FAO kumuunga mkono Samia mikakati ya kilimo

Rome, Italia

SHIRIKA la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo (FAO), limeahidi kuunga mkono jitihada za Serikali ya Tanzania inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Sulihu Hassan katika kukuza, kuendeleza sekta ya kilimo.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alisema hayo juzi jioni baada ya ufunguzi wa Mkutano wa Jukwaa la Kimataifa la Chakula Duniani ulioanza Oktoba 16-20, 2023.

Majaliwa alihutubia mkutano huo kwa niaba ya Rais Dkt. Samia na kueleza kuwa, Serikali ya Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zina mipango ya kuifanya Tanzania kuwa mzalishaji mkubwa wa chakula ndani ya nchi na ziada kuuza nje ifikapo 2030.

Kabla ya ufunguzi wa mkutano huo ulioshirikisha wakuu wa nchi na serikali, majaliwa alishiriki Maadhimisho ya miaka 78 tangu kuanzishwa kwa FAO.

“Zipo jitihada zilizowekwa nchini kwa kushirikisha vijana, wanawake kuhakikisha tunaongeza teknolojia, kutumia mbolea kwenye kilimo, ushirikishaji wa sekta binafsi, FAO wameahidi kutuunga mkono,” alisema.

Alisema serikali imeendelea kuimarisha miundombinu mbalimbali ikiwemo ujenzi wa reli ya kisasa, barabara, nishati vijijini ili kurahisisha shughuli za kilimo.

“Maboresho mengine ni ujenzi wa viwanda vya kuzalisha pembejeo za kilimo na kuhamasisha wakulima kutumia teknolojia za kisasa katika uzalishaji,” aliongeza.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa FAO, Dkt. Qu Dongyu alisema Tanzania ina fursa kubwa ya kuendeleza sekta ya kilimo na uchumi wa buluu.

Shirika hilo liko tayari kushirikiana na Tanzania kutoa msaada wa kitaalam, kukuza mifumo ya uzalishaji chakula.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *