Dkt Samia: Tusishawishike kuivuruga amani ya nchi

Na Mwandishi Wetu, Kilimanjaro

MGOMBEA urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt Samia Suluhu Hassan amewakata Watanzania wasishawishike kuivuruga amani katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu, huku akiwahakikishia usalama siku hiyo.

Amesema wanaoshawishi kuivuruga amani, familia zao zina makazi nje ya Tanzania, hivyo wanafanya hivyo kwa sababu wanapo pa kukimbilia.

Dkt Samia alitoa kauli hiyo wilayani Hai, mkoani Kilimanjaro jana, alipozungumza na wananchi wa eneo hilo, katika moja ya mikutano yake wa kampeni za urais, uliohudhuriwa na maelfu ya wananchi.

Alisema wananchi wasikubali kushawishiwa, kwani kufanya hivyo kutasababisha waharibu amani ya nchi.

“Msikubali kushawishiwa tukaharibu amani ya Tanzania. Msikubali hata kidogo. Wanaoshawishi wanapo pa kwenda.

“Familia zao haziko hapa. Wapo wao kuja kufanya fujo, kukikorogeka wakimbie wakaungane na familia. Sisi tunakwenda wapi? Ni hapa hapa Tanzania,” alisema Dkt Samia.

Aliambatanisha ujumbe huo na hakikisho la kuwepo kwa usalama siku ya uchaguzi, akisisitiza vyombo vya ulinzi na usalama vimejipanga vema.

“Ninawahakikishia usalama, vyombo vya ulinzi vimejipanga vema, tutakuwa salama. Lakini na ninyi wananchi mtunze usalama,” alisema.

Alisema kila anayetoka nyumbani kwake siku ya uchaguzi ahakikishe anawashawishi wenzake kwenda kupiga kura, huku viongozi nao wawajibike kushawishi wananchi wa maeneo yao kwenda kupiga kura.

“Tukipiga kura kwa wingi, tukiinyanyua CCM kwa wingi, wale wanaoitazama Tanzania kwa jicho jingine, wataweka heshima sawasawa,” alisema Dkt Samia.

Anayojivunia

Dkt Samia alisema katika miaka mitano iliyopita, Serikali yake imeimarisha ushirika na kuinua sekta ya kilimo cha mazao mbalimbali ikiwemo kahawa.

Kwa mujibu wa Dkt Samia, juhudi hizo zimechochea kupanda kwa bei ya kilo moja ya kahawa, kutoka Sh4,000 hadi Sh12,000 inayouzwa sasa kutoka kwa wakulima.

Mbali na zao la kahawa, alisema Serikali yake imekuza na kulea ushirika na kuuondoa katika mtazamo wa kuwa chaka la wizi na unyang’anyi kwa wakulima, sasa umegeuka kuwasimamia.

“Tumeujenga ushirika leo, tunaamini kuuachia ugawaji wa pembejeo za mbolea na pembejeo nyingine. Ushirika unafanya hiyo kazi na unagawa kwa wakulima wenzao,” alisema.

Alieleza kwa sababu ushirika unaaminika sasa, amesema anatarajia kuukabidhi viwanda mbalimbali nani imani yake kuwa vitaendelezwa vema.

Mengine yaliyofanywa kwenye kilimo, alisema ni kujengwa kwa skimu za umwagiliaji na kutengeneza fursa kwa vijana kupitia mradi wa Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT).

“Miaka mitano iliyopita tumefanya kazi kweli kweli na kwa maana hiyo, napata ujasiri wa kusimama mbele yenu kuomba kura za CCM,” alisema.

Aahidi barabara Kilimanjaro

Aliahidi kuboresha na kujenga barabara za Mkoa wa Kilimanjaro ili kurahisisha usafiri na usafirishaji wa mizigo na abiria, kadhalika kuiunganisha mikoa ya Tanzania.

“Kipaumbele chenu wananchi wa Kilimanjaro na kote nilikopita ni miundombinu ya barabara. Hapa Moshi Mjini tutajenga barabara ya mchepuko ya Kae hadi uwanja ndege yenye urefu wa kilomita 31,” alisema.

Alisema fedha zimeshatengwa za ujenzi wa barabara ya kilomita 10 kupitia mradi wa uendelezaji wa miji utakaotekelezwa mji wa Moshi.

Kwa Moshi Vijijini, aliahidi kukamilisha barabara za Moshi International School-Kibosho Kati kwa Rafael yenye urefu wa kilomita 13.

“Lakini pia barabara ya Kidia-Urisini yenye kilomita 10, barabara ya Mamboleo- Shimbwe kilomita 10.3, barabara ya Rau-Madukani-Mamboleo- Materuni kilomita 10, barabara ya Samanga-Chemchem kilomita 10.

“Barabara zote zinajengwa na zimefikia katika hatua mbalimbali, tunakwenda kuzikamilisha kwa kiwango cha lami,” alieleza.

Alieleza kwa upande wa Jimbo la Vunjo, Dkt Samia ameahidi kukamilisha barabara za Pofu- Mandaka- Kilema yenye urefu kilomita 10 ambayo ni tegemeo la wananchi na watalii wanaoshuka Mlima wa Kilimanjaro.

Katika jimbo hilo hilo, Dkt Samia aliahidi kukamilisha ujenzi wa barabara ya kipekee, Uchira- Kisomachi ambayo wananchi walianza mchakato huo kwa nguvu zao, kisha Serikali ikaongeza nguvu.

Dkt Samia hakuiacha Same, alikoeleza tatizo hasa milimani ambako nyakati za mvua maji yanashuka chini, akiahidi timu ya watalaamu kufanya utafiti kisha ujenzi wa barabara wa kiwango cha lami ngumu utafuata.

“Kule Rombo tutakamilisha ujenzi wa barabara ya kimkakati ya kukuza biashara mpakani kati ya jirani zetu Kenya kupitia barabara ya Horiri- Tarakea yenye kilomita 53,” alisema.

Kuhusu wananchi wa Moshi Vijijini wanaosifika kwa kulima kahawa, Dkt Samia aliwaahidi kuwaanzisha vituo vya ukodishaji wa zana bora za kilimo ili kuwawezesha kufanya kilimo chao kwa gharama nafuu zaidi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *