Dkt. Samia akata kiu mradi LNG

Na Mwandishi Wetu, Lindi

MGOMBEA urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt Samia Suluhu Hassan, amewakata kiu Watanzania, akiahidi mradi wa uchakataji na usimikaji gesi asilia mkoani Lindi (LNG), uko mbioni kutekelezwa.

Kwa mujibu wa Dkt Samia, Serikali yake ipo katika hatua za mwisho za mazungumzo na mwekezaji, kwa ajili ya pande hizo mbili kusaini mikataba na hatimaye mradi uanze kutekelezwa na kuwanufaisha wananchi wa Lindi na Tanzania kwa ujumla.

Hatua ya Dkt. Samia kutekeleza mradi huo, itavunja mwiko wa mkwamo wa miaka 12 katika utekelezaji wa mradi huo. Mara kadhaa mazungumzo yameishia njiani au pande mbili kutoafikiana.

Mradi huo, wenye thamani ya zaidi ya Sh. trilioni 70 unatarajiwa kuzalisha fursa za ajira 13,000 za moja kwa moja na hivyo kukuza vipato vya wananchi na Taifa kwa ujumla.

Hakikisho la kutekelezwa kwa mradi huo, limetolewa leo, Alhamisi Septemba 25, 2025 na Dkt Samia alipozungumza Lindi Mjini, katika mkutano wake wa kampeni za urais, uliohudhuriwa na maelfu ya wananchi.

“Natambua kiu yenu kubwa na ya Watanzania kwa ujumla ni kuona mradi wa gesi asilia ya kimiminika yaani NLG wa kule Mchinga,” amesema.

Amesema mradi huo unagharimu Dola za Marekani 40 bilioni hivyo anayewekeza anapaswa kuwa na uhakika wa faida kutokana na uwekezaji wake.

“Anayewekeza lazima awe na uhakika wa fedha yake anayokuja kuweka hapa itamzalishia kitu gani. Lakini na sisi tunaoletewa mradi lazima tuwe na uhakika mradi huu tutapata nini kutokana na rasilimali yetu inayokwenda kutumika,” amesema.

“Tumekuwa na mizunguko ya mazungumzo ndugu zangu, tumezungumza sana kwa miaka miwili, sasa tunakaribia kukubaliana, tupo hatua za mwisho za kukubaliana,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *