
Na Mwandishi Wetu, Arusha
MGOMBEA urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt Samia Suluhu Hassan ametoa hakikisho la kuwapo kwa usalama siku ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu, akisisitiza vyombo vya ulinzi na usalama vimejipanga vema.
Ameambatanisha hakikisho lake hilo na nasaha kwa Watanzania, kujitokeza kwa wingi kupiga kura siku ya uchaguzi, ili kujenga hadhi ya nchi dhidi ya wale wanaoitazama vibaya.
Dkt. Samia ametoa kauli hiyo, leo Jumatano Oktoba 1, 2025 alipozungumza na wananchi wa Hai, mkoani Kilimanjaro, katika mkutano wake wa kampeni za urais.
“Ninawahakikishia usalama, vyombo vya ulinzi vimejipanga vema, tutakuwa salama. Lakini na ninyi wananchi mtunze usalama,” amesema.
Amesema kila anayetoka nyumbani kwake siku ya uchaguzi ahakikishe anawashawishi wenzake kwenda kupiga kura, huku viongozi nao wawajibike kushawishi wananchi wa maeneo yao kwenda kupiga kura.
“Tukipiga kura kwa wingi, tukiinyanyua CCM kwa wingi, wale wanaoitazama Tanzania kwa jicho jingine, wataweka heshima sawasawa,” amesema Dkt Samia.
