Fainali za CRDB Bank Supa Cup 2024 zawa kivutio Arusha

Na Mwandishi Wetu

FAINALI za mashindano ya CRDB Bank Supa Cup 2024, zimefikia tamati mwishoni mwa wiki jijini Arusha huku zikikonga nyoyo za mashabiki wengi wa michezo nchini kutokana na ushindani uliokuwepo.

Mashindano hayo yalishirikisha michezo ya soka na netiboli huku timu mbalimbali kutoka kanda tofauti za Tanzania zilishiriki katika fainali hizo ambazo zilileta burudani, mshikamano na ushindani mkubwa.

Akizungumza katika fainali hizo, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela, amesema benki hiyo imeweka mikakati na sera mbalimbali za kuongeza chachu kwa wafanyakazi wake na michezo ni mojawapo ya nyenzo muhimu katika kuhakikisha wanajenga umoja, afya njema na furaha miongoni mwao.

“Mashindano ya CRDB Bank Supa Cup ni zaidi ya michezo, ni jukwaa la mshikamano, mawasiliano na afya bora kwa wafanyakazi wetu. Tunajivunia kuona mashindano haya yakiendelea kuwa sehemu muhimu ya utamaduni wa benki yetu,” amesema Nsekela.

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela (kulia), akishuhudia utoaji wa zawadi za michezo mbalimbali wakati wa kuhitimisha fainali za mashindano ya CRDB Bank Supa Cup 2024 zilizofanyika mwishoni mwa wiki jijini Arusha.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Rasilimali Watu, Godfrey Rutasingwa, amesisitiza umuhimu wa mashindano hayo katika kuongeza mshikamano miongoni mwa wafanyakazi.

“Michezo huchangia kwa asilimia kubwa kuwaleta watu pamoja na kupitia Supa Cup tumeweza kuona mshikamano wa kipekee kati ya wafanyakazi wetu kutoka kanda mbalimbali,” amesema Rutasingwa.

Mashindano ya CRDB Bank Supa Cup 2024 yamehitimishwa kwa mafanikio makubwa huku timu ya iMbeju kutoka Kanda ya Pwani iking’ara kwa kushinda vikombe vyote vya soka na netiboli.

Shangwe na matarajio yameanza kuandaliwa kwa mashindano ya mwakani huku wafanyakazi na mashabiki wakiisubiri kwa hamu kubwa msimu ujao wa burudani.

Katika mchezo wa soka kutafuta mshindi wa tatu, timu ya Ulipo Tupo FC kutoka Kanda ya Ziwa, imeibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Boom Advance FC kutoka Kanda ya Kaskazini na kuzawadiwa sh. 6,000,000.

Fainali ya soka imeshuhudia timu ya iMbeju FC kutoka Kanda ya Pwani ikiibuka kidedea kwa ushindi mnono wa mabao 4-0 dhidi ya Al Barakah FC kutoka Kanda ya Magharibi. Ushindi huu umeifanya iMbeju FC kutwaa ubingwa wa CRDB Bank Supa Cup 2024 na kuzawadiwa sh. 13,000,000 huku Barakah ikipata sh. 9,000,000.

Kwa upande wa netiboli, nafasi ya tatu imechukuliwa na Lipa Hapa Queens kutoka Kanda ya Dar es Salaam baada ya kuwashinda Popote Inatiki Queens kutoka Kanda ya Kati kwa alama 50-45 na kuzawadiwa sh. 4,000,000.

Fainali ya netiboli imewaweka uso kwa uso iMbeju Queens kutoka Kanda ya Pwani na Ulipo Tupo Queens kutoka Kanda ya Ziwa. iMbeju Queens walishinda kwa alama 45-39 na hivyo kutwaa ubingwa wa netiboli na kuvuna sh. 9,000,000 huku Ulipo Tupo Queens ikipata sh. 6,000,000 .

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *