizwa zaidi Juni 2017 baada ya Hayati Rais Dkt. John Magufuli kupiga marufuku wanafunzi wanaopata mimba mashuleni kuendelea na masomo ya shule ya msingi na sekondari akisema ndani ya utawala wake hakuna mwanafunzi aliyepata mimba na angeruhusiwa kurudi shuleni.
Lakini Rais Samia akasema kwamba, suala la kurudi shule haliwahusu wanafunzi waliopata mimba pekee bali wanafunzi wote walioacha shule kwa sababu mbalimbali ikiwemo utoro, ujauzito na nidhamu ili kutoa fursa kwa watoto wa Tanzania kupata elimu.
Akasema Serikali imejipanga vizuri kuhakikisha utekelezaji wa uamuzi wa kuwarudisha wanafunzi shuleni huo hauathiri sekta ya elimu nchini.
Hata hivyo, ruksa iliyotolewa na Rais Samia isiwe sababu ya wazazi na walezi kusahau wajibu wao wa malezi, kwani kwa kuangalia kwa undani, asilimia kubwa ya watoto waliopata ujauzito chanzo ni malezi hafifu ya wazazi, migogoro katika ndoa na jamii kushindwa kuwajibika kwa ujumla wake.
Hali inasikitisha sana wakati tunapopewa takwimu hizi, na inaonyesha dhahiri kuwa kuna kasoro mahali fulani kwenye jamii.
Ni wakati sasa kwa wazazi na walezi kuhakikisha wanawasaidia watoto wao katika malezi sahihi, kwani kuwaacha ‘wakjichunge’ wenyewe kunawaweka hatarini.