
• Aahidi uchaguzi wa amani na salama
• Asisitiza hakuna ‘nywinywi’ wala ‘nywinywinywi‘
Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
MGOMBEA urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewasihi wananchi wasikubali kuchokozwa na wakachokozeka na hatimaye kuivuruga amani ya nchi, katika uchaguzi.
Msingi wa kauli yake hiyo ni kile alichoeleza, mara kadhaa wenye nia ovu, hutumia nyakati za uchaguzi kuchokozana ili kusababisha vurugu na kuharibu amani ya nchi, akisisitiza Watanzania wasikubali kuchokozeka.
Dkt. Samia ametoa kauli hiyo leo Septemba 20/2025, alipozungumza na wananchi wa Gombani visiwani Pemba, alipokwenda kwa ziara ya kampeni za uchaguzi wa urais.
Amesema katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, Serikali yake imejitahidi kusimamia utulivu wa kisiasa, usalama na amani ndani ya nchi.
Katika kipindi hicho, amesema hazikusikika kashikashi zozote, zaidi ya matukio ya ajali na hata waliofanya majaribio ya kuivunja amani walishughulikiwa na kudhibitiwa.
“Niwaombe sana ndugu zangu, kipindi hiki ni kipindi wengine wanakitumia kuchokozana. Niwaombe msichokozeke, msichokozeke kuweni kama mimi mama yenu, dada yenu, bibi yenu, ndugu yenu, nachokozwa sana lakini sichokozeki.”
“Kwa hiyo niwaombe sana msichokozeke. Tusivunje amani kwa sababu ya uchaguzi hapana… akiumia mmoja imeumia familia, akiumia mmoja familia yote itahangaika,” amesisitiza.
Katika hoja hiyo, amewataka Watanzania wasikubali kuvunja amani kwa sababu ya uchaguzi, akidokeza wananchi wote ni wamoja.
Ameeleza hatafurahia kuona mtu yeyote kutoka eneo lolote ameumizwa kwa kipigo, hivyo wananchi wote wajitahidi kutunza amani na utulivu.
Aidha, amewatoa hofu wananchi kuwa, siku ya kupiga kura hakutakuwa na vurugu kwa kuwa vyombo vya ulinzi na usalama vimejipanga vema kuilinda nchi, hivyo wananchi wajitokeze kwa wingi kwenda kupiga kura.
“Na mimi ndiye Amiri Jeshi Mkuu ninayesema hapa. Tumejipanga vema kuilinda nchi hii kwa hiyo hakutakuwa na nywinywi waka nywinywinywi, kwa hiyo watu jitokezeni mkapige kura,” amesema.
Ameeleza wananchi wanapaswa kujitokeza kwa wingi hata kwenye kupiga kura kama wanavyoendelea kujitokeza wakati wa mikutano ya kampeni.

Kuhusu madai ya upinzani
Dkt. Samia alitumia hotuba hiyo, kugusia malalamiko ya vyama vya upinzani, akisema hakuna hata moja lisilozungumzika, hivyo anahitaji nafasi zaidi kukaa na kuyazungumza ili kuona namna ya kuiendesha Zanzibar.
“Lakini tusiende kuvunja amani, kwa sababu tuliwaambiwa hayakufanyika hapana. Naomba kila mtu awe mlinzi wa mwenziwe. Tutaweka historia tukafanyeni kazi yetu, tupige kura, rudi nyumbani subiri matokeo. Aliyepata kapata aliyekosa ajipange kwa miaka mitano ijayo,” amesema Dkt Samia.

CCM ni vitendo
Katika hotuba yake hiyo, Dkt. Samia amesema Serikali ya CCM imejikita katika vitendo zaidi, badala ya maneno, akitumia msemo wa ‘Ada ya mja kunena, muungwana ni vitendo.
“Serikali za CCM, ile ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ya Mapinduzi Zanzibar vyetu ni vitendo na wala sio blaa blaa… sisi vyetu ni vitendo,” amesema.
Dkt Samia amesema Serikali ya Zanzibar imefanya kazi kubwa ya kusimamia na kutekeleza miradi yote ambayo alikuwa anashirikiana naye kuitafuta na hatimaye kufanikisha utekelezwaji wake.
Ameeleza ushahidi wa makubwa yaliyofanyika, ni mabadiliko anayoyashuhudia kila wakati anaposafiri kwenda visiwani Pemba.
Amesema kwa kutumia njia za kidiplomasia mazingira yameandaliwa, makontena yanayoleta bidhaa visiwani humo, yanashusha mizigo moja kwa moja Pemba, badala ya Unguja kama ilivyokuwa zamani.
Jambo jingine lililotekelezwa, amesema, ni kuweka miundombinu ya maji ili kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma.
“Tupo kazini kufanya maji yawe kipaumbele chetu kila mwananchi apate maji safi na salama saa zote 24 kwa wiki nzima,” amesema Dkt Samia.
Amesema kwa njia za kidiplomasia, wamefanikisha kuomba mashindano ya AFCON yafanyike katika nchi za Tanzania, Kenya na Uganda na hivyo miundombinu ya michezo imeboreshwa.
Kuhusu viwanda, amesema katika miaka mitano iliyopita viwanda vimeongezwa na kuajiri vijana wa Pemba. Viwanda hivyo ni vya Mwani, Karafuu na Maji.
Amerejea historia ya alivyowahi kuwatembelea visiwa hivyo, mwaka 2022, ikiwa ni mwaka mmoja tangu alipoapishwa kuwa rais na alipata fursa ya kuzungumza na wazee wa eneo hilo.
Ameeleza miongoni mwa mambo waliyomweleza ni kuhusu hali ngumu ya uchumi katika visiwa hivyo, lakini suala la kuzingatia amani na utulivu wakati wa uchaguzi, na kuwa ahidi kuwa masuala hayo yanashughulikiwa.

Uhusiano wake na Pemba
Katika hotuba yake hiyo, alisema alisoma Pemba katika eneo la Ziwani, wakati huo baba yake akiwa mwalimu katika moja ya shule za msingi visiwani humo.
Mbali na kusoma shule ya msingi, alisema pia aliwahi kufanya kazi kwa zaidi ya mwaka mmoja katika eneo la Pemba, kabla ya kuhamia katika maeneo mengine.
“Mimi bwana ni Mpemba mwenzenu, Pemba oyeeeee…! Mara ya mwisho nilikuja Pemba kula futari na ndugu zangu, sasa mara hii nimekuja kwa shughuli maalumu ya kuomba kura,” amesema.
Amesema Serikali zote zinafanya kazi kwa karibu ili kukabiliana na changamoto za kidunia na kukamilisha miradi mbalimbali ya maendeleo.
“Tutaendelea kushirikiana, umoja wetu, muungano wetu huu maana yake tufanye kazi pamoja, tushirikiane pamoja kama ni maendeleo tuendelee pamoja na kama matatizo tukabiliane nayo pamoja,” amesema Dkt Samia.


