
Na Mwandishi Wetu, Arusha
MKOA wa Arusha ni miongoni mwa maeneo yatakayonufaika na Mradi wa Reli ya Kisasa (SGR), utakaotekelezwa katika kipindi cha miaka mitano ijayo chini ya Serikali ya Dkt Samia Suluhu Hassan.
Kwa mujibu wa Rais Dkt. Samia ambaye pia ni Mgombea urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), ujenzi wa kipande hicho cha SGR, utaanzia katika Bandari ya Tanga, kisha Arusha hadi Musoma.
Dkt. Samia ametoa kauli hiyo leo, Alhamisi Oktoba 2, 2025 katika hotuba yake kwa wananchi wa Arusha Mjini, mkoani Arusha, wakati wa mkutano wake wa kampeni za urais uliohudhuriwa na maelfu ya wananchi.
Sio SGR pekee, amesema katika Mkoa wa Arusha kutajengwa kituo kikubwa cha reli hiyo, kinachotarajiwa kuzalisha fursa kwa wananchi wa Jiji hilo.
“Lakini kwa sababu Arusha ni Mji mkubwa, lazima kutakuwa na kituo kikubwa hapa kwa reli ile kituo ambacho kitaleta tena fursa za ajira na wafanyabiashara, pia vijana wetu wa Arusha,” amesema Dkt Samia.




