-Awakosoa kushindwa kufanya maandalizi uchaguzi serikali za mitaa
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
MWANASIASA mkongwe na aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Balozi, Dkt. Wilbroad Slaa, ameshangazwa na viongozi wa chama hicho kushindwa kufanya maandalizi ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vitongoji na Vijiji.
Dkt. Slaa ameonya kuwa kwenda kulalamika kwa mataifa ya Magharibi kuhusu mchakato na matokeo ya uchaguzi kutawafanya wajiulize maswali magumu kuhusu maandalizi yao hafifu.
Kauli ya Dkt, Slaa ameitoa jana katika mahojiani maalum aliyofanya na chombo cha habari kuhusu mwenendo wa chama hicho katika kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa.
Aidha, amemkosa Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika, kwa kushindwa kutoa maelekezo ya wazi kwa viongozi wa ngazi za chini na wadau wa chama na kusababisha kukwama kwa maandalizi ya uchaguzi huo.
Dkt. Slaa alitilia mkazo umuhimu wa chama hicho kuwa na mikakati ya kuwajengea uwezo wananchi, akieleza kuwa kwa muda mrefu wananchi wa Tanzania hawajawahi kupewa mwongozo madhubuti wa kujitegemea katika harakati za kisiasa.
“Usitegemee wananchi wawe mstari wa mbele, wanahitaji kuongozwa… Chadema mliwajengea uwezo? upi? Kama mliwajengea uwezo wamefika wakashindwa kutekeleza, wananchi wajibu wao nini?” alihoji Dkt. Slaa, akisisitiza kuwa ni jukumu la viongozi wa kisiasa kuwaongoza wananchi na kuwapa moyo wa kusimama kidete kwaajili ya haki zao.
Dkt. Slaa alitoa mfano wa matukio mbalimbali ya siku za karibuni likiwamo tukio la Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha) kuchoma vitenge vilivyokuwa vimetolewa kama zawadi na Rais Samia Suluhu Hassan. Tukio kama hilo ni ishara ya namna chama kimeshindwa kuleta ushawishi wa kutosha kwa wananchi.
“Kwenye suala hili kwa mfano la kuchoma kanga na vitenge, wananchi hawakumualika Rais Samia, nyinyi ndiyo viongozi mliomualika, mlikwenda kama chama kwenda kumbana Samia kwamba ulitupa zawadi, sasa leo tunataka kuchoma hizi zawadi na mkachoma mbele yake? Wananchi mtawaingiza kwenye matatizo tu bila sababu,” amesema Dkt. Slaa na kuongeza,
“Wananchi wana jukumu lao, wananchi mliwaomba kwenye maandamano wametokea. wananchi wanahitaji kupewa ujasiri na kauli za vyama vya upinzani juu ya maandamano zilitokaje?”
Aidha, amezungumzia suala la maridhiano akilitaja kuwa halikuwa shirikishi kwasababu walikaa kwenye meza moja na serikali katika mchakato wa maridhiano bila kuwa wazi kwa wananchi.
Dkt. Slaa amedau kitendo cha viongozi wa chama kukaa na serikali kimya kimya kiliwafanya wananchi kuendelea kukosa ujasiri wa kushiriki kikamilifu katika harakati za kisiasa.
“Leo unategemeaje wananchi walipuke wakati nyinyi wenyewe mlikuwa mnakaa meza moja na serikali mkinywa juisi… Vitendo vile vilifanya wananchi waendelee kulala,” amesema Dkt. Slaa.
Amesema chama kilipaswa kuwa na mikakati ya wazi na madhubuti ya kushirikiana na wananchi ili kuongeza hamasa katika kudai haki.
Pia, Dkt. Slaa ameeleza kuwa chama kinachotaka kushinda na kuongoza lazima kiwe na mbinu nyingi na za kisasa za kufanikisha malengo yake.
Amehoji kama Chadema imewahi kuwa na mbinu zaidi ya 1,000 kama ambavyo chama tawala, Chama Cha Mapinduzi (CCM), hujigamba kuwa nacho.
“CCM wana mbinu 1,000, nyinyi CHADEMA mna ngapi? Mliwahi kutoka hadharani kutuambia?” amehoji Dkt. Slaa.
Ni ishara nyingine kwamba Chadema, badala ya kutengeneza mipango ya kushindana kidemokrasia, wanaendelea kujificha nyuma ya kelele za malalamiko na hoja zisizo na msingi, huku wakiwaacha wanachama na wafuasi wao katika mkanganyiko na kukata tamaa.