Ewura yaeleza sababu kushuka bei ya mafuta

Na Salha Mohamed, Dar es Salaam

MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imesema mabadiliko ya bei za mafuta kwa Desemba 2023 yaliyoonesha kupungua kwa bei yanatokana na bei za mafuta (FOB) kwenye soko la dunia kupungua mwezi huu kwa wastani wa asilimia 0.86 kwa mafuta ya petroli na silimia 9.11 kwa mafuta ya dizeli.

Pia gharama za kuagiza mafuta (premium) kwa Bandari ya DSM zimepungua kwa wastani wa asilimia 24 kwa mafuta ya petroli na asilimia 30 kwa mafuta ya dizeli.

Mkurugenzi Mkuu EWURA, Dkt. James Mwainyekule alisema kuwa sababu nyingine ni kupungua kwa gharama za kuagiza mafuta (Premium) kwa Bandari ya Tanga kwa asilimia 30 kwa mafuta ya petroli na asilimia 17 kwa mafuta ya dizeli.

Alisema pia mabadiliko hayo yanatokana na kupungua kwa bei za mafuta ghafi katika soko la dunia kwa wastani wa asilimia asilimia 8.72 na gharama za uagizaji wa mafuta kwa wastani wa asilimia 27 kwa petroli asilimia 23 kwa dizeli.

Aidha bei hizo kwa mwezi uliopita kwa Mkoa wa Dar es Salaam bei ya rejareja petrol ilikuwa ikiuzwa Shs. 3,274 na sasa sh 3,158, Dizel Shs. 3,374 na sasa itauzwa Shs. 3,226.

Alisema, Bandari ya Mtwara haikupokea shehena ya mafuta Mabadiliko ya bei za mafuta kwa Desemba 2023 yanatokana na kupungua kwa bei za mafuta ghafi katika soko la dunia kwa wastani wa asilimia asilimia 8.72 na gharama za uagizaji wa mafuta kwa wastani wa asilimia 27 kwa petroli na asilimia 23 kwa dizeli.

“EWURA inapenda kuwakumbusha wafanyabiashara wa bidhaa za mafuta kwa jumla na rejareja pamoja na jamii kuzingatia bei kikomo za bidhaa za mafuta ya petroli kwa eneo husika zinapatikana kupitia simu za mkononi kwa kupiga namba *152*00# na kisha kufuata maelekezo.

Alisema kwa mujibu wa Sheria ya Mafuta ya mwaka 2015, kifungu namba 166, bei za bidhaa za mafuta ya petroli zitaendelea kupangwa na soko.

“EWURA itaendelea kuhamasisha ushindani kwa kutoa taarifa za bei kikomo za bidhaa za mafuta. Kampuni za mafuta ziko huru kuuza bidhaa za mafuta ya petroli kwa bei ya ushindani isipokuwa bei hizo zisizidi bei kikomo (Price cap) au kuwa chini ya bei iliyoruhusiwa (Floor Price) kama zilivyokokotolewa kwa mujibu wa Kanuni za EWURA za Kupanga Bei za Mafuta za Mwaka 2022 zilizotangazwa tarehe 28 Januari 2022 kupitia Gazeti la Serikali Na. 57 na marekebisho ya kanuni tajwa kupitia Gazeti la Serikali Na. 761A la tarehe 30 Oktoba 2023,”alisema.

Alisema vituo vyote vya mafuta vinatakiwa kuchapisha bei za bidhaa za mafuta katika mabango yanayoonekana bayana yakionesha bei za mafuta, punguzo, vivutio vya kibiashara vinavyotolewa na kituo husika. Pale ambapo inawezekana kuchagua, wateja wanashauriwa kununua bidhaa za mafuta katika vituo vinavyouza mafuta kwa bei nafuu zaidi ili kushamirisha ushindani.

“Ni kosa kuuza mafuta bila kuweka mabango ya bei inayoonekana vizuri kwa wateja. Adhabu kali itatolewa kwa kituo husika kwa kutotekeleza matakwa ya kisheria kwa mujibu wa kanuni husika.

“Wauzaji wa bidhaa za mafuta ya petroli wanatakiwa kutoa stakabadhi za mauzo kutoka kwenye Electronic Fiscal Pump Printers (EFPP) na wanunuzi wahakikishe wanapata stakabadhi hizo za malipo zinazoonyesha jina la kituo, tarehe, aina ya mafuta yaliyonunuliwa na bei kwa lita,” alisema.

Alisema, Stakabadhi hizo zitatumika kama kidhibiti kwa wanunuzi wa mafuta endapo kutajitokeza malalamiko ya kuuziwa mafuta kwa bei ya juu kuliko bei kikomo au kuuziwa mafuta yasiyo na kiwango cha ubora unaotakiwa.

Stakabadhi hizo pia zitasaidia kurahisisha ukusanyaji wa kodi za Serikali zitokanazo na mauzo ya bidhaa za mafuta ya petrol.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *