Gamondi: Ratiba mwishoni mwa mwaka ngumu

Na Badrudin Yahaya

KOCHA wa timu ya Yanga SC, Miguel Gamondi, amesema ratiba yao kuelekea mwisho wa mwaka sio nzuri lakini watajitahidi kupambana ili kupata matokeo chanya.

Kauli hiyoayo ameitoa akiwa mkoani Dodoma wakati kikosi chake kikijiandaa kukabiliana na Tabora United kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara utakaopigwa kesho kwenye Uwanja wa Jamhuri.

Gamondi amesema ratiba ni ngumu kwasababu wanahitajika kucheza mechi kila baada ya siku tatu kitu ambacho sio rahisi kwa kawaida.

“Ratiba inatubana, tunalazimika kucheza mechi kila baada ya siku tatu, ni ngumu lakini inabidi tupambane ili kupata matokeo mazuri,” amesema.

Aidha kocha huyo amebainisha hali ya Uwanja wa Jamhuri ambao watautumia kwa ajili ya mchezo wa dhidi ya Tabora kwamba sio nzuri na haitoi fursa kwa timu yake kucheza soka wanalohitaji.

Katika hatua nyingine, Kocha huyo, amesema kwenye mchezo wa kesho wataendelea kumkosa mchezaji wa Joyce Lomalisa kutokana na majeraha.

Kocha huyo amedai walitarajia Lomalisa angerudi mapema uwanjani lakini hadi sasa anaonekana kutokuwa tayari hivyo nafasi yake itaendelea kuzibwa kikosini hadi atakapokuwa fiti.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *