FIFA yazifungia Kitayosce, Fountain Gate kusajili

Na Asha Kigundula

KLABU ya Kitayosce ya Tabora, iliyopanda Ligi Kuu Tanzania Bara, imefungiwa kusajili wachezaji na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) kwa kosa la kutomlipa Kocha Mmisri, Ahmed El Faramawy Soliman.

Mbali na timu hiyo, pia Fountain Gate inayocheza Ligi ya Championship imefungiwa kusajili.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Dar es Salaam jana na Ofisa Habari wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), uamuzi huo umefanywa na FIFA baada ya Soliman kushinda kesi za madai dhidi ya klabu hizo.

Kocha huyo alizifundisha timu hizo kwa nyakati tofauti, alifungua kesi FIFA akipinga kuvunjiwa mikataba kinyume cha taratibu.

“Baada ya Soliman kushinda kesi, klabu hizo zilitakiwa zime zimemlipa ndani ya siku 45 tangu uamuzi huo ulipotolewa, lakini hazikutekeleza hukumu hizo,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Wakati FIFA ikizifungia klabu hizo kufanya uhamisho wa wachezaji wa kimataifa, TFF imezifungia kufanya uhamisho wa wachezaji wa ndani.

TFF inazikumbusha klabu kuheshimu mikataba ambayo zimeingia na wachezaji pamoja na makocha ili kuepuka adhabu mbalimbali ikiwemo kufungiwa kusajili.

Kama klabu inataka kuvunja mkataba na mchezaji au kocha, inatakiwa kufanya hivyo kwa kuzingatia taratibu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *