- Yasema mgawo wa umeme utakwisha Machi
- Yasisitiza matumizi ya gesi kwenye magari
Na Daniel Mbega,
Dar es Salaam
MAMLAKA ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura) imesema kwa kushirikiana na Wizara ya Nishati na idara nyingine, inaendelea kutekeleza maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha mgwo wa umeme nchini unakwisha kufikia Machi 2024.
Hayo yameelezwa leo Jumatatu, Novemba 6, 2023 na Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Dkt. James Andilile, katika kikao kazi baina ya mamlaka hiyo na Wahariri wa Vyombo vya Habari nchini.
Dkt. Andilile alisema, licha ya changamoto zilizopo, lakini Serikali inaendelea kuzikabili na kuhakikisha kwamba upatikanaji wa nishati ya umeme unatengemaa, kwani hayo ni maisha ya wananchi.
“Ni kweli zipo changamoto, lakini changamoto hizi haziwezi kuondoka ukweli kwamba Serikali inatekeleza mambo mengi kuhakikisha wananchi wanapata huduma stahiki.
“Sisi, kwa kushirikiana na Wizara tunaendelea kujitahidi kuhakikisha kwamba umeme unapatikana bila mgawo ifikapo Machi 2024 kama alivyoagiza Mheshimiwa Rais,” alisema.
Alisema kwamba, mwaka 2015 uzalishaji wa umeme nchini ulikuwa megawati 1,400 ambapo asilimia 65 ya Watanzania walikuwa wameunganishwa na nishati hiyo.
Akaongeza kwamba, kwa sasa uzalishaji umefikia megawati 1,900, ukihusisha umeme uliokokwenye Gridi ya Taifa nan je ya Gridi, huku asilimia 78 ya Watanzania wakiwa wameunganishwa.
“Kwa mwaka 2015 mahitaji yalikuwa megawati 980 lakini sasa mahitaji ni megawati 1,400. Kwa ujumla, mahitaji yanaendelea kuongezeka na tunajitahidi kuhakikisha kwamba vyanzo mbalimbali vya kuzalisha umeme vinaimarika,” alisema.
Alibainisha kwamba, ongezeko la watumiaji wa nishati ya umeme limechangiwa pakubwa na Programu ya uunganishaji umeme vijiji (REA) ambapo mpaka sasa zaidi ya vijiji 10,000 kati ya 12,000 nchini kote vimekwishaunganishwa huku vilivyosalia vikitarajiwa kuunganishwa ifikapo mwishoni mwa mwaka 2024.
Dkt. Andilile alisema, katika kuhakikisha upatikanaji wa umeme wa uhakika, Serikali inaendelea kukamilisha miradi mikubwa ya uzalishaji umeme ukiwemo wa Julius Nyerere huko Rufiji utakaozalisha megawati 2,115 ambao umefikia asilimia 92 kwa sasa.
Mradi huo wa JNHPP unatarajiwa kukamilika mwaka 2024, ambapo kukamilika kwake kutaondoa kero ya mgawo wa umeme nchini.
Aliitaja miradi mingine kuwa ni wa Kinyerezi 1 unaotakiwa kuzalisha megawati 185 ambapo kwa sasa unazalisha megawati 180, na mradi wa umeme wa maji wa Rusumo utakaozalisha megawati 87 zitakazogawanywa katika nchi tatu za Tanzania, Burundi na Rwanda, ambao kwa sasa umefikia asilimia 99.
Matumizi ya gesi asilia
Dkt. Andilile alisema, Serikali inaendelea na mkakati wa kuhakikisha wananchi wanatumia gesi asilia, ambapo Tanzania ina akiba ya futi za ujazo trilioni 57.54 zilizothibitishwa.
“Ili kuleta unafuu wa maisha kwa wananchi, Serikali imeona ni vyema ikatumia nishati inayopatikana nchini kwa gharama nafuu, na utumiaji wa gesi asilia utawakomboa wengi na kuwapunguzia mzigo wa gharama za mafuta hasa ya dizeli na petrol,” alisema.
Alimshukuru Rais Samia kwa kuwezesha ujenzi wa Mradi wa Usindikaji Gesi Asilia (LNG) mkoani Lindi ambao ulikuwa umekwama, akisema hatua hiyo itachochea maendeleo ya uchumi wa taifa.
Mradi huo wa Mtambo wa LNG unatarajiwa kugharimu takriban Dola za Marekani milioni 40, ambapo mbali na gesi hiyo kutumika nchini, lakini pia inaweza kusafirishwa nje ya nchi.
Dkt. Andilile alisema, tangu gesi asilia ilipoanza kutumika mwaka 2002, mpaka sasa kuna viwanda 54 vinavyotumia gesi hiyo na kuachana na mafuta mazito ya kuendeshea mitambo ambayo yalikuwa yakiongeza gharama za uendeshaji na kupandisha bei ya bidhaa.
“Kuna taasisi saba, ikiwemo Hoteli ya Serena, ambazo zinatumia gesi asilia, lakini kuna wananchi wa kawaida 5,011 wanatumia nishati hiyo huku mgari 3,758 yakiwe yamefungwa mfumo wa gesi asilia (NCG) badala ya mifumo ya petrol na dizeli,” alisema.
Hata hivyo, alihimiza Watanzania wanaomiliki magari kubadili mifumo na kutumia gesi asilia ambayo gharama yake ni nafuu sana kulinganisha na dizeli na petrol.
Aidha, alisema kwamba, mpaka sasa kuna vituo vitatu vinavyotoa huduma ya kujaza gesi kwenye magari yenye mfumo huo ambavyo ni TPDC-Pan African cha Ubungo Maziwa na Aric Tanzania jijini Dar es Salaam vinavohudumia magari 350 kwa siku na kituo cha Mtwara-Dangote kinachohudumia magari 250 kwa siku, yakiwemo magari ya Dangote yaliyofungwa NCG Tanker.
Alisema, kituo cha Taqa Dalbit-Airport kinatarajiwa kukamilika na kuzinduliwa kabla ya mwisho wa mwezi Novemba, wakati ambapo Dangote amepewa kibali cha kujenga kituo kingine Mkuranga mkoani Pwani.
Aidha, TPDC imepewa kibali cha kujenga vituo vitatu ambavyo ni Mlimani City, Muhimbili na Kibaha, huku Taqa Dalbit wakiwa wamepewa kibali cha kujenga kituo kingine kwenye Barabara ya Sam Nujoma – Mawasiliano.
Mnamo Machi 2, 2023, Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) lilisema jumla ya vituo tisa (9) vya kujaza gesi asilia kwenye magari vinatarajia kujengwa na kukamilika katika kipindi cha miezi 24.
Ilielezwa kwamba, wananchi wamekuwa na mwitikio mkubwa wa kuweka mifumo ya gesi asilia kwenye magari kiasi kwamba vituo vilivyopo vinaonekana kuzidiwa na ili kutatua changamoto hiyo zipo jitihada mbalimbali ambazo TPDC inaendelea kuzifanyia kazi ambapo hadi sasa kampuni zipatazo 20 zimepewa leseni ya kujenga vituo vipya katika maeneo mbalimbali.
Aidha, katika azma hiyo ya kuongeza vituo nchini, TPDC itajenga Kituo Kikuu (Mother station) katika maeneo ya Mlimani City chenye uwezo wa kuhudumia magari sita kwa wakati mmoja pamoja na malori sita ya kubeba CNG kwa ajili ya kupeleka katika vituo vidogovidogo.
Taarifa zinasema, Kampuni ya Turky Petroleum itajenga kituo eneo la Bagamoyo, Kampuni ya Anric itajenga eneo la Mkuranga, Kampuni ya BQ itajenga kituo eneo la Goba pia Kampuni ya Dangote itajenga eneo la Mkuranga.
Uwepo wa Vituo hivi vyote vitasaidia kutatua changamoto za ujazaji wa gesi asilia kwenye magari.
Suala la mafuta
Dkt. Andilile alisema, suala la ununuzi wa pamoja wa mafuta ya petrol linaendelea kutekelezwa ambao jumla ya kampuni 18 ndizo hushindanishwa kwenye zabuni.
Alisema, utaratibu huo unasaidia Serikali kujua akiba ya mafuta iliyopo na mahitaji, ingawa alisema wapo baadhi ya waagizaji mafuta ambao si waaminifu wanaoficha nishati hiyo ili kusubiri bei ipande kwa mwezi unaofuata.
Hata hivyo, alisema kwamba, kwa sasa, kwa kuwa wanazo rekodi zote za kiasi cha mafuta kilichopo, wameweka kanuni za kupanga bei ya wastani kwa mafuta yanayobakia yanapochanganywa na yale yanayokuja kwa mwezi unaofuata ili kuwapa unafuu walaji.
Dkt. Andilile alisema pia kwamba, wanaendelea kutekeleza maagizo saba waliyopewa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Dotto Biteko, ikiwemo kuimarisha mfumo wa uagizaji wa mafuta na kuangalia upya gharama za uagizaji wa pamoja.
Alisema ushiriki wa kampuni katika zabuni ni mdogo ambapo wakati mwingine zinazoshindani zabuni ni kati ya tano na nane tu kati ya 18, hivyo wamerekebisha kanuni ambapo kuanzia sasa, kampuni isiyoagiza mafuta katika kipindi cha miezi mitatu itafutiwa leseni.
Awali, kampuni hizo zilikuwa zinakaa hata miezi sita ndipo zinaagiza mafuta, hali ambayo Dkt. Andilile alisema, inaathiri uagizaji kwa kuwa kampuni hizo huchaguliwa kutokana na vipengele vya premium.