Dough Works yaongeza ajira 800 kwa kufungua tawi jipya

Na Mwandishi Wetu

KAMPUNI ya Dough Works Limited (DWL), imeongeza zaidi ya nafasi 800 za ajira kwa Watanzania kupitia mtandao wake unaopanuka wa migahawa ya KFC.

Haya yamebainishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Dough Works Limited, Vikram Desai, wakati wa uzinduzi wa tawi la 12 la KFC lililopo Shekilango, kwa ushirikiano na TotalEnergies Tanzania.

Desai amesema ufunguzi wa tawi hilo jipya ni sehemu ya dhamira endelevu ya chapa ya KFC ya kutoa huduma bora na za kisasa za chakula kwa jamii mbalimbali nchini. Alieleza DWL inajivunia kuchangia soko la ajira kwa msaada wa serikali.

“Ushirikiano huu na TotalEnergies unaakisi dhamira yetu ya pamoja ya ubora na upatikanaji wa huduma. Uwepo wetu Ubungo siyo tu kwa ajili ya chakula kizuri bali pia kwa ajili ya kuleta ajira, kuinua jamii na kubadilisha maisha ya kila siku,” amesema Desai.

Amefafanua Tawi la KFC Shekilango linawawezesha wateja kupata chakula wanachokipenda kwa urahisi katika mazingira ya kisasa yanayoendana na viwango vya kimataifa vya ubora na huduma vinavyohusishwa na chapa ya KFC.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa TotalEnergies, Mamadou Ngom, Mkurugenzi wa Mtandao wa Kampuni hiyo, Abdul Rahim Siddique, amesema ushirikiano na Dough Works ni hatua nyingine muhimu katika safari ya ukuaji, ushirikiano na mafanikio ya pamoja kati ya kampuni hizo mbili.

Ameongeza mpango huo ni sehemu ya mkakati mpana wa kuboresha huduma kwa wateja kwa kuchanganya ubora, ufanisi na faraja katika kila hatua.

“Tunajivunia kushirikiana na DWL ili kutoa huduma bora zaidi kwa wateja nchini. Tawi hili jipya litaongeza thamani kubwa kwa wateja wetu,” amesema Siddique.

Wakati huohuo, Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Albert Msando, amezipongeza kampuni zote mbili kwa kuongeza nafasi za ajira na kuahidi kuwa ofisi yake itaendelea kushirikiana nao katika shughuli zao za kibiashara.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *