Hawa Ndio Marais ‘Wezi’ Duniani

Na Daniel Mbega na Mashirika

TAASISI ya Transparency International kupitia Bribe-Payers Index ilieleza kwamba, Mobutu Seseko wa ‘Zaire’, Mohammed Suharto wa Indonesia na Ferdinand Marcos wa Ufilipino kwa pamoja walifisidi nchi zao jumla ya Dola 50 bilioni, kiasi ambacho kwa wakati huo kilikuwa sawa na bajeti nzima ya mwaka ya misaada kutoka nchi wahisani.

Ripoti ya TI iliyoonyesha orodha ya wanasiasa mafisadi zaidi wa miongo miwili iliyopita inaonyesha kwamba anayeongoza ni dikteta wa Indonesia, Mohammed Suharto, lakini ripoti hiyo ikasema kwamba hakuna nchi ambayo iko salama kwa rushwa na ufisadi, huku ikibainisha ufadhili wa kisiasa nchini Ugiriki, uhusiano wa karibu kati ya makampuni kadhaa na utawala wa familia ya Bush wa Marekani na utawala usio wa upinzani wa aliyekuwa waziri mkuu wa Italia, Silvio Berlusconi.

Lakini ufisadi mkubwa zaidi umetokea katika nchi zinazoendelea, ambako viongozi wamekomba rasilimali za mataifa yao na kujilimbikizia mali.

Suharto alikomba takriban Dola 35 bilioni katika kipindi cha utawala wake wa miongo mitatu kabla ya kufukuzwa wakati ambapo Mobutu yeye alichota nusu ya Dola 12 bilioni za misaada ambazo zilitolewa na Shirika la Fedha Duniani (IMF) kwa kipindi chote cha utawala wake na kuifanya nchi hiyo ibaki na madeni makubwa hadi sasa.

Ndiyo maana Ijumaa ya Mei 16, 1997 mara tu baada Laurent Desire Kabila kuipindua serikali ya mwanahabari Mobutu Sese Seko Kuku Ngbendu Wa Za Banga nchini Zaire, alitangaza kutaifisha mali zote za dikteta huyo aliyeitawala kwa mkono wa chuma nchi hiyo ya pili kwa ukubwa barani Afrika kwa miaka 32.

Siku moja baadaye, yaani Jumamosi Mei 17, 1997 serikali ya Uswisi nayo ikatangaza kuzuia mali za Mobutu kwa kipindi cha mwaka mmoja baada ya kupokea maelekezo kutoka kwa utawala mpya wa Kabila, ambaye wakati huo alikuwa ameweka makao yake makuu jijini Lubumbashi.

Mali zilizozuiliwa kufuatia uamuzi wa serikali ya Uswisi ni pamoja na hekalu lake lenye vyumba 300 lililokuwa eneo la Savigny pembezoni mwa ziwa huko Lausanne, ambalo kwa wakati huo thamani yake ilikuwa yapata Dola 5 milioni. Hili lilikuwa miongoni mwa vitegauchumi vyake vingi tu barani Ulaya ambako ilielezwa kwamba vyote kwa pamoja vilikuwa na thamani ya takriban Dola 37 milioni kwa wakati huo.

Ingawa kulikuwa na taarifa kwamba Mobutu, ambaye jina lake la ubatizo aliitwa Joseph-Desiré Mobutu, alikuwa ameficha karibu Dola 4 bilioni, lakini serikali ya Uswisi ilichunguza katika benki zote 400 nchini humo na haikuona fedha zozote zilizowekwa kwa jina lake au jina la wanafamilia wake.

Mobutu, ambaye alithubutu kulipa Dola 10 milioni kwa mabondia Muhammad Ali na George Foreman (Dola 5 milioni kila mmoja) ili wakapigane jijini Kinshasa Oktoba 30, 1974, hakuona shida yoyote kutumia fedha hata kwenda kufanya ‘shopping’ Ulaya na ndiye rais pekee Afrika kutumia midege mikubwa na ghali zaidi duniani, Concorde.

Mwaka 1989, Mobutu alikodi ndege ya Concorde yenye namba za usajili F-BTSD kutoka Shirika la Ndege la Ufaransa (Air France) kwa ajili ya safari ya Juni 26– Julai 5 kwenda tu kutoa hotuba kwenye Mkutano wa Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani, Julai 16 akakodi ndege hiyo kwenda Paris, Ufaransa kuhudhuria sherehe za nchi hiyo baada ya kualikwa na Rais François Mitterrand, Septemba 19 akakodi dege hilo kutoka Paris hadi mjini Gbadolite, Zaire na safari nyingine ya moja kwa moja kutoka Gbadolite hadi jijini Marseille akiwa na kwaya ya vijana wa Zaire.

Kwa kutumia fedha za Wazaire, aliamua kujenga uwanja maalum mjini Gbadolite, kaskazini mwa nchi hiyo ambako ndiko alikotokea, ili kuliwezesha dege la Concorde litue na kuruka.  Uwanja huo uliokuwa kwenye kilele cha meta 460 kutoka usawa wa bahari, njia yake ya kurukia ilikuwa na urefu wa meta 3,200 (kilometa 3.2) na upana wa meta 60.

Hata hivyo, ukiangalia katika orodha hiyo ya Transparency International, majina yaliyomo ni ya viongozi ambao walikuwa wakilindwa na kukingiwa kifua na Mataifa ya Magharibi ambayo yalifumba macho kutokana na vitendo vilivyokuwa vikifanywa na watawala hao kama namna ya mabadilishano wakati wa Vita Baridi.

Suharto, ambaye alifahamika kwamba ni mpinzani wa ujamaa barani Asia, alikwiba takriban Dola 35 bilioni kutoka kwenye nchi hiyo wakati wa utawala wake wa kidikteta kwa miongo mitatu, kabla hajang’olewa mwaka 1998 katika vurugu kubwa zilizoibuka kufuatia mdororo wa uchumi barani Asia.

Alishtakiwa kwa kukomba Dola 500 milioni kutoka serikalini kupitia taasisi mbalimbali zilizoongozwa na familia yake, lakini majaji wakasema alikuwa mgonjwa hivyo hakustahili kusimama mahakamani.

Marcos, ambaye mkewe alikuwa na jozi 3,000 za viatu alikuwa msamiati maarufu kutokana na rushwa aliyoitenda wakati wa utawala wake, lakini alikuwa kipenzi cha Marekani na hawakuwahi kumnyoonyeshea kidole.

Jitihasa za kuzisaka Dola 10 bilioni alizokwiba wakati wa utawala wake wa miaka 20 hazikuweza kuzaa matunda na zilivurugwa kutokana na sheria kali za kibenki nchini Uswisi. Mnamo Agosti 2003, miaka 14 baada ya kifo chake, mahakama za Uswisi hatimaye ziliamuru Dola 657 milioni za dikteta huyo zilizofichwa nchini humo zirudishwe kwa serikali ya Ufilipino.

Mobutu alitumia hil na vitisho kwamba angeweza kuivamia serikali ya Angola iliyokuwa na mrengo wa Marxist ili kuwanyamazisha watawala wa mataifa ya magharibi wasimnyooshee kidole kuhusu namna alivyokuwa anaiba rasilimali za taifa lake ambalo linaongoza kwa kuwa na madini mengi barani Afrika.  Marekani iliishawishi IMF iendelee kuipatia Zaire mikopo, licha ya mashaka makubwa waliyokuwa nayo maofisa wa IMF dhidi ya utawala wa dikteta Mobutu.

Mpaka anapinduliwa mwaka 1997, Mobutu alikuwa ameiba karibu nusu ya Dola 12 bilioni za misaada ambazo Zaire ilipata kutoka IMF wakati wa utawala wake wa miaka 32, akiiacha nchi yake ikiwa na mzigo mkubwa wa madeni.

Ripoti ya Global Financial Integrity (GFI) ya mwaka 2008 ilionyesha kwamba kumekuwa na ongezeko la kiasi cha fedha kinachotoroshwa katika nchi mbalimbali duniani kutoka Dola za Marekani 1.06 trilioni za mwaka 2006 hadi kukaribia Dola 1.26 trilioni za mwaka 2008.

Katika kiasi hicho cha fedha, wastani wa Dola 725 bilioni hadi 810 bilioni zilitoroshwa kwa mwaka tangu mwaka 2000 hadi 2008 kutoka katika nchi zinazoendelea.

Ripoti hiyo inaonyesha pia kwamba, Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini, zinaongoza kwa asilimia 24.3, nchi zinazoendelea za Ulaya asilimia 23.1, Afrika asilimia 21.9 na Asia asilimia 7.85.

Katika ripoti hiyo, nchi 10 zinazoongoza duniani kwa kuwa na kiwango kikubwa cha fedha kilichotoroshwa kati ya mwaka huo 2000 hadi 2008 na kiasi katika mabano ni China (Dola 2.18trilioni), Russia (Dola 427bilioni), Mexico (Dola 416 bilioni), Saudi Arabia (Dola 302bilioni), Malaysia (Dola 291bilioni), Umoja wa Falme za Kiarabu (Emirates, Dola 276 bilioni), Kuwait (Dola 242bilioni), Venezuela (Dola 157bilioni), Qatar (Dola 138bilioni) na Nigeria (Dola 130bilioni).

Ifuatayo ndiyo orodha ya marais ‘wezi na mafisadi’ zaidi duniani katika kipindi cha miongo 20 iliyopita;

Mohammed Suharto
Taifa – Indonesia, 1967-98
Kiasi – Dola15bn hadi 35bn

Ferdinand Marcos
Taifa – Ufilipino, 1972-86
Kiasi – Dola 5bn hadi 10bn

Mobutu Sese Seko
Taifa – Zaire, 1965-97
Kiasi – Dola 5bn

Sani Abacha
Taifa – Nigeria, 1993-98
Kiasi – Dola 2bn hadi 5bn

Slobodan Milosevic
Taifa – Serbia, 1972-86
Kiasi  – Dola 1bn

Jean-Claude Duvalier
Taifa – Haiti, 1971-86
Kiasi – Dola 300m hadi 800m

Alberto Fujimori
Taifa – Peru, 1990-2000
Kiasi – Dola 600m

Pavlo Lazarenko
Taifa – Ukraine 1996-97
Kiasi – Dola 114m hadi 200m

Arnoldo Alemán
Taifa – Nicaragua, 1997-2002
Kiasi – Dola 100m

Joseph Estrada
Taifa – Ufilipino, 1998-2001
Kiasi – Dola 78m hadi 80m

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *